KASHFA YA MEREMETA YAWEZA KUZAMISHA SERIKALI
MAWE YAKISEMA, SERIKALI ITAUMBUKA
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI waziri Jeremiah Sumari achokoze Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kutumwa au kwa sababu zake binafsi.
Majeshi ni mawe makubwa. Majabali. Miamba. Majeshi ni wagumba. Majeshi yakitaka kuzaa sharti yakubali kufa polepole; kwa maana kwamba atokee wa kuyapasua ili yatoke mengi kwenye mawe makubwa au miamba. Hapo hayabaki mojamoja na imara tena.
Na kawaida majeshi ya nchi hayachokozwi na mtu wa ndani wala wa nje. Wachokozi huchokoza nchi na watawala wa nchi zilizochokozwa huagiza majeshi yake kwenda mstari wa mbele na kukunja uchokozi kama jamvi la wageni.
Lakini uchokozi uliofanywa na waziri Sumari ni wa ndani na unaweza kufanya mawe makubwa, miamba kutamani kutoa sauti na kusema hayataki kupasuliwa; yaachwe kama yalivyo.
Akijibu swali la Dk. Willibrod Slaa juu ya ufisadi ndani ya mradi wa Meremeta, Sumari alitoa majibu ya vitisho. Alimwambia mwakilishi wa Karatu (CHADEMA) aachane na hoja ya ufisadi ndani ya Meremeta.
Kiasi kinachodaiwa kupitia Meremeta kwenda mifuko isiyojulikana si haba. Ni zaidi ya Sh. 155 bilioni. Waziri anamwambia mbunge aachane na hoja ya Meremeta kwa madai kuwa mradi huo ulikuwa wa jeshi; kwamba ni suala nyeti na labda ni kuingilia suala la usalama wa taifa.
Waziri anataka kulazimisha mawe kusema. Mawe yatabaki kimya juu ya ahadi zao; juu ya mipango yao na silaha zao; juu ya mikakati ya sasa na baadaye; juu ya mbinu mpya walizopata katika medani ya vita; juu ya wanachopanga kufanya hivi sasa.
Ukimya huu ni kama jua, mvua na upepo vipigapo kwenye mwamba na mwamba ukavumilia. Zaidi ya hapo, miamba husema. Miamba mingi imeota juu ya mizimu ya kale iongeayo wakati wa jua kali.
Inawezekana, siku moja unapita karibu na miamba hiyo, wakati wa jua kali, ukasikia mtu akikuita kwa sauti ya juu sana – mara mbili au mara tatu – na usimwone.
Wale dhaifu wa moyo huweza kuanguka chini na kuzimia; wengine humudu kukimbia hadi nyumbani kwao, wakitweta na kulowa jasho mwili mzima huku wakiishiwa na kauli. Mawe, majabali, miamba imeamua kusema!
Wakati huo hujawahi kuichokoza. Hujailalamikia wala kuituhumu. Hujaisingizia wala kuihusisha katika miradi bubu ya watawala. Inasema tu. Inabubujika. Sembuse utakapoihusisha na wizi, uporaji, ukwapuaji, au kwa ujumla – ufisadi!
Ikae kimya? Sitaki waziri Sumari achokoze miamba na yenyewe iseme kwamba haijui Meremeta ni nini na ya nani. Kwamba haijawahi kunufaika na kampuni hiyo. Kwamba mafao yaliyotokana na Meremeta hayafahamiki jeshini. Kwamba hayakuingia jeshini.
Sitaki waziri achokoze miamba ianze kukohoa na kunong’ona na hatimaye kulipuka. Miamba hii inajua kuwa fedha za kuendesha jeshi hutoka kwenye bajeti ya serikali inayosomwa na kupitishwa bungeni.
Miamba hii inaelewa vema kwamba wakati Meremeta wanaanzisha mradi walihamisha wananchi kutoka makazi yao. Walihamisha hata kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa na kutawanya askari katika vijiji kwa kutumia mikokoteni.
Si wananchi – raia, wala askari walionufaika na mafao ya Maremeta baada ya kuanza kuvuna kutokana na mgodi. Shule na zahanati vilivyong’olewa havijarudishwa. Bwawa kubwa la maji lililokuwa sehemu ya uhai wa watu na viumbe anuwai, halijarejeshewa hadhi yake.
Sitaki watawala jeshini wajitokeze na kuiumbua serikali juu ya matumizi haya. Sitaki wapatikane watumishi wa Wizara ya Ulinzi na kuthibitisha kuwa hawajawahi kupanga fedha za Meremeta au sehemu yake katika matumizi ya wizara.
Sitaki maofisa wa ngazi za kati jeshi waanze kufurukuta na kusema hawataki kusingiziwa katika suala la ukwapuaji na hivyo kujitokeza na ukweli utakaoangamniza hadhi ndogo ya watawala iliyosalia.
Sitaki askari wa vyeo vya chini ambao wanajua vema kilichokuwa kinaendelea waanze kujitokeza na kusema walichoona na nani hasa walikuwa wavunaji wakuu wa Meremeta na siyo jeshi.
Wala sitaki askari wakumbushe serikali kwamba Tume ya Jaji Bomani iliishasema kuwa Meremeta si mali ya serikali bali ni ya binafsi. Labda likisemwa na wao ndipo serikali itasikia na waziri Sumari ataelewa.
Nani anataka azibuliwe masikio kuliko alivyofanya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aliiambia Kamati ya Bunge kuwa Meremeta haimo katika orodha ya mashirika ya umma na kwamba ofisi yake haijawahi kuikagua.
Mei mwaka jana tulipeleka baruapepe kwa benki ya Nedcor Trade Services ya Afrika Kusini kuhusiana na suala hili. Hatukujibiwa. Tuliwaandikia Deutsche Bank AG ya Uingereza. Hawakujibu.
Lakini kwa kufuatilia kinachoendelea ni kwamba serikali haifanyi lolote. Imetafuta mahali pa kuegesha na kusahau hoja za wananchi wanaotaka kujua huyu Meremeta ni nani na fedha alizochota alizitumia wapi.
Matumizi ya visingizio vya jeshi, kama anavyosema Sumari, hayana uzito tena. Hayamtishi yeyote. Wananchi, wachunguzi na wengine wanaotafuta ukweli wangestuka na hata kuogopa kama wangekuwa wameingilia undani wa shughuli za jeshi.
Lakini hili la kikampuni cha Meremeta halimtishi mtu. Badala yake linaweza kuiweka serikali pabaya, kwani inaendelea kujichanganya; kuficha ukweli na hatimaye kusema uwongo.
Hatari kubwa inaweza kuzuka pale mawe, majabali na miamba itakaoamua kuvunja kimya; siyo lazima kwa mikutano ya hadhara bali kwa mn’ong’ono tu ambao hatimaye utavuma kama upepo wa kimbunga.
Na askari – hiyo miamba – ni watoto wa watu masikini na wao ni masikini pia. Hawana cha kupoteza kwa kusema ukweli wanaoujua. Hapo ndipo serikali itaumbuka zaidi.
Nani anaweza kuiondolea aibu serikali kwa kusema ukweli na kuijengea heshima na uhalali? Kama siyo mawaziri wake, nani hasa? Tusubiri majabali yaite wakati wa jua kali na kwa mzizimo wahusika wazimie?
Uwezekano wa aliyezimia kupitiliza hadi dunia nyingine ni mkubwa kuliko aliyesimama. Kwa nini serikali ijiingize kwenye majaribu tata? Ukimya unaidhalilisha serikali na kuiondolewa uhalali. Itoboe kilichomo ndani ya Meremeta.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili Juni 2009)
No comments
Post a Comment