Header Ads

LightBlog

MAANDALIZI YA VURUGU UNGUJA NA PEMBA




Mategemeo, subira bila mafao Pemba


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI mtu mzima, nyumbani kwake na familia yake, aambiwe na mgeni jinsi ya kuvaa vizuri, kulea watoto, kuweka nyumba yake katika hali ya usafi, kutafuna polepole na kutoacha mdomo wazi wakati anapopiga miayo.

Mtu mzima atang’aka na kuuliza iwapo ni wewe umekuwa ukimwelekeza kwa miaka yote hadi kufikia umri huu wa miaka 50. Atakushangaa. Aweza kukujibu kwa hamaki na hasira.

Ndivyo ilivyokuwa mwishoni mwa wiki. Marafiki wa serikali za Muungano wa Tanzania na Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BMZ), waliona serikali hizi zinataka kupiga miayo bila kuweka kiganja mdomoni. Wakazibonyeza: Tahadhari!

Mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Ulaya, Marekani, Japan na Canada wamezitaka serikali za Muungano na BMZ kuwa makini na demokrasi. Hii inafuatia hatua ya kusimamisha zoezi la kuhakiki daftari la wapigakura kisiwani Pemba, wiki mbili zilizopita, baada ya milipuko miwili ya mabomu katika makazi ya wananchi.

Katiba ya Zanzibar inazingatia kuwa kila raia ana haki ya kupiga na kupigiwa kura. Vigezo vya raia vipo. Lakini sheria ya uchaguzi inaongeza matakwa mengine, kuwa kila anayetaka kujiandikisha kupiga kura sharti awe na hati ya ukazi Zanzibar.

Kwa wiki mbili sasa kumekuwepo migongano kisiwani Pemba. Siyo kwamba wote wanapinga kuwepo matakwa ya hati ya ukazi, bali hata wenye hati wanadai kuwa wamekuwa hawaandikishwi au kuhakikiwa.

Ukazi umekuwa ukazi. Hivi kitambulisho kuwa ulipiga kura uchaguzi uliopita hakitoshi? Hivi kuwa na kitambulisho cha uraia kwa misingi ya ulipozaliwa, kukulia na bado unaishi hapo hakutoshi? Hivi ilikuwa lazima vitambulisho vya ukazi vitakiwe hivi sasa wakati wa uhakiki wa daftari; kwa nini kazi hiyo haikufanywa mapema?

Tayari kuna madai ya wananchi kwamba wamekwenda kwenye vituo wakiwa na hati ya ukazi, hati ya kupigia kura uchaguzi uliopita na vyeti vya kuzaliwa, lakini wakakataliwa kuhakikiwa. Hapa ndipo penye utata.

Madai mengine ni kwamba kuna waliokwenda vituoni, bila hati ya ukazi, bila hati ya kuzaliwa, bila hati ya kupiga kura katika uchaguzi wowote uliopita, lakini wakapokewa na kuhakikiwa. Wananchi wanajiuliza: Huu ni mradi maalum wa serikali, upendeleo maalum na wa makusudi au ngekewa?

Kwa hiyo, kabla serikali haijasimamisha uhakiki katika daftari la kupiga kura, tayari kulikuwa na makundi hapa na pale; yakijadili hali hii. Utata unazidi inapokuwa Pemba ni ngome ya chama kikuu cha upinzani Visiwani – Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa kuzingatia ushindi wa asilimia 100 wa CUF katika uchaguzi mkuu uliopita kisiwani Pemba, kila sehemu ya kisiwa hicho ni ngome ya chama hicho. Hatua yoyote ile basi, ya kuweka taratibu ngumu au zenye utata katika kuhakiki majina ya wapigakura, itafikiriwa kuwa inalenga kuhujumu CUF.

Katika mazingira ambamo hakuna maelezo ya serikali yanayoeleweka juu ya chanzo cha milipuko ya mabomu; na kutokana na milipuko hiyo kuwa ndani ya ngome ya chama cha upinzani, tayari kuna madai kuwa milipuko ililenga kutishia wapigakura wa upande wa upinzani.

Kwa kuwa milipuko ya mabomu imefanya watu watawanyike na kukimbilia mafichoni; yawezekana wengi wasirudi kujiandikisha kupiga kura. Inawezekana wengine wakaja wakati wa kujiandikisha umeisha au wakachukia na kukata tamaa kwa kuwa siasa imeingiliwa na tishio kwa maisha yao.

Yote haya yakifanyika, haitakuwa kwa manufaa ya chama kikuu cha upinzani au hata vyama vidogo. Yaweza kuwa faida kuu kwa chama kilichoko ikulu ya Zanzibar. Kwa ufupi, inaweza kueleweka kuwa kura za wananchi tayari zimepigwa mabomu.

Katikati ya hali hii mabalozi wa Ulaya, Marekani, Canada na Japan wamesema kuwa hawafurahishwwi na hali kama ilivyo Kisiwani Pemba. Hilo tu, kwamba “Ndugu yangu, ziba kidogo mdomo wakati wa kupiga miayo.”

Kauli ya mabalozi tayari imeleta kizaazaa. Serikali ya Muungano imejibu kwa kusema iliishawaonya mabalozi wasiingilie mambo ya ndani ya nchi; huku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikisema mabalozi wamevuka mpaka.

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) nao umekuja juu, mwenyekiti wake Hamad Masauni Yusuf Masauni akisema kuwa Tanzania iliishatoka kwenye ukoloni na kwamba “mabalozi wafanye kazi zilizowaleta nchini.”

Ni kauli kali zisizojibu hoja ya mikingamo katika uhakiki wa daftari la wapigakura kisiwani Pemba. Ni kali lakini ambazo sharti zitolewe ili kujikakamua ingawa wote waliosema wanajua kuwa mataifa hayo ni wabia wa serikali, tena kwa muda mrefu.

Vyovyote itakavyokuwa, tayari zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka kesho, limeingia doa. Kwa mtindo huu, inawezekana madoa mengi yataingia hata kabla siku ya kudondosha karatasi katika sanduku la kura.

Bali jambo moja ni muhimu hapa. Serikali, pamoja na ukali wake na kauli nyingine ambazo zinaweza kuwa zinakiuka itifaki, zinaelewana vema na wafadhili. Ukiangalia kwa undani utaona vema kwamba wanasikika kupingana lakini hawatupani.

Kinachofanyika ni kutaka kuonekana kuwa waliona jambo likifanyika; walihisi siyo sahihi; walilitolea kauli kwamba hawakufurahishwa; lakini mambo yanakwenda kama wanaoyafanya wanavyopenda. Hiyo ndiyo “itifaki.” Hakuna malumbano zaidi wala kukabana shingo.

Kama kuna aliyetegemea kauli za mabalozi kutikisa lolote katika mazingira ya sasa Pemba na huenda Unguja na Bara, anashauriwa avute pumzi. Kile ambacho mataifa haya wabia wa serikali wanaonekana wanaweza kufanya, huwa hakifanywi au kinafanywa kwa njia isiyofikia kubadilisha maamuzi.

Kwani ni mataifa haya ambayo utasikia yamekwishaahidi au tayari yametoa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya shughuli za uchaguzi nchini – katika hali yoyote ile ambamo utakuwa umeandaliwa na watawala. Hatimaye watatangaza uchaguzi kuwa huru na wa haki.

Imekuwa hivyo siku zote. Itakuwa hivyo mwaka huu na mwaka kesho. Anayetaka mabadiliko katika msimamo wa mataifa ya nje kuhusu suala hili, atasubiri sana. Na kunakucha, kunakuchwa.

Sharti nguvu ya mabadiliko itoke kwa wanaoumia pindi wanapoweka mguu chini. Kuna mwiba. Kama unachoma, basi uondoe. Wanaoona unachechemea huenda wakadhani siku hizi una mikogo. Chukua hatua.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii ilichapishwa katika Tanzania Daima Jumapili, toleo la 16 Agosti 2009)

No comments

Powered by Blogger.