UDIKITEA MBAYA SASA WAJA
CCM na ukandamizaji wa fikra
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiwe nguzo ya nne ya dola. Nilitarajia kikae uwani, kijirembe kwa vipodozi na mavazi ya kila aina, kisubiri harusi, lakini kisikoromee nguzo yoyote ya dola.
Jijini Dodoma, kupitia kwa mjumbe wa NEC ambaye pia ni spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano, CCM ilitoa onyo kwa wawakilishi wa wananchi kwamba wamepanua mno midomo yao; wamekijeruhi chama na serikali; sasa wachunge sauti na kauli zao.
Wabunge wameambiwa, kupitia kwa Spika Samwel Sitta kuwa wasijadili masuala yahusuyo “ufisadi” ndani ya bunge bali ndani ya vikao vya chama, kikiwemo kikao cha wabunge wa CCM. Wameamriwa. Kutofanya hivyo ni “kukiumiza” chama na serikali na kuneemesha upinzani.
Amri hizo kutoka Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, hakika zinakwenda kinyume cha matarajio. Kinyume cha utaratibu. Kinyume cha mwenendo wa “klabu” za kisiasa. Kinyume cha Katiba.
Leo CCM inakaripia spika wa bunge; eti ametoa mwanya mkubwa kwa wabunge kuisakama serikali. Eti ameruhusu serikali idhalilishwe. Eti ameacha mwanya mkubwa unaotumiwa na baadhi ya wabunge kukaripia viongozi wa chama, serikali na hata viongozi wastaafu.
CCM inataka spika wa bunge awanyamazishe wabunge. Awakemee na kuwakoromea pindi wanapokuwa wakali kwa serikali. Kwani sasa inadaiwa wabunge “wamekuwa huru kupita kiasi” na kwamba wanastahili kudhibitiwa.
Hatua ya CCM inalenga kufanya bunge kuwa kamati ya chama. Inalenga kufanya spika kuwa mhamasishaji wa shughuli za chama na serikali ndani ya bunge. Inalenga kugeuza bunge – kutoka msimamizi na mshauri wa serikali – kuwa sekretarieti ya chama na serikali.
Hiyo ndiyo maana ya kukemea spika kwa madai kuwa “ameruhusu uhuru zaidi.” CCM inataka bunge lililopigwa pasi; lile la “Chama Kushika Hatamu” – magereza ya siasa yaliyoandaliwa na Pius Msekwa kutukuza mfumo wa chama kimoja. Watawala wanataka bunge liimbalo sifa na utukufu wa chama kimoja na kiongozi mmoja mwenye fikra ngumu na “zinazodumu.”
Kupitia kwa spika aliyenyamazishwa, wabunge wanyamaze. Kupitia kwa wabunge walionyamaza, wananchi nao “wafyate mkia.” Kuwepo na sauti moja, kauli moja – ile ya klabu moja siasa – CCM na serikali yake.
Hapa ndipo panakuza ukinzani. Wananchi hawakuchagua wabunge ili wabunge waitetee serikali. Mbona serikali ina watetezi wengi bungeni? Dhana ya uwakilishi ina maana ya jicho, sikio na mdomo wa nyongeza wa wananchi; vilivyopewa jukumu la kusimamia na kushauri serikali na kutetea maslahi yao.
Kwa chama na serikali kutafuta kunyamazisha wananchi kupitia vijembe, vitisho na tuhuma dhidi ya spika, ni kutaka kuwa na taifa la mazezeta; linalosikia bila kuelewa; lisilofikiri na lisiloongea kwa kuwa limekatwa ulimi; lisilotoa hata mgumio wala mguno kwa kuwa limetumbukizwa katika woga usiomithilika.
Kesho CCM yaweza kukemea Jaji Mkuu kwa madai kuwa hukumu zake zinakuwa kali kwa viongozi wa chama, serikali na viongozi wastaafu. Jaji mkuu aweza kusutwa kwa kutoa uhuru zaidi kwa mahakimu na majaji wenzake na kwamba uhuru huo “unadhoofisha serikali.”
Ikifikia hapo, siyo tu uhuru wa kufikiri utakuwa umeingiliwa sana na hata kunyongwa; uhuru wa watu wa kuishi utakuwa mashakani. Hii ndiyo hatari kubwa zaidi. Kwa chama kilichoko ikulu kutamani taifa lililokimya, ni sawa na kutamani kutawala miti, mawe na wanyamapori. Siyo watu.
Hoja kuu inayowagawa wabunge hivi sasa na ambayo CCM na serikali hawataki kusikia wabunge wakiijadili hadharani, ni juu ya “ufisadi.” Chama hiki na serikali yake vinataka hoja hii ijadiliwe kimyakimya kwenye vikao na siyo kweupe.
Hii ni hoja inayoeleweka kwa urahisi. Inayopenya katika vichwa vya wengi. Inayojadilika. Inayoweza kuhusishwa na maisha ya kila mmoja popote alipo. Inayofanya watu wafikiri, waulize maswali na watake majibu. Inahusu uhai wao – kufa au kupona.
Kwa upande wa watawala, hoja hii ni mbaya. Inaingiza watu wengi kwenye mjadala ambao serikali haiwezi kudhibiti. Ni mjadala huu mpana unaoweza kuathiri maamuzi ya wananchi wakati wa uchaguzi wa viongozi. Unaleta vidonda mwilini mwa serikali na CCM na unatonesha daima.
Mjadala huu ungehusu vyama vya upinzani, usingetafutiwa mbinu za kuuzima. Ungekuwa kipenzi cha watawala na ungekuzwa na kuenezwa nchini kote ili penye uoza paonekane. Yote yangefanywa “kwa jina la demokrasi na uhuru wa maoni.”
Bali mjadala unapolalia watawala, basi hakuna suala la demokrasi wala haki na uhuru wa maoni. Unakuwa mchungu. Unatishia walioko kileleni. Unatishia uhalali wa utawala wa serikali. Matokeo yake, serikali inatafuta kuuzima kwa njia yoyote ile.
Vitisho vilivyoelekezwa kwa spika vinakwenda mithili ya hadhithi ya Karumakenge – maji yanatishia kuzima moto; moto unatishia kuchoma fimbo; fimbo inatishia kupiga Karumakenge; na Karumakenga anakubali kwenda shule. Bali hii ni hadithi ya kimaendeleo na endelevu.
Sasa NEC ya CCM inatishia kufukuza Spika Sitta; Sitta atishie kuadhibu wabunge; wabunge watishie kugomea wananchi wanaowatuma; na wananchi wanyamaze – kama maiti. Kunahitajika ukimya ambamo kishindo cha mende kitasikika kama tsunami. Hii si hadithi; ni hali halisi inayopingana na maendeleo. Ni ujima mchafu.
Ukame wa fikra na mijadala ambao CCM inataka utawale bunge na jamii kwa ujumla, ni msiba mkubwa kwa taifa. Hii ni sababu ya kutosha kupinga kuendelea kuwepo utawala wa serikali ya CCM.
CCM, kama vilivyo vyama vingine, ni klabu ya kisiasa – moja ya asasi za kijamii za kuragbishia raia kushiriki katika siasa na utawala wa nchi zao. Kama klabu hii imeshindwa kutambua umuhimu wa uhuru na haki ya kuwa na maoni; na inatafuta njia za kuvihujumu; basi heri klabu ife kuliko uhuru wa watu na watu wenyewe.
0713 614872
ndimara@yahooo.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la Jumapili tarehe 23 Agosti 2009)
No comments
Post a Comment