Header Ads

LightBlog

WAFUGAJI 'WAKIRUDI KWAO' ITAKUWAJE?


Yatatokea maafa makubwa ya kuangamiza mali na maisha

Na Ndimara Tegambwage


SERIKALI haiwezi kukimbia wajibu wake wa kurejesha amani kwa jamii za wafugaji nchini, kusitisha uvamizi na uporaji ardhi yao ambao umewafanya wakose mahali pa kuishi na kulishia mifugo yao.

Kile ambacho serikali inatakiwa kufanya sasa, ni kupanga na kutangaza maeneo maalum ya makazi ya wafugaji na maeneo ya kufugia na kuchungia mifugo yao.

Kumbukumbu zinaonyesha uzoefu wa serikali kutangaza mbuga za wanyama; mbuga za kuwindia kwa kuua wanyama au kuwinda kwa kutumia kamera (kupiga picha). Ni nadra kusikia serikali ikipanga, kutenga na kutangaza maeneo ya wafugaji na mifugo yao.

Kwani kinachoendelea hivi sasa, katika mbuga za Loliondo, wilayani Ngorongoro, katika mkoa wa Arusha, ni mwendelezo wa ukatili usiomithilika unaoendeshwa kwa baraka na mipango ya serikali, kuwang’oa wafugaji kama magugu na kuwaacha juani wakauke.

Baada ya miaka mingi ya uporaji, uliopangwa, kutekelezwa na kuratibiwa na serikali – ya kikoloni na ile ya uhuru – au matendo ya watu binafsi ambayo hayakukemewa na mamlaka, watawala sasa wanageuza kibao na kusema wafugaji ni wavamizi. Wanasema warudi walikotoka.

Chukua mfano wa Kilimanjaro Magharibi (West Kilimanjaro). Wakazi wa maeneo haya, wengi wao wakiwa Wamasai, walifukuzwa katika maeneo ya Enduimet na kuswagwa hadi chini ya mlima Kilimanjaro.

Madai yalikuwa kwamba wafugaji wanaharibu mazingira kwa “kuchezea vyanzo vya mito ya asili.” Baada ya wafugaji kuondolewa, wakulima wa kizungu na baadhi ya Waafrika walivamia maeneo ya mlimani na kuharibu vyanzo vya maji ambavyo wafugaji walitunza kwa miaka nendarudi.

Leo hii, vyanzo vya maji vya Olmorog, Lelanwa, Kamwanga na Engare-Nairobi, vimepungukiwa maji na vingine kukauka kabisa.

Katika hali hii, nani ameharibu mazingira: Wafugaji walioyalinda miaka yote au wavamizi, wakiwemo wazungu wa Kiholanzi waliodai kuyalinda lakini wakayakausha kwa kilimo na ukosefu wa mipango endelevu?

Madai hayohayo yalitumiwa kufukuza wafugaji kutoka eneo lote la Monduli. Wananchi katika eneo lenye rutuba la Lorkisalie waliswagwa nje kwa madai kuwa wazungu wanataka kuanzisha kilimo cha mbegu za maharage.

Kilimo hakikudumu. Ardhi ikawa tayari imechafuliwa kwa wingi wa mbolea za kisasa na kupoteza uasili wake. Wafugaji wakawa wemeswagwa kama mifugo, kwenda “kokote kule” bila kutengewa sehemu maalum iliyopangwa na serikali kwa ajili ya kuishi na machungio.

Naberera katika Simanjiro, lilikuwa eneo zuri la wafugaji. Ardhi nzuri iliyokuwa ikinawirisha watu na mifugo yao ilinyakuliwa na wazungu na Waafrika, wakiwemo viongozi wa siasa na serikali. Wafugaji wakatupwa nje.

Twende Kiteto. Sehemu kubwa ya ardhi iliyokuwa makazi ya wafugaji na malisho ya mifugo, ilivamiwa na baadhi ya viongozi wa siasa, serikali na matajiri wengine. Wafugaji wengi wakaswagwa nje na wakuja wakaanzisha kilimo cha mahindi.

Katika eneo hili, wakulima wamefanya kufuru. Wameparamia hata vilima vya kijani vilivyotunzwa na wafugaji. Wameingilia vyanzo vya maji vilivyoneemesha mifugo. Sikiliza sauti ya mfugaji:

“Sisi wachache tuliokuwa timesalia, tukawa kama ulimi katikati ya meno,” anaeleza mmoja wa wafugaji wa Kiteto. Wafungwa. Huu ukawa mwanzo wa mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hili.

Uporaji ardhi ya wafugaji ulienea na bado unaendelea katika maeneo mbalimbali. Angalia Serengeti ambako wafugaji wengi waliswagwa kama mifugo yao, nje ya makazi yao na malisho ya mifugo, kwa madai ya kuhifadhi wanyamapori.

Serengeti ambayo imekuwa makazi ya wanyamapori ainaaina; kutambuliwa na kutangazwa dunia nzima kuwa kivutio cha aina ya pekee kwa watalii na labda “boma” la mwisho la viumbe wa porini, imelindwa na kuhifadhiwa na wafugaji ambao mifugo yao ilifanya urafiki na wanyamapori.

Njama za kutawanya, kutelekeza na labda hata kuteketeza wafugaji katika Serengeti ni njama za ngazi ya kimataifa. Vimeandikwa vitabu vingi juu ya maajabu ya Serengeti lakini nafasi ya mfugaji kama mhifadhi wa wanyama hao haijazingatiwa. Itaonekana picha ya mfugaji kwenye jalada tu.

Leo hii, ndani ya mbuga za Serengeti, ambamo wafugaji waliishi, kufugia ng’ombe, mbuzi na kondoo na kuchunga mbuga na wanyamapori, ndimo kumejaa wanaoitwa wawekezaji.

Wawekezaji hawa hawataki hata kuona mtoto wa mfugaji akikatiza, wala ng’ombe akinusa maji ya mto ambao wafugaji wametunza kwa maisha yao yote. Kutoka ng’ambo moja ya mto hadi nyingine limekuwa kosa kubwa la kusababisha vifungo kwa walinzi wa Serengeti na watoto wao.

Mwekezaji ndani ya Serengeti hataki kuona mwananchi; anataka kuona watalii kutoka nje. Anataka kuona shilingi tu itokanayo na wanyamapori ambao wananchi wametunza na kuhifadhi kwa kipindi chote cha maisha yao.

Hapa pia wafugaji waliswagwa nje ya maeneo yao walikoishi, kufuga na kulinda wanyamapori. Wafugaji walilinda wanyamapori kwa kuwa hawawali; wao hula mifugo yao tu.

Hivi sasa wafugaji waliobaki Serengeti wanaishi kwa mfano uleule wa “ulimi katikati ya meno.” Wamefungwa. Wamebanwa mithili ya watumwa; katika nchi yao iliyopata uhuru wa kisiasa yapata miaka 50 iliyopita.

Yaliyotokea West Kilimanjaro, Monduli, Simanjiro, Kiteto na Serengeti, ndiyo hayohayo yaliyotokea Ngorongoro: Kuvamiwa kwa ardhi na kufukuzwa kwa wakazi wa miaka yote ili kuanzisha “Jamuhuri za Wanyamapori.”

Maeneo yote tuliyojadili yamekuwa yakiitwa Masailand – kuanzia Kilimanjaro Magharibi hadi Lobo – kwenye mpaka wa Kenya. Haya ndiyo yalikuwa makazi ya Wamasai.

Historia inasema Wamasai ni taifa linalotembea. Linalohamahama. Lina mifugo na linafuata maji na malisho. Lakini ukweli ni kwamba taifa hili lilikuwa limetua na kuridhika katika maeneo yaliyojadiliwa.

Kama ambavyo hakuna mwenye asili ya mahali alipo, kwamba vizazi vilivyotangulia viliumbiwa hapo (imani) au viligeukia hapo kutoka nyani wangurumao (sayansi), Wanilotiki kutoka milima ya Golani sasa walikuwa wametua na “ardhi” yao kupewa jina na wakoloni kuwa Masailand.

Jirani na Wamasai walikuwa Wabarbaig ambao pia katika miaka ya hivi karibuni walitendewa unyama huohuo wa kuporwa ardhi na kufukuzwa kwenye makazi yao na kuanza kutangantanga.

Mradi wa Basotu, Arusha wa kilimo kikubwa kilichoitwa “mashamba ya ngano ya Basotu” yaliyoendeshwa na Wakanada, uliwaacha Wabarbaig bila makazi.

Leo hii hakuna mashamba. Kilimo kimeshindikana. Yalikuwa mazingaombwe. Ardhi imechoka. Limebaki vumbi tupu. Wabarbaig waliishatupwa nje; wanatangatanga na mifugo yao.

Kwa mtindo huu, jamii za wafugaji zimefanywa za wakimbizi wasiotakiwa popote pale ndani ya nchi yao.

Soma majina haya: Lomnyak Siololo, Kayiok Leitura, Ngiliyayi Ndoinyo, Ngirimba Ndoinyo, Sepekita Kaura na Tokore Siololo. Hawa ni miongoni mwa waathirika wakuu wa mipango ya serikali iliyofukarisha wananchi na kuneemesha watu kutoka nje ya nchi.

Wananchi hawa, kutoka kijiji cha Ololosokwan, wamechomewa nyumba, mazizi ya ng’ombe na wanaswagwa, wao na ng’ombe wao, kutoka walikoishi kwenda kusikojulikana.

Ni kutokana na mfumo huu wa uvamizi na uporaji makazi, wafugaji wametafuta makazi na malisho katika maeneo mengine ya nchi hii. Ni nchi yao. Ni kwao kama kulivyo kwa wengine.

Tatizo hapa ni kwamba serikali, iliyoshiriki kuwafanya wafugaji kuwa watu wa kutangatanga kuliko asili yao, ndiyo inatangaza kuwa wafugaji “warudi kwao.”

Sasa wafugaji wanauliza” “Kwetu ni wapi?” Swali kubwa hapa ni hili: Wafugaji wakirudi kwao, itakuwaje?

Jibu: Vitatokea vita vikubwa vya kuangamiza watu na mali zao; kile kilichoimbwa kwa miaka mingi kuwa ni amani na utulivu wa nchi, kitatoweka kama ukungu wa asubuhi.

Kutatokea vita kwa kuwa maeneo walikofukuzwa wafugaji sasa ni mbuga za wanyama zilizomo mikononi mwa waporaji wakubwa wa maliasili wanaopewa upendeleo kwa kuitwa “wawekezaji.”

Unawekeza nini katika mbuga yenye wanyama waliolindwa na kuhifadhiwa na wafugaji kwa karne na karne? Hapana. Hapa unachuma usipopanda. Vita vya wafugaji kujaribu kurudi walikotoka vitakuwa vikubwa na huenda endelevu na kwa gharama kubwa ya maisha.

Wafugaji wakirudi walikotoka – Kilimanjaro Mashariki, Lorkisalie, Simanjiro, Kiteto na Basotu (Barbaig), kutakuwa na vita ambavyo vitaharibu mashamba ya “wakubwa,” majumba ya kifahari, mifumo ya maisha ambayo tayari imejengwa na kuangamiza uhai wa watu na viumbe vingine.

Bali amani pia haiwezi kuwepo kwa kuendelea kuwa na watu wanaofukuzwa kila waendapo kwa kuambiwa “rudi kwenu.”

Wakati umefika kwa serikali kufanya mambo yafuatayo, yakiwa hatua za haraka na za mwanzo ili kusitisha uonevu na udhalilishaji wa wafugaji na kuepusha migongano na hata vita:

Kwanza, kusimamisha na kuacha kabisa mipango ya kufukuza wafugaji kutoka makazi yao ya sasa. Hili litahusisha kuacha kuchoma moto makazi yao. Nchi hii ni yao.

Pili, kurejesha wafugaji mahali pao katika sehemu ambako walifukuzwa hivi karibuni na kupanga, kuunda na kutangaza makazi ya wafugaji na malisho ya mifugo yao.

Tatu, serikali isitishe na izuie uchochezi wa wanasiasa na baadhi ya watendaji wake kwa wafugaji waliohamishwa zamani, kwa kuwaambia kurejea walikotoka, kwani hilo litazua vita ya maangamizi makubwa.

Nne, wafugaji wakaribishwe pale walipo; waelezwe kuwa safari yao imefika mwisho; watengewe ardhi kwa makazi na malisho bila kujali walikotoka.

Tano, maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya ufugaji yatengwe rasmi kwa alama zinazoonekana. Wafugaji wenye mifungo mingi, washirikishwe katika kugharimia miundombinu muwafaka katika mpangilio mpya.

Sita, serikali ijenge mahusiano mapya kati yake na wakulima badala ya kuwakemea na kuwalaani kwa madai dhaifu kuwa mifugo mingi “inaharibu mazingira.”

Saba, serikali iondokane na dharau na kutojali; badala yake itambue kuwa mifugo – mamilioni ya ng’ombe, mbuzi na kondoo wa wafugaji wanaotangatanga katika nchi yao – ni mali na kwamba kwa kuweka mazingira bora, itakuwa ya manufaa zaidi kwa wafugaji na taifa kwa jumla.

Nane, wafugaji washawishiwe na asasi za kijamii na serikali, “kusimama” na kubaki walipo sasa na kufanya makazi hayo kuwa ya kudumu.

Tisa, wafugaji washirikishwe katika kuandaa makazi, malisho na miundombinu. Kwa mfano, malisho yawe ya maeneo makubwa ambamo mifugo itahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ndani ya eneo husika, ili kuruhusu upatikanaji wa chakula katika maeneo walikochungiwa kwanza.

Umuhimu wa kushirikisha wafugaji katika kuandaa miundombinu unatokana na kuwepo kwa baadhi yao wenye uwezo kifedha kutokana na kuwa na mifugo mingi.

Ni hao ambao wana uwezo wa kuchangia ujenzi wa mipaka ya kutenganisha makazi na malisho, kujenga mabwawa wakati serikali inasaidia katika ujenzi wa miundombinu mingine kama ile ya maji, elimu, barabara na afya.

Kumi, ndani ya mipaka ya maeneo ya malisho, na wafugaji wakiwa sehemu ya jamii ya wakulima katika maeneo husika, ndimo inaweza kuendeshwa elimu juu ya upunguzaji wa mifugo kwa ufugaji wa kisasa.

Hatua hii itakayoendana na wafugaji kukataa kuendelea kusukumwa nje ya mahali walipo, itajenga mshikamano mkubwa kati ya wakulima na wafugaji na kufanya uhasama kuwa historia.

Nilipata fursa ya kuongea na Luteni mstaafu Lepilall ole Molloimet (60) kuhusu suala hili. Aliwahi kuwa mbunge kwa miaka tisa, mkuu wa wilaya kwa miaka 12 katika wilaya za Kiteto, Babati, Korogwe, Musona na Rombo.

Molloimet ambaye sasa ni mfanyabiashara, anasema wakati umefika kwa Wamasai na wafugaji wengine kukataa kuhama kutoka walipo sasa.

Anasema, “Wamasai wabaki pale walipo. Wakatae kuondoka. Washiriki elimu lakini wabaki na mila na desturi zao nzuri; wachague viongozi wao wazuri, wajiamini, wawe jasiri na wakatae kuonewa; wawe tayari kukosoa na kukosolewa.”

Molloimet anasema anawashangaa wabunge katika maeneo ambako wananchi wanaswagwa kama mifugo kutoka kwenye makazi yao ya miaka mingi. Anasema wabunge hao, kwa kukaa kimya, ina maana wanaunga mkono unyama ambao wananchi wanatendewa.

“Kwa ufupi, wabunge hawa wanastahili kujiuzulu maana wameshindwa kazi ya kuwakilisha na kutetea waliowachagua,” anasema Molloimet.

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Molloimet anaungana na baadhi ya wananchi wa Olorien, Soitsambu na Magaiduru-Lorien huko Ngorongoro.

Amasema, “Dunia haituelewi. Tunafukuza Wamasai katika maeneo yao; lakini tunakaribisha Wazungu na Waarabu! Nani atatuelewa. Mimi nasema tu kwamba wafugaji wanataka amani.”

Taarifa zinasema juzi Jumatatu, ulifanyika mkutano juu ya hali ya wafugaji na hifadhi ya Loliondo. Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo katika kijiji cha Ololosokwan ni wawakilishi wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT).

Wengine ni asasi ya kimataifa ya utetezi wa wafugaji tawi la Tanzania (PINGOs), maofisa wa Idara ya Wanyamapori, Ortelo Business Corporation Limited ya Nchi za Falme za Kiarabu (OBC) walioshikilia eneo kubwa ya mbuga ya Loliondo na wajumbe wa kijiji cha Ololosokwan.

Haijafahamika waliongelea nini. Lakini taarifa zinasema watakuwa walijadili hatua ya serikali ya kuchoma makazi na maboma ya mifugo wakilazimisha wananchi kutoka kwenye makazi yao na katika vijiji vilivyoandikishwa kisheria.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 12 Agosti 2009)

1 comment

Foundation said...

Na Jana Mwakilishi wa Rais Mkuu wa Wilaya ya Tarime Frank Uhahula kawambia wananchi kuwa WAO NI serikali na wana uwezo wa kupiga marufuku ufugaji kama wizi wa mifugo utaendelea!!!

Ndio hulka ya 'viongozi' wetu tulio nao hapa Tz.

Powered by Blogger.