Header Ads

LightBlog

WOGA WA SERIKALI SASA WAPINDUKIA



Serikali inapotishia uhuru wa mijadala



Na Ndimara Tegambwage

SITAKI watawala wakatae Waraka wa Kanisa Katoliki ambao hasa ni elimu ya uraia ambayo ni mhimu kwa maisha ya kiroho, kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa wananchi na taifa lao.

Kwa upande wa watawala, kukataa elimu kunaweza kuonekana kuwa jambo la kawaida; kwani kwao, elimu ambayo haikutolewa na watawala, siku zote huonekana ama yenye kasoro au isiyofaa kabisa.

Kitu kibaya zaidi ni kwa watawala kutaka kuzuia raia kusambaza elimu ya uraia kwa jamii kupitia asasi zao. Ni kama inavyodhihirika sasa kwa baadhi ya walioko kwenye utawala kupinga Waraka wa madhehebu ya Katoliki unaochokoza mawazo tu juu ya kupata viongozi bora nchini.

Nimesoma waraka husika. Maudhui ni yaleyale ambayo tumezoea kuyasikia kanisani, misikitini na katika maoni ya watu wanaojali maslahi ya taifa. Lakini mara hii yameandikwa. Yamewekwa kwenye hali ya kudumu kwa muda mrefu na yataweza kufanyiwa rejea.

Kwa ufupi waraka ni wito kwa wananchi kukaa chini, kujadili na kuamua nani wanastahili kuchaguliwa kuwaongoza; wawe watu wa mwenendo na tabia gani. Sikuona zaidi.

Waraka unafanya jambo moja kubwa ambalo watawala hawataki kusikia. Unawapa wananchi fursa, uwezo na ujasiri wa kujadili na kuamua nani wawachague kuwa viongozi wao. Basi.

Waraka unahimiza utekelezaji wa haki ya kila raia katika kupata uongozi; unahimiza wajibu wa kushiriki katika kuchagua viongozi na uongozi, kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ya taifa.

Ni waraka huu unaohimiza njia ya kukaa pamoja, kufanya uchambuzi na ikiwezekana kukubaliana juu ya vigezo vya kijamii mahali husika katika kupata viongozi.

Lakini hata baada ya majadiliano ya pamoja, bado kila raia ana uwezo na haki ya kupima nani, kati ya wagombea, anazidi wengine na anaweza kuwa kiongozi bora.

Waraka unasaidia kuchokoza mbongo za washiriki katika mjadala kwa kueleza kiongozi bora ni nani. Huu ni uchokozi tu. Katika mjadala, wahusika waweza kutanua wigo wa waraka na kugusa hata hoja ambazo hazijafukuliwa na kuweka vigezo vyao. Hawafungwi.

Kupatikana kwa mwafaka wa vikundi, makundi au jumuia pana juu ya nani wanafaa kuongoza, kunawatwisha wapigakura wajibu wa kipekee wa kufuatilia viongozi na utendaji wao.

Labda ni hapa ambapo watawala wanapata shida kuelewa au wanaelewa lakini wanaogopa. Wanafikiri kuwa zinaweza kupatikana kura za makundi na wao kuenguliwa kwa njia ya sanduku la kura.

Bali ni ukweli usiopingika kuwa ujinga na umasikini ni mitaji mikubwa ya watawala. Kadri raia wengi wanavyobaki katika ujinga ndindindi, ndivyo watawala wanavyozidi kujichimbia ikulu mwaka baada ya mwaka.

Kama kuna kitu kinaitwa elimu ya uraia ambayo hutolewa na watawala, basi ni ile ya kueleza uwezo wa serikali, majukumu yake, mafanikio yake, utii na heshima ya raia kwa mamlaka. Ni vitisho vitupu vinavyopora ujasiri wa wananchi na kuzidisha upofu na ujinga.

Woga mkubwa wa serikali ni kwamba wananchi wakijua kinachoendelea ndani ya utawala, wataasi kimyakimya au watalipuka na kudai mabadiliko.

Katika hali hii, ikipatikana elimu ya kufanya watu wafikiri, wajadili kwa pamoja hoja kuu zinazowahusu; zinazohusu uhusiano wao na watawala na jinsi ya kufanya maamuzi; basi serikali hujawa na woga.

Ujasiri uliolengwa kupatikana kwa njia ya waraka wa kanisa unatishia “elimu” ya watawala; unabomoa kuta za siri, unaandaa jamii kuachana na ujinga na kuasisi mabadiliko ya fikra, bila kujali rangi, mahali mtu alipozaliwa wala imani.

Kanisa lisipofanya haya, na hasa leo, litabaki asasi kama asasi nyingine zisizo na uhai. Asasi zote, yakiwemo madhehebu, hazina budi kutambua kuwa haziwezi kuhudumia kiroho wale ambao ni dhaifu kimwili. Sharti zisimame nao na kuwapa ujasiri wa kufikiri na kutenda.

Mahali pengine, kuhubiri dini kwa watu masikini kumeongeza ukandamizaji. Wakati watawala wameishi katika uhondo, wametumia ghiliba ya kisiasa na mahubiri ya dini kufanya raia wawe butu zaidi na kulazimishwa kukiri kuwa hali waliyomo ndio matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Hatua ya baadhi ya madhehebu kufundisha umuhimu wa kuwa na jamii inayofikiri, inayoelewa kinachotendwa na watawala, inayodai haki na inayojadili jinsi ya kuwa na viongozi na uongozi bora, ni ya kukaribisha na siyo kusuta.

Walioingia katika uongozi kwa njia ya wizi, ghiliba, upendeleo na hujuma kwa wengine, ndio wanaweza kutilia mashaka fursa mwanana ya wapigakura kukaa pamoja na kujadili jinsi ya kupata viongozi bora.

Kuna swali: Kila madhehebu yakitoa waraka wa uchaguzi itakuwaje? Jibu: Kwa kuzingatia maudhui ya waraka wa kanisa Katoliki, madhehebu mengine yatasema mambo hayohayo lakini kwa maneno tofauti.

Hoja ya kuwa na kiongozi bora haina sura ya madhehebu. Hoja ya kukaa chini na kujadili nani katika jamii yenu anaweza kuwa kiongozi, haina hata harufu ya madhehebu.

Hoja ya uongozi bora ina misingi katika utu wa mtu na haki ya kila raia bila kulalia imani za dini – za asili na za kuja – isipokuwa pale imani hizo zinapokuwa zinakiri kwelikweli kile tunachotaka: Haki.

Kwa hiyo, katika mazingira ya uhuru wa maoni, siyo madhehebu tu yenye haki ya kutoa elimu ya uraia kwa kutumia waraka; bali mashirika na asasi zote za kiraia na watu binafsi.

Kinachohitajika siyo madhehebu au imani ya mtu au asasi, bali hoja ya kiongozi bora kutoka katika jamii na bila kujali ni wa madhehebu yapi.

Elimu ya uraia inayopendekezwa na waraka wa sasa, haifuti wala kudhoofisha sifa za mgombea uongozi au mpiga kura ambazo zinatajwa na Katiba ya nchi.

Hivyo ndivyo zinaweza kuwa nyaraka nyingine za madhehebu mengine, asasi nyingine, mashirika mengine na watu binafsi. Zitakuwa zinaimarisha sifa na misingi ya Katiba kwa kuwezesha raia kushiriki vya kutosha na kutumia utashi wao kupata viongozi bora.

Waraka uwe mwanzo tu. Tunatamani pamoja na viongozi wa dini kuombea amani na utulivu, waanze kufikiria kuacha kuombea watawala na kuwafanya sehemu ya utukufu wa Mungu.

Ni maombi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ambayo yamesimika madikiteta; kuwadumisha kwenye tawala na kuwaaminisha wananchi kuwa mamlaka waliyonayo (madikiteta) inatoka kwa Mungu.

Sharti wanaoogopa waraka wa kanisa Katoliki waanze kuogopa kutoombewa na kubarikiwa. Labda huu ndio utakuwa mwisho wa mwanzo wa kutenda mema.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 2 Julai 2009)

No comments

Powered by Blogger.