POLISI WAUA MWANDISHI WA HABARI
Mwandishi wa habari wa
Channel Ten TV aliyeuawa mikononi mwa polisi
Jumapili, 2 Septemba 2012. Aliwahi kuandikia
gazeti la michezo la MSETO, mdogo wake
MwanaHALISI lililofungiwa na serikali kwa muda
usiojulikana kuanzia 30 Julai 2012.
1.
2.
David Mwangosi
3.
Katikati ya watesi wake. Kamera hiyoooo, juu inachukuliwa. Bomba kubwa la bunduki yenye mdomo mpana likielekezwa kwenye tumbo lake.
4.
Masalia ya Daudi Mwangosi
5.
Masalia ya Mwangosi.
Askari aliyekuwa karibu
naye alikumbwa na moto wa bomu.
Amejinyosha pembeni mwa masalia
yaMwangosi: Atakuwa ana mengiya
kusimulia; huenda pamoja
na kueleza kuwa alijitahidi kusihi wenzake kuwa
"...huyo ni mwandishi wa habari ninamfahamu..."
Nani atamhoji? Waandishi? Serikali? Lini?
Nani anaweza kumtambua Mwangosi hapo juu baada ya kulipuliwa kwa bomu tena mikononi mwa polisi, kijijini Nyololo, Mufindi mkoani Iringa, Jumapili tarehe 2 Septemba 2012?
Waandishi wa habari na wapigapicha waliochukua picha hizi na kuzisambaza, hakika wanastahili heshima inayolingana na kazi waliyofanya.
Kutoa picha hizi hadharani siyo kuvunja maadili. Hapana! Kutumia neno "maadili" katika hili ni kuotesha kichaka au kujenga andaki ambamo wahusika wanataka kuficha ukatili, unyama na kila uchafu ili wananchi na dunia nzima wasiweze kujua na kuchukua hatua.
Naomba vyombo vya habari - hasa magazeti na televisheni - vitoe picha hizi ambazo haziumizi hata wazazi wa Daudi au mke wake na watoto; bali zinaonyesha unyama usiomithilika uliotendwa na wanaodaiwa kuwa "walinzi wa raia na mali zao."
Lengo la kuua kwa njia hii ni:
1. Kupandikiza woga miongoni
mwa waandishi wa habari.
2. Kutumia woga huo kugawa waandishi
- huku wakikaa wanaodai wanataka
"amani" na kule wakikaa wanaosema
"tutaendelea kurekodi matukio kwa
usahihi" na kuyapa tafsiri mwafaka.
3. Kupanda mbegu ya woga miongoni
mwa umma kwamba vita vyaja na hivyo
wakae kama kuku wa "kisasa" - mabroila -
wachinjwao bila kutoa purukushani
wala mlio wa kujipigania.
Leo, gazeti la TanzaniaDaima lilichapisha makala yangu iliyokuwa itoke jana, Jumapili katika safu ya SITAKI hata kabla ya kujua kuwa Daudi Mwangosi angeuawa. Mhariri anasema hawakuipata mapema na ndiyo maana ameamua kuitoa leo. Isome:
Polisi,
ukombozi na ‘bahati mbaya’
Na
Ndimara Tegambwage
SITAKI polisi wazuie maandamano na mikutano ya
vyama vya upinzani. Sitaki wazuie maandamano ya vyama. Sitaki wapige na
kujeruhi waandamanaji. Sitaki waue wanaoandamana.
Jirani yangu hapa ananiambia, “…wanaua kwa
bahati mbaya. Siyo kwa kukusudia.” Nakataa. Polisi wenyewe wanakataa.
Huwezi kuzuia maandamano kwa bahati mbaya.
Huwezi kuswaga wananchi kwa kiboko kwa bahati mbaya. Hapana! Huwezi kupiga
wananchi mabomu ya machozi kwa bahati mbaya.
Huwezi kufyatua risasi ya plastiki katikati ya
wananchi waandamanaji wasio na silaha kwa bahati mbaya. Nasema huwezi! Huwezi
kutwanga risasi ya moto katikati ya umati kwa bahati mbaya.
Huwezi kuendeleza vitisho kwa wananchi,
viongozi wao na vyama vyao kwa bahati mbaya. Huwezi kujiapiza, kwa bahati
mbaya, kuvuruga mikutano ya vyama vya siasa.
Huwezi kufinyanga na kuvaa sura ya ukatili
wakati wa kubugudhi wananchi halafu ukasema ni bahati mbaya. Hapana.
Huwezi kutumwa, ukatii, ukafinyanga na kuvaa
sura ya ukatili; ukashika silaha, ukafyatua risasi katikati ya waandamaji – iwe
ya plastiki au ya moto – halafu ukasema ni bahati mbaya.
Nasema yote haya kwa kuwa polisi ni chombo cha
serikali. Katika demokrasi, serikali huja na kuondoka. Leo kuna serikali hii.
Kesho kuna serikali ile. Keshokutwa kuna serikali nyingine.
Hata katika udikiteta, serikali huja na
kuondoka. Ama lidikiteta kuu litapinduliwa kwa mabavu kama
linavyotawala, litazeeka, litalewa na kusambaratika akili na wenzake watachukua
au litakufa.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, jeshi la polisi
linabaki la serikali iliyoko madarakani. Hii ndiyo maana askari polisi hupaswa
kuwa; na hasa kubaki waandilifu.
Hii ndiyo maana polisi wakaitwa walinzi wa
raia na mali
zao. Hii ndiyo sababu baadhi ya wananchi hujitolea kufanya kazi ya polisi –
ulizi – wakati baadhi ya polisi wamelala na kukoroma.
Mlinzi wa raia hafanyi mambo kwa bahati mbaya.
Mlinzi wa mali
za raia haongozwi na bahati mbaya. Kukubali upolisi ni kukubali bahati nzuri ya
kulinda raia na mali
zao. Bahati mbaya inatoka wapi?
Upolisi unaingiliwa na wanaotaka kulindwa
kuliko wengine. Wanaotaka kuiba haki za wengine. Wanaotaka kupora mali
za wengine. Wanaotaka kuneemeka zaidi kuliko wengine.
Hapa ndipo upolisi unapochafuliwa. Ni hapa
panapozaliwa kinachoitwa bahati mbaya. Sasa tukubali kwamba “bahati mbaya” ni
moja ya kazi ya polisi.
Tunajadili haya kwa kuwa Tanzania imo katika hatua muhimu ya
mabadiliko. Kuna vyama vya siasa vinapambana kuhakikisha utawala uliodumu kwa
miaka 50 unapisha akili mpya na mipango mipya.
Akili iliyogota haikukwamisha elimu peke yake;
biashara peke yake; usafiri peke yake, tiba peke yake; ilikwamisha pia mafao
kwa wananchi wakiwamo polisi.
Mafao ya jamii ni mengi – siyo mishahara peke
yake. Ukosefu wa mipango inayohakikisha kwamba mtumishi wa kima cha chini
anastahili kuishi hata baada ya kustaafu, ni mipango ya kwenda kuzimu.
Ukosefu wa mipango na taratibu za kukuza
kilimo cha mkulima mdogo – kwa ushindani tu wa kununua mazao yake ili achocheke
kuongeza eneo, kutumia mbegu bora, mbolea na mbinu za kisasa ili aweze kupata
zaidi na kuuza zaidi – ni kuita kifo kije haraka.
Mipango ya kufuga wananchi kama
kuku wapumbavu aina ya broila; kwa kuwazuia kusema au kuzima nyenzo zao za
mawasiliano na hivyo kunyamazisha umma na kuziba mifereji yake ya fikra, ni
kuandaa jahanamu kwa waliohai.
Kushiriki, kuruhusu au kufumbia macho wizi,
uporaji, ufisidi fedha na raslimali za umma na halafu kukaa kimya na kupakatana
na wezi na mafisadi, huku ukijiita mtawala; siyo tu kudharau akili ya umma
uliohai, bali pia ni kuangamiza umma huo.
Wanapotokea wenye hoja mpya, sera mpya, muono
mpya – wakitafuta mabadiliko katika utawala wa siasa, uchumi na utamaduni wa
wengi waliopoteza matumaini zamani – inatoka wapi “bahati mbaya” ya polisi
kuwapiga?
Au ni bahati mbaya kwamba polisi wametumwa au
wameamrishwa na wakubwa zao, kwenda kuzima nyota iliyoanza kutoa nuru kwa jamii
iliyoishi gizani kwa miaka nendarudi?
Iko wapi bahati mbaya isoyoona umuhimu wa
mabadiliko, tena kwa njia bora ya majadiliano na umma?
Nani asiyeona umuhimu wa wananchi kufikia
hatua wakasema, tena katika mazingira ya amani: nataka huyu aniongoze na sitaki
yule anitawale?
Inatoka wapi bahati mbaya ya kuzima matumaini
ya umma? Polisi, acheni wananchi watafute ukombozi wao na wenu pia.
0713 614872
No comments
Post a Comment