Header Ads

LightBlog

MJADALA WA UFISADI WAENDELEA

Ombaomba waliomkwaza Mkapa

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI viongozi na wananchi ombaomba ambao wanaweza kumkwaza rais na kumfanya achukue maamuzi yanayokinzana na maadili ya kazi yake au maslahi ya taifa.

Kwani kuna madai kuwa kila wanapomkera kwa kuomba kazi, vyeo, fadhila au chochote kile, ‘wanamkosesha muda wa kufikiri; wanaziba mtiririko wa fikra mwanana’ na kusababisha akiuke maadili ya ofisi yake.

Na hilo ndilo linadaiwa kumpata rais mstaafu Benjamin W. Mkapa; kwamba wanaosema kuwa alikiuka maadili alipokuwa ikulu ni wale waliomwomba vyeo na fadhila lakini hakuwapa. Sasa wanalalama.

Mkapa alinukuliwa akisema kijijini kwao katika wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba wanaosema alikiuka maadili akiwa ikulu ni waongo; na kwamba ni wale waliomwomba vyeo lakini hakuwatekelezea maombi yao.

Haya ni madai makubwa sana. Yanahusisha kila mmoja anayejenga mashaka juu ya mwenendo wa rais akiwa ikulu; awe aliomba au hakuomba kazi, uongozi au fadhila kutoka kwa Mkapa.

Sasa twende hatua kwa hatua kwa kuangalia mifano michache. Kwamba uamuzi wa rais na timu yake wa kununua ndege ya kifahari, kwa Sh. 40 bilioni, ulitokana na watu kumzonga kwa maombi ya kazi, vyeo na fadhila?

Na ndege yenyewe anasa tupu. Haitui kiwanja chenye vumbi; itaugua mafua na kufa. Haitui Zanzibar kabla ya kunusa anga za Madagascar; kwani kabla ya kukaa sawa angani inakuwa tayari imepita Zanzibar.

Kwamba wanaosema uamuzi wa rais na timu yake, kununua rada ya kijeshi kwa Sh. 70 bilioni, tena kwa milungula inayoanza kuwatokea puani baadhi ya wahusika, ni wale ambao rais hakutimiza maombi yao?

Katika hali hii, wale wanaosema serikali ya Mkapa, hapa na pale haikuwa na vipaumbele vinavyolenga kuborehsa maisha ya wananchi bali ufahari, wanaweza kusemwaje kuwa ni walalamikaji kwa kuwa maombi yao hayakutekelezwa?

Hivi inawezekana wanaosema kampuni ya Meremeta ilianzishwa na kunawiri na kuiba mabilioni ya shilingi ikidai kuwa ni kampuni ya serikali chini ya utawala wa Mkapa, nao walikosa vyeo na fadhila walizoomba kwa rais?

Makampuni 22 yaliyochota kifisadi Sh. 133 bilioni kutoka Benki Kuu yaliundwa na kukamilisha kazi zake wakati wa utawala wa Mkapa. Iweje wanaosema hayo na kwamba huenda watawala walihusika kwa njia mbalimbali, wawe ombaomba wa vyeo na fadhila?

Kuna wanaosema Mkapa na waziri wake wa zamani Daniel Yona, walijichukulia kimyakimya na kwa bei chee, mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira bila kutangaza tenda. Je, ni kweli kwamba wanaosema haya walikosa vyeo walivyoomba kwa rais?

Hivi Mkapa anaweza kuoanisha vipi ombaomba wa vyeo na yeye kuanzisha kampuni akiwa bado ikulu kwa kujiita mjasiriamali?

Kuwa na kampuni inaweza kuwa hoja hafifu kidogo. Kuna kufanya biashara akiwa ikulu. Kutumia muda wa ajira inayolipiwa na wananchi, kufanya kazi zake binafsi. Je, wanaosema hilo ni wale walioomba lakini hakuwapa vyeo?

Na hoja hii ina uzito wa aina yake. Rais analipwa kufanya kazi za urais na anapokuwa amestaafu, anaendelea kulipwa hadi mwisho wa uhai wake. Kutumia muda huo kufanya shughuli za binafsi ni kukosa uadilifu.

Muda wa rais kupanga ikulu ni miaka 10. Rais, familia yake na watumishi wake, bado wanaendelea kulipwa hata baada ya kustaafu. Hivyo anayetaka kufanya biashara anaweza kusubiri amalize ngwe ndipo ajitose katika biashara.

Je, ni sahihi kusema wanaosema rais amekosa uadilifu katika hilo ni wale ambao maombi yao ya kupata vyeo hayakushughulikiwa?

Kijana aliyetumwa kushughulikia uandikishaji kampuni ya rais, ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti benki, bila shaka hakuwa anakwenda kama “mwenyewe” bali mwakilishi wa rais.

Kama hivyo ndivyo, basi alipewa upendeleo wa aina yake kwa kuwa anatoka nyumbani au ofisini kwa rais. Kwa njia hiyo, rais alitumia nafasi yake isivyotarajiwa na kuvunja maadili. Tuseme wanaoona hayo ni wale ambao hakuwapa vyeo?

Kuna mikataba ya kinyonyaji iliyosainiwa wakati wa utawala wa Mkapa. Kuna taratibu na kanuni zilizopitishwa katika kipindi chake. Kuna maagizo yaliyotolewa ambayo yaliathiri maisha ya wananchi. Haiwezekani wote wanaolalamikia yote hayo wawe wale waliokosa vyeo.

Tuchukue uamuzi wa kuuza nyumba za serikali. Kuna wanaoona kwamba hiyo ilikuwa hongo kwa baadhi ya watumishi na kwa viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kuna wanaofikia hatua ya kusema kuwa ni ufisadi wa aina yake, kwani katika jiji la Dar es Salaam, bei ya nyumba iliyouzwa hailingani hata na thamani ya kiwanja! Nani atakubali kwamba wanaolalamikia hilo ni wale ambao rais hakuwapa vyeo?

Kuna madai mengi juu ya mambo mengi ambayo yalifanywa chini ya utawala wa Mkapa na ambayo, ama hayakuswa sahihi au hayakuleta tija. Njia nzuri ya kuyakabili siyo kuyakana au kudai kuwa wayasemao walikosa vyeo.

Katika hili, Bwana Benjamin William Mkapa ajiandae kutoa majibu sahihi; na hata pale anapokana, awe na sababu zilizosimama kwa miguu yote na siyo madai kuwa wanaokosoa wanafanya hivyo kwa kuwa walikuwa ombaomba wa vyeo na hawakufanikiwa kuvipata.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 1 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.