Header Ads

LightBlog

MAFISADI NA UTAWALA WA KIKWETE

SITAKI

Sabuni ya Mkulo haina povu

Ndimara Tegambwage

SITAKI mjadala mpya ulioanzishwa bungeni na Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo juu ya fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zilizoibwa Benki Kuu (BoT).

Hoja ya Mkulo kwamba fedha zaidi ya Sh. 133 bilioni zilizochotwa na makampuni 22 yaliyooteshwa kama uyoga katika kipindi cha wiki mbili hazikuwa za BoT wala serikali, si muhimu na ina lengo baya.

Hii ni hoja inayofuatana na hoja nyingine mbili: Ile inayopinga Kamati Teule ya Bunge na maamuzi yake juu ya mkataba wa Richmond; na ile inayoongoza mkakati wa "kusafisha" watuhumiwa wote katika sakata la Richmond.

Kwa hiyo hoja zote tatu - mapacha haya yanayohusu ufisadi - yameletwa wakati huu kwa shabaha moja kuu: Kuzima moto uliowawakia watuhumiwa, kuwasafisha na kutafuta jinsi ya kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Tuanze na hoja ya fedha za EPA. Hoja ya wizi wa fedha zilizokuwa katika ghala la taifa haiwezi kuwa ile ya kuuliza fedha zilikuwa za nani. Tayari tunajua ndani ya benki kulikuwa na akaunti. Kwenye akaunti hiyo kulikuwa na fedha.

Fedha zilizoko kwenye akaunti ya benki zilikuwa mikononi mwa benki ya umma; siyo kasha la walanguzi wa madawa ya kulevya au wachuuzi wakora wanaobangaiza mitaani. Kuwepo kwa fedha hizo BoT kunaonyesha kuwa umma una maslahi katika fedha hizo au mafao yatokanayo na fedha hizo.

Kwa msingi huo, kuibiwa kwa fedha hizo zilizoko chini ya dhamana ya ghala la umma, kunahusu benki na umma unaomiliki benki, lakini pia kunaathiri mwenendo wa benki ya umma na umma wenyewe.

Popote kule ambako fedha hizo zilitokea, ukweli kwamba zilikuwa BoT, zikihifadhiwa na benki na kuibwa zikiwa mikononi mwa benki, na benki hiyo ni benki ya umma na siyo ya Daudi Ballali wala Mkulo, fedha hizo ni za benki na wale wanaoimiliki.

Hata kama fedha hizo zilikuwa za wafanyabishara, na wenyewe hawazihitaji tena kwa kuwa wameishafidiwa na makampuni ya kwao kutokana na ucheleweshaji malipo, bado fedha hizo zilizoko katika mkoba wa umma, ni za umma.

Vilevile, hata kama wafanyabishara hao wangejitokeza hivi sasa na kukuta fedha zao zimeibiwa, ni benki ya umma ambayo ingewajibika kuwalipa. Lakini hata kama fedha hizo hazikuibiwa, nani asiyejua kuwa fedha hulindwa na bima na ni bima ya benki ya umma iliyokuwa inalinda fedha hizo?

Hata kama wafanyabiashara au serikali zao zilishasamehe madeni kwa waaagizaji, misamaha hiyo ilikuwa kwa taifa na umma wa taifa hili ambao ndio mmiliki wa BoT.

Itoshe kusema kwamba suala la fedha zilikuwa za nani si suala la maana kwa sasa. Suala ni kwamba fedha ziliibwa na nani. Fedha ziliibwa lini? Fedha ziliibwa kwa ushirikiano wa nani? Aliyerahisisha wizi au aliyeamuru uchotaji ni nani?

Hoja ni fedha hizi zilizoibwa zilipelekwa wapi. Ziko mikononi mwa nani? Yuko wapi? Anafanya nini? Afanyweje katika mazingira haya ya ukwapuaji wa wa jeuri?

Kinachofahamika ni kwamba BoT siyo duka la mtaani. Benki inalindwa kwa silaha na bima; kwa mitambo na mbongo. Kinachohitajika ni kujua kama hata viongozi wa nchi walishiriki katika wizi huu mchafu na fedha hizo zilitumikaje.

Hakika hoja haiwezi kuwa ile ya Mkulo, eti fedha hazikuwa za BoT wala serikali. Wala hakuna anayetaka kujua hilo. Na hata kama atatokea anayetaka kujua hilo, hilo haliwezi kuhalalisha wizi kutoka mkoba wa umma.

Sasa ile kauli ya kwamba fedha siyo za serikali wala benki inaletwa kwa shabaha ipi? Ili kuhalalisha wizi? Kwamba kisichokuwa cha serikali wala benki kichotwe tu? Kwamba kilichofanyika ni halali?

Hapana. Kwamba hakuna sababu ya kilio cha serikali, benki na umma? Kwamba Rais Jakaya Kikwete apanguse machozi, azime hasira na asahau kwa kuwa fedha hazikuwa zake? Kwamba hatua zote alizochukua hazikuwa na maana kwa umma bali alikuwa anatumikia watu wa nje?

Hapana. Kauli ya Mkulo inataka kujenga hoja kuwa hata hatua alizochukua Kikwete, kuamuru uchunguzi, kuajiri wataalam na kuahidi kurejesha fedha, zote zinatokana na rais kutojua anachofanya; na kwamba angejua kuwa si fedha zake basi asingejishughulisha?

Hapana. Kwamba hata hatua ya rais kumwajibisha aliyekuwa gavana wa BoT kwa kumfukuza kazi, ilikuwa inatokana na rais kutokujua alichokuwa akifanya? Au hoja ya Mkulo inataka kupendekeza kuwa rais alikuwa anajua anachofanya lakini hakihusiani na uchungu wa fedha za umma? Ni kipi hicho?

Hoja ya Mkulo inataka kutushawishi kuwa hata kinachoitwa juhudi za kurejesha fedha hizo ni kiinimacho na kwamba hakuna kinachofanyika; au kama kipo basi fedha hizo zitaingigwa katika matumizi ya ovyo kwa kuwa "waliokuwa wanadai wengine wamekufa."

Kuna viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali ambao wanadaiwa kushiriki katika wizi huu ndani ya BoT. Kauli za Mkulo zinaashiria utetezi wa ajabu kwa wakwapuaji ambao anataka uambatane na "msamaha." Hili halikubaliki.

Hoja ya Mkulo inakuja wakati mmoja na ufufuaji wa mjadala juu ya Richmond na mkakati wa "kusafisha" watuhumiwa. Hakuna mwenye chembe ya mashaka kwamba "utatu huu" unalenga kuua chuki na hasira ya umma juu ya ufisadi.

Lakini sabuni ya kusafisha mafisadi haijatengenezwa. Hata kiwanda cha kuitengeneza hakijajengwa. Kilichopo ni hoja za kujenga kiwanda au kutowasafisha kabisa; bali kuwatosa wanakostahili na jahazi likaendelea.

Kwa kuzingatia kilichotokea katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na katika mkutano wa pamoja wa wabunge na Halmashauri Kuu hivi karibuni mjini Dodoma, ambapo ziliibuka hotuba za kusugua ufisadi kutoka mwilini mwa watuhumiwa, hoja ya Mkulo yaweza kuchukuliwa kuwa chaguo rasmi la kuzima tuhuma.

Wakati taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya watuhumiwa katika Richmond wako pia katika EPA, hoja ya Mkulo inachukuliwa kuwa sehemu ya mkakati wa "kulindana." Lakini sabuni ya Mkulo haina povu.

Rais Kikwete atawalinda wangapi? Atafikia mahali atashindwa hata kujilinda; atakuta amewekwa katika kapu lao. Ni hapa ambapo wachunguzi wa mwenendo wa siasa za Tanzania wanauliza, "Je, Kikwete atabadilisha baraza lake la mawaziri mara ngapi kupata watu makini?"

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 29 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.