Header Ads

LightBlog

ASKOFU KAKOBE ATAMANI UDIKITETAKUZIMA MAWAZO KWAWEZA KULETA VURUGU;
KUKUBALI YATOKE KWAWEZA KUZIEPUSHA


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Askofu Zakaria Kakobe wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) ajiingize katika mjadala ambao hauwezi na hautaleta manufaa kwa kanisa wala waumini wake.

Mapema wiki iliyopita alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa Rais Jakaya Kikwete amezidi kwa upole kwa vile hajakemea kanisa Katoliki kwa kutoa “Waraka” wa elimu ya uraia kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kakobe alisema pia rais amekuwa mpole mno kwa kutokemea Shura ya Maimamu kwa kutoa “Muongozo” wa waislamu ambao maimamu wanasema unalenga kumwelimisha mwislamu juu ya nafasi yake katika siasa za nchi hii.

Askofu wa kanisa la FGBF anasema maandishi haya yanaweza kuleta utata mkubwa na hata mifarakano katika jamii. Alimpongeza Kingunge Ngombale-Mwiru, mbunge mteule wa rais, kwa kukemea Waraka na kufikia hatua ya kusema “wauondoe” na kwamba Ngombale-Mwiru “aliona mbali.”

Lakini ukali wa rais unahitajika kwa lipi hapa? Katoliki wanasihi wananchi kujadili aina ya viongozi wanaowahitaji na ndio hao wawapigie kura. Wametoa andishi la kusaidia kuendesha mijadala miongoni mwa waamini na jamii kwa jumla.

Shura ya Maimamu imetoa andishi la kukumbushia lawama zao kwa utawala; malalamiko kuhusu kubaguliwa; nafasi ya mwislamu katika siasa za awali katika kutafuta uhuru na kuhimiza waislamu kuwachagua waislamu au wale wanaoona wataendeleza maslahi yao.

Kwanza, tujadili ukali wa rais. Huyu ni mtawala mkuu wa nchi. Ametokana na mfumo wa utawala ambao analazimika kuulinda, kuutetea na kuuendeleza. Ni mfumo huo ambao unatoa viongozi wanaolalamikiwa kwa kutokuwa makini.

Rais awe na ukali upi zaidi; wa kiasi gani kuliko huu alionao sasa; anaoutumia na kuusimamia na unaosababisha kupatikana kwa viongozi wanaolalamikiwa?

Askofu Kakobe anasema Rais Kikwete anatembeza tabasamu tu. Lakini tabasamu la rais ni ishara ya utulivu wake moyoni; kwamba hana presha; kila kitu kinakwenda kama anavyotaka na kwa mujibu wa mfumo anaosimamia.

Laiti Kakombe angejua kuwa mfumo wa jana na leo, ambao rais anasimamia, ni wa kibaguzi; unanyima fursa ya kuwa kiongozi wa siasa mpaka uwe mwanachama wa chama cha siasa.

Ni mfumo katili unaokufungia katika “mahabusu” ya chama hichochicho kiasi kwamba ukihama unakuwa umejifukuza kazi uliyopewa na umma kwa njia ya sanduku la kura.

Vilevile ukiwa na maoni tofauti, hata yanayolenga kuimarisha chama chako, kama yanaelemea baadhi ya wazito ndani ya vikao vya juu vya chama hicho kilichoko ikulu, basi utakuwa unajipalia mkaa; tena wa moto. Utawindwa. Unaweza kuuawa kisiasa. Huo ndio mfumo ambao rais anasimamia huku akiwa anatabasamu.

Katika mfumo huu ndimo aliyeiba mabilioni ya shilingi anasamehewa kwa kurejesha kiasi, lakini aliyeiba chungwa anafungwa miaka mitatu. Ubaguzi mzito.

Ni humuhumu ambamo kuna makubwa ya kukamua utajiri wa taifa hili. Mikataba ya kinyonyaji; wizi wa waziwazi kabisa wa fedha za umma; uporaji raslimali hata wanyama, magogo na mchanga.

Yote haya, hata kama hayakuanzishwa na viongozi wa utawala wa sasa, yako chini ya utawala wa rais anayeambiwa na Kakobe kuwa anunie barua ya kanisa kwa waamini na malalamiko ya waslamu.

Pili, katika mfumo huu ndimo kuna waandishi wa Waraka na Muongozo. Machapisho haya yanaeleza ama jinsi ya kujikwamua kutoka katika mazingira tuliyomo kwa kuwa na viongozi wakweli na thabiti; au yanawasilisha maoni ya makundi na watu binafsi katika mustakabali wa siasa za nchi yao.

Sasa Kakobe anataka rais awe mkali katika kuzuia maoni ya makundi, asasi na taasisi za wananchi? Akifanya hivyo atajuaje maoni yao? Atajuaje kuwa anapingwa katika hatua hii au ile? Atajuaje malalamiko na lawama ambazo serikali yake inabebeshwa?

Askofu Kakobe atakuwa ameona kuwa baadhi ya madhehebu duniani yameingia katika mageuzi ya fikra. Yanakiri kuwa hayawezi kuhudumia “roho za waamini na na waumini bila kufikiria hali zao kidunia.”

Roho za wafuasi wa madhehebu hayo zinakaa katika makasha yaitwayo “miili.” Kama miili itakuwa imedhoofika kwa njaa, maradhi na ujinga, hata kile wanachohubiriwa ili kukidhi matakwa ya roho hakitaingia.

Kunahitajika maandalizi ya roho. Haya yanaanza kwa kutambua kuwa kuna mwili. Kwamba mtu yupo; tunamwona na anashikika; siyo wa kufikirika. Kwamba ana mahitaji ambayo sharti ayapate ili aweze kuwa na uwezo wa kupokea mahubiri.

Maandishi makuu kwamba binadamu haishi kwa mkate (chakula) peke yake yana makali ya pili; kwamba binadamu haishi kwa kuhubiriwa tu, bali kwa chakula pia na mahitaji mengine ya mwili.

Ukamilifu wa mwili unahitajika ili kupata ukamilifu wa roho. Mbingu siyo kwa watu masikini na hohehahe peke yao, bali hata matajiri kwa njia ya halali ambao wamepondeka mitima.

Hii ndiyo maana hata kama rais hataki Waraka au Muongozo, sharti ajitahidi kuvisoma, kupata maoni ya wengine, kuyachambua na hata kuyatumia kutekeleza yale ambayo maandishi yanasema hata kulalamikia.

Bali kuna tabia ya serikali kuhusudu ukimya wa watu, ujinga na umasikini wao. Hii ni mitaji mikubwa ya serikali nyingi duniani. Vilevile ni mitaji mikuu ya baadhi ya madhehebu ambayo yanataka “kupakia” wananchi mahubiri kama anayepakia gunia.

Wanaohubiriwa ni watu wenye akili timamu na wana uwezo wa kufikiri. Wakipata fursa ya kujadili na kufanya maamuzi, wanaitumia vilivyo kuliko kutaka rais awanunie, awazibe mdomo na hivyo kuziba akili zao ili wasifikiri. Hapa Kakobe amekwama.

Fikra za Kakobe zinafanana na za serikali ya Zanzibar ambayo juzi ilitangaza kupiga marufuku Waraka na Muongozo. Bali hii siyo mara ya kwanza kwa serikali ya Zanzibar kufanya viroja.

Kuna wakati ilizuia ufundishaji wa historia (na fasihi?) mashuleni kwa madai kuwa historia inaibua chuki na uhasama. Haya ni maamuzi ya woga, ya kidikiteta; yenye shababa ya kudhibiti akili za watu na utashi wao.

Mbona nchi hii inahitaji nyaraka nyingi tu zenye maoni mbalimbali, tena ya mirengo tofauti. Zinaweka wazi maoni ya waandishi na wananchi. Zinasaidia watawala kuona walikofika au walikoshindwa kufika.

Kuziba maoni ni kujifungia katika kiza cha ujinga na ubabe wa kidikiteta. Ni kuhalalisha juhudi za wananchi, kupitia asasi mbalimbali, kuandaa mikakati halali ya kuondoa watawala madarakani.

Hata katika ukimya wa uzao wa udikiteta, mawasiliano hupenya na mikakati huundwa. Kipi bora: Kupata maoni ya wananchi au kusubiri hasira zao zijae vifuani na utokee mlipuko?

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 6 Septemba 2009)

No comments

Powered by Blogger.