Serikali na utata wa Ballali
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI serikali ijiingize kwenye utata wa kutoeleweka, kutoaminika na kutothaminiwa.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, ni serikali ambayo ilisema haijui aliko Dk. Daudi Ballali, yule aliyekuwa gavana wa Benki Kuu (BoT) na ambaye alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na kusema kwamba Ballali anaumwa na yuko kwenye matibabu nchini Marekani, serikali ilikataa kusema mambo mengi juu ya mtu muhimu katika jamii.
Ilikataa kusema yuko katika jimbo gani nchini Marekani. Ilikataa kusema amelazwa hospitali gani. Ilinyamazia ugonjwa unaomsubua gavana; ilikataa kutoa taarifa juu ya hali yake kadri ilivyoendelea na ilikataa kusema kifo chake kimetokana na nini.
Ukimya huu ulizaa mashaka. Ulizaa utata. Ilifikia mahali wananchi wakauliza, tena kwa kishindo na mfululizo, iweje serikali isijue wapi amelazwa mtu muhimu kama gavana wa benki.
Leo hii, Ballali hayupo. Amefariki. Taarifa zinasema alifariki Mei 16, Ijumaa ya wiki iliyopita. Lakini kauli ya serikali ilitoka siku tano (5) baada ya kifo cha Ballali.
Hata kauli ya serikali ilishinikizwa na waandishi wa habari watukutu walioizonga wakitaka itamke kama Ballali amefariki kweli au ulikuwa uvumi.
Ukimya huu unaendelea kuzaa utata na mashaka. Kifo cha Ballali kimekuja wiki mbili baada ya serikali kusema kuwa haimhitaji Ballali kwa sasa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu aliwaambia waandishi wa habari kuwa “serikali ikimhitaji Ballali utampata” na kwamba serikali ina mkono mrefu.
Sasa tuone ukimywa huu wa serikali ulivyo na athari kwa utawanyaji habari. Mmoja wa wasomaji wa safu yangu hii, ameniaandikia ujumbe wa simu. Unasema hivi:
“Jamani ninyi waandishi wa habari, hamjui wala kutafakari. Mwili utakaochomwa moto (wa Ballali) sio wa mtu halisi, lakini Ballali mwenyewe wala hayupo Washington. Hii ni njama imeandaliwa kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa. Namba yangu (ya simu) msiitoe popote tafadhali. Baada ya kuisoma hii, uifute. Ni mimi raia mwema.”
Huyo ni msomaji mmoja. Wapo wengi walioandika juu ya Ballali na “madai” kuhusu kifo chake. Wakizingatia kuwa serikali imekuwa ikikataa kutoa taarifa, wana haki ya kupokea hata uvumi na kuuamini.
Lakini kama nilivyowahi kuandika katika kitabu changu, “Who Tells The Truth In Tanzania?” (Nani Msema Ukweli Tanzania), kila uvumi una asili na chimbuko lake.
Kwa wote waliofuatilia suala la wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka BoT; walioshuhudia Rais Kikwete akiunda Kamati ya kurejesha mabaki ya mabilioni hayo na wanaofuatilia kauli za viongozi, kifo cha Ballali, kama kimetokea, kinaweza kutafsiriwa kwa njia nyingi.
Mhusika mkuu wa tafsiri nyingi za wananchi wengi ni serikali. Ni serikali iliyoficha ukweli wa mahali alipo Ballali kwa kudai kuwa haijui.
Ni serikali iliyokataa kumtafuta Ballali akiwa hai, kumrejesha nyumbani ili asaidie katika kutoa taarifa juu ya uchotaji wa mabilioni ya shilingi kutoka BoT.
Kauli kwamba Ballali siyo mtuhumiwa na wala hahitajiki kwa sasa, siyo tu zinazidisha utata, bali pia zinathibitisha kushiriki kwa, ama watendaji au serikali yenyewe katika ufujaji wa fedha za umma.
Na hapo ndipo vinapatikana viini vingi vya taarifa zisizorasmi. Kwamba kama Ballali angerudi nchini na kupewa kibano, angetaja nani alimwamuru kuvunja misingi na maadili ya kazi yake.
Kwamba walioko kwenye utawala na waliostaafu wangekumbwa na “tsumani ya ukweli” usiopingika kuwa walishiriki ufisadi usiomithilika.
Kwamba fedha zilizothibitika kukombwa, Sh. 133 bilioni, kweli ni “vijisenti” kwani hizo ni kutoka akaunti moja tu katika mwaka mmoja wa fedha.
Iwapo akaunti zote zingepitiwa, ungekuta ni mamilioni ya mabilioni ya shilingi ambazo zilikombwa. Mwenye taarifa hizo ni Ballali.
Kwamba huenda ni kweli Ballali alikuwa anaumwa na watawala waliona hawezi kupona; hivyo wakaamua wamwache “afe salama” bila usumbufu wa nyongeza.
Kwamba huenda kipindi cha miezi sita ambacho Kikwete alitoa kwa kamati yake kufuatilia mabilioni yaliyokwapuliwa benki, kilikuwa kinalingana na muda ambao Ballali alikuwa amebakiza kuaga dunia.
Kwamba kwa vyovyote vile, hakuna mtawala ambaye angekubali Ballali arejee nchini na kuruhusiwa kufungua kinywa chake. Ama angeapishwa kuwa atakaa kimya au angenyamazishwa kwa vyovyote vile.
Kwamba hakuna, miongoni mwa wanufaika wakuu wa ukwapuaji BoT, aliyetaka hata Ballali aendelee kuishi, kwani walijua kuwa iwapo ataendelea kuwapo, popote pale duniani, na katika utulivu wa akili na afya njema, angeweza kufikika na taarifa ambazo angetoa zingekuwa za madhara makubwa kwao.
Kwamba inawezekana kabisa kuwa ukimya wa Ballali, mke wake, watoto wao, ndugu zake, jamaa na marafiki zake, uliundwa rasmi na genge la mafisadi. Walinyamazishwa kwa vitisho, ahadi na “mishiko” hadi alipofariki.
Kwamba ndugu na jamaa hao walilishwa yamini, kuwa hata baada ya kifo chake, asitokee wa kuinua kidole au kichwa na kutoa kauli inayomwakilisha Ballali, yenye uwezekano wa kuwaangamiza wakwapuaji.
Yote haya yamesababishwa na ukimya wa serikali. Vyovyote vile ambavyo serikali ingetaka kufanya, ingekuwa vizuri kama ingekuwa inatoa taarifa, hata kama zisingekuwa zinakubalika moja kwa moja kwa wananchi.
Hakuna ubishi kuwa Ballali alifukuzwa kazi. Lakini alibaki hazina muhimu ya taarifa ambazo zingesaidia serikali kurejesha mabilioni ya shilingi za umma na angalau kuwa na ukweli juu ya waliozichota na kwa amri au pendekezo la nani.
Kama kweli Ballali amekufa na kuzikwa, basi amezikwa na hazina ya taarifa muhimu. Hii inatokana na jeuri na ubabe wa baadhi ya wale waliotakiwa kupata kauli yake kabla ya juzi.
Hapana. Labda siyo ubabe wala jeuri. Labda ni kwa kuwa wanaohusika ni wahusika pia katika ukwapuaji.
(Makala hii itachapishwa katika Tanzania Daima Jumapili ya 25 Mei 2008. Mwandishi anapatikana pia kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments
Post a Comment