Header Ads

LightBlog

KUSAJILI SIMU ZA MKONONI NI UHALIFUBADALA YA KUVUMBUA WANADIDIMIZA TEKNOLOJIANa Ndimara Tegambwage

SITAKI mpango wa kusajili wamiliki wa simu za mkononi na namba zao kama serikali inavyotaka na kama inavyoshinikiza.

Hii ni kwa kuwa sababu zilizotolewa na serikali; na kusisitizwa na Mamlaka ya Udhibiti ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); zile ambazo zinatumiwa kuhalalisha usajili; siyo za msingi na hazina mashiko.

Serikali ina maoni kuwa simu za mkononi zinatumiwa vibaya. Inadai zinatumiwa kufanya uhalifu. Kwamba zinarahisisha mawasiliano ya wale wanaopanga uhalifu.

Uhalifu unaotajwa ni pamoja na kutukana, kupanga wizi na, au hujuma; kutoa vitisho kwa watu mbalimbali; kutoa taarifa za upotoshaji na wakati wote huo bila muhusika kufahamika.

Inadaiwa kuwa namba na wamiliki wakisajiliwa, itakuwa rahisi kujua nani ametoa taarifa, uzushi, vitisho; na kupitia namba ipi ya simu. Serikali inafikiri kwa njia hii, kazi yake ya “ulinzi wa amani” itakuwa imerahisishwa.

Hii ina maana kwamba serikali na wenye makampuni ya kutoa huduma za simu za mkononi, wamekula njama. Wamekubaliana kuingilia mawasiliano ya wananchi na labda wamekuwa wakifanya hivyo, tena kwa kiwango kikubwa.

Uhalifu hauletwi na simu. Uhalifu hauletwi na siri katika mawasiliano. Vyombo vya mawasiliano ni mifereji ya kupitishia taarifa. Unahitaji mawasiliano mapana kukabili uhalifu.

Katika mazingira ambamo waliopewa jukumu la kuzuia uhalifu ndio wenyewe wanaofanya uhalifu; unahitaji vyanzo vya siri vya kuibua uhalifu. Pale penye uhalifu unaofanywa na watawala na wateule wao, unahitaji mifereji isiyo bayana.

Katika mazingira ambamo aliyeibua uhalifu anatendewa kama mhalifu; na wakati mwingine jina lake kuwekwa wazi kwa wahalifu – wawe wakwapuzi wa mabilioni benki, wauza dawa za kulevya au majambazi yaliyokubuhu – unahitaji mifereji ya mawasiliano isiyo bayana.

Tujenge hoja kuwa mtu asiyejulikana, ambaye amekupelekea simu ya vitisho kupitia namba ya simu isiyojulikana ya nani, basi ameshindwa kutekeleza anachotaka. Tumuone kama anayetishia tu.

Bali inawezekana akawa anatishia kweli. Hapo atakuwa ametoa onyo; amekupa muda wa kujipekua na kujiandaa. Simu hiyo pia yaweza kukupa fursa ya kuacha kile ulichokuwa ukifanya na ambacho tayari wengine wameona hakifai au kinawadhuru.

Katika mazingira ya Tanzania, taarifa juu ya kifo cha mahabusu ambaye maofisa wa magereza hawataki kijulikane, inapatikana kwa mfereji wa siri wa mawasiliano – simu isiyoweza kutambulika.

Orodha za wahalifu walioko serikalini, karibu sana na watawala wakuu, inafikia vyombo vya habari kwa njia ya simu ya siri. Maagizo ya siri ya kuumba au kuua, yanapatikana kwa njia ya namba ya simu isiyosajiliwa.

Kilio cha wananchi wakazi wa Kilosa, mkoani Morogoro na Ololosakwani, mkoani Arusha juu ya unyama wanaotendewa, kinafikia vyombo vya habari, watawala na dunia nje ya nchi, kwa njia ya simu isiyopekuliwa.

Dereva wa mbunge ambaye hajalipwa mshahara wake kwa miezi sita, anatumia namba isiyosajiliwa kuwasiliana na vyombo vya habari na hata spika wa bunge ili angalau kilio chake kiweze kusikika na yeye apate kushughulikiwa.

Hayo ndiyo matakwa ya mazingira ya sasa. Dereva akijulikana kuwa analalamika, basi anafukuzwa kazi. Karani akifahamika kuwa “amevujisha” majina ya wezi idarani, anafukuzwa kazi palepale.

Ofisa Utumishi akijulikana kuwa hakushirikishwa katika ajira ya watoto wa bosi wake, siyo tu atafukuzwa kazi; aweza kuundiwa kosa kubwa hata la kufikishwa mahakamani.

Mfugaji wa Kilosa na Ololosakwani akijulikana kuwa ni yeye aliyepeleka taarifa za askari wa FFU kuchoma nyumba zao na kutesa wananchi, huenda “akapotezwa” katika mazingira ya kutatanisha.

Tetesi nyingi kwa vyombo vya habari, watumishi makini na waaminifu ndani ya serikali, taasisi zake na hata makampuni na mashirika binafsi; zinapatikana kwa mifereji ya siri, kwa kuwa “uwazi” limekuwa neno tupu la wanasiasa na halimo katika utendaji.

Tetesi hizi zimekuwa muhimu kwa hatua za kwanza za uchunguzi. Wakati aliye karibu aweza kukuona na kuongea nawe, aliye mbali anapata fursa ya kukupa taarifa bila wasiwasi wa kuchukuliwa hatua na wale wanaodaiwa kutenda uhalifu.

Aidha, wakati baadhi ya waandishi wa habari wamesahau au wamedharau msingi muhimu wa “kutunza chanzo cha taarifa,” baadhi wametaja majina ya waliowapa taarifa na kuwaweka hatarini.

Simu ambazo haziwezi kuingiliwa ni nyenzo kuu ya wananchi na wafanyakazi waliomo katika karakati za kupigania uhuru na haki zao. Watapanga jinsi ya kukutana hadi jinsi ya kufanya walichopanga.

Asasi za kijamii zilizomo katika ushawishi ainaaina, huweza kutumia njia hii ya simu isiyo wazi ili taarifa zisivuje, hadi hatua ya mwisho iliyolengwa na kufanya hoja zao kuibuka kwa kishindo na labda kupatikana kwa mafanikio yaliyotarajiwa.

Uhalifu hauletwi na simu za mkononi ambazo namba zake na wamiliki hawajulikani kwa watawala. Nyenzo hii ya mawasiliano ya teknolojia ya kisasa inaweza kutumiwa na mkweli au mwongo; mtiifu au mwasi; mwaminifu au mkora, “mungu” au “shetani.”

Aliwahi kusema Karl Marx, kuwa uhalifu ni tasnia pana inayoajiri kuanzia mtu wa kada ya chini kabisa kama mesenja hadi profesa wa masuala ya jinai. Hapa kuna hoja ya “uendelevu.”

Kadri jamii zinavyopita katika nyakati tofauti za maendeleo na kuingia na kutoka katika ustaarabu tofauti, ndivyo zinavyokumbana na matatizo mapya na changamoto mbalimbali.

Mlango wa kusumumiza hautoshi kuziua mwizi. Chomeko siyo tena chombo cha ulinzi. Kofuli haifai tena kulinda nyumba. Magrili yanatawanywa kwa moto wa gesi.

Kukua kwa maarifa ya kuhudumia jamii kunaenda sambamba na uvumbuzi katika tasnia ya uhalifu. Huwezi kuzuia hili. Lakini serikali inakwenda mbali. Inafikiri kuwa simu ambazo haijui ni za nani, zinaleta au zinachochea uhalifu(!?) Huu ni udhaifu mbaya.

Badala ya kutafuta mbinu za kisasa za kukabiliana na kile wanachoona ni tatizo, serikali na makampuni ya simu wanatafuta kufanya teknolojia na matumizi yake kuwa butu. Huu ni mkasa.

Serikali inaziba mifereji ya taarifa za siri kuhusu utendaji wake. Hasa kuziba kasi ya kuenea kwa taarifa juu ya mambo inayofanya lakini hayakustahili kufanywa na waliopewa madaraka ya utawala.

Hapa serikali imeingilia uhuru wa mawasiliano wa mtu binafsi. Inakana maendeleo ya teknolojia. Inaziba upenyo wa kupitishia kilio na tetesi. Serikali inatenda uhalifu.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii iichapishwa katika gazeti la Tanzania daima Jumapili, toleo la 22 Julai 2009)

No comments

Powered by Blogger.