Header Ads

LightBlog

UFISADI NDANI YA BUNGE

SITAKI:
Ukumbi wa Bunge unapokuwa ‘hautoshi’

Ndimara Tegambwage
SITAKI ukumbi wa Bunge mjini Dodoma uwe mdogo kiasi cha Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki kutamka wazi kwamba “hapatatosha.”

Kumefurika. Joto limetawala. Hewa haitoshi. Anne Malecela anahema. Anatweta mithili ya aliyemaliza mbio fupi zenye ushindani mkali.

Anne alikuwa akijadili hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, ambapo alitaka wezi wa fedha za umma zipatazo Sh. 133 bilioni, kupitia Benki Kuu (BoT) sharti watajwe kwa majina.

Ni Anne aliyekumbusha pia juu ya Sh. 216 bilioni zilizokopwa mwaka 1992, kupitia mpango wa uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje, ambao wamekataa au wameshindwa kuzirejesha.

“Patakuwa hapatoshi hapa,” aling’aka Anne “iwapo fedha hizo hazitarudishwa” na majina ya wachotaji kutajwa hadharani.

Kumbe tatizo siyo viti au eneo la ukumbi wa bunge. Tatizo ni kwamba utazuka mgogoro mkubwa, mvutano, patashika ya fulana na sidiria kuchanika.

Na tayari pameanza kuwa finyu. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Anna Abdallah (Msekwa), mbunge viti maalum, ameanza kukosa hewa. Juzi Ijumaa, badala ya kujenga hoja yake, alisimama bungeni na kuanza kuchambua Anne Malecela tena kwa kauli dhaifu

Waziri wa fedha Mustapha Mkulo naye ameanza kukosa pumzi. Anasema fedha za EPA hazikuwa za serikali wala BoT; bali zilikuwa za wafanyabiashara kupitia benki ya NBC na kwamba zilirudishwa BoT kutokana na kushindwa kupata fedha za kigeni.

Fedha za kigeni hupatikanaje? Fedha zilizoko chini ya uangalizi wa BoT zikichotwa, kwa mtindo wa EPA, nani analipa? BoT kama dude la kuchunga na kusimamia fedha na uchumi wa nchi, lenyewe litapata wapi fedha za kufidia kama siyo fedha za umma?

Lakini hoja kamambe ni kwamba makampuni yaliyolipwa fedha za EPA siyo yaliyostahili kulipwa. Mkulo anataka turudie uchunguzi na kuwavua nguo wahusika wote na mara hii bungeni? Hakika hapatatosha.

Hadi sasa, wajumbe wa Kamati ya Rais Jakaya Kikwete wanaochunguza na kufuatilia fedha hizo, watendaji wa kamati, hata polisi wanaotoa ulinzi, wanalipwa na nani?

Kama wanalipwa kutokana na fedha zinazokusanywa, je kule ambako walistahili kufanya kazi, upungufu uliopo wa raslimali watu unafidiwa na nani; na fedha kutoka wapi? Fedha za umma!

Gharama za kulipa maodita wa Ernst & Young waliogundua ukwapuaji EPA; gharama zinazohusisha rais kuingiza ndani ya ratiba yake ya kila siku masuala ya EPA; gharama ya muda wa bunge kujadili na kuisisitizia serikali kuwa wazi; zote hizi zinalipwa na nani kama siyo umma wa nchi hii?

Kauli ya Mkulo inamsogeza zaidi karibu na kusema fedha za EPA “zilistahili kuchotwa kwa kuwa hazikuwa na mwenyewe.” Sitaki kuamini hiyo; na hili litafanya ukumbi wa bunge pawe padogo zaidi.

Tuachane na kuhema kwa Anna Abdallah na kutokwa jasho kwa Mkulo. Turejee kwa Anne Kilango. Hii ni mara ya kwanza kwa mbunge kuonya serikali kwa ukali kuhusu ufisadi. Lakini Anne anataja matukio mawili ya jumla ya Sh. 349.

Kama kiasi hicho kitafanya bungeni pasitoshe, basi yakitajwa makubwa zaidi baadhi ya wabunge watakimbia mijadala; baadhi watazimia kwa kukosa pumzi; wengine wataaga dunia na bunge litalipuka kwa moto.

Kuweni na akina Anne 10 tu. Waiambie serikali kuwa bilioni 40 za kununua ndege ya rais zilitumika vibaya na waishinikize iiuze! Hakika bungeni hapatatosha.

Naibu Waziri wa Fedha, Omar Yusuf Mzee, akijibu hoja za wabunge, anasema uuzaji ndege ya rais unatoa chanzo cha mapato ambacho siyo endelevu.

Waziri, ama kwa kutojua au kwa kupuuza au kwa kusahau darasa, anakataa kuona kwamba ndege ya rais ni chanzo cha Hasara Endelevu, hivyo sharti hasara hiyo isitishwe.

Tayari bungeni panaanza kutotosha. Hapatatosha hata kidogo pale wabunge watakapohoji waliokula mlungula kutokana na ununuzi wa ndege hiyo na hata rada ya kijeshi iliyonunuliwa kwa zaidi ya Sh. 70 bilioni. Wahusika watazimia.

Itakapotakiwa kutaja hadharani majina ya wote waliokula mlungula katika mradi wa umeme wa IPTL; wahusika watagongana vichwa langoni.

Hakika bungeni hapatatosha yakihitajika maelezo ya kina juu ya makampuni ya umeme ya Aggreko na Songas ambayo gharama za umeme wao ni njia ya kuangamiza nchi.

Atoke wapi wa kubakiwa na pumzi pale mchakato mzima wa kuajiri kampuni ya Net Group Solutions ya Afrika Kusini utakapowasilishwa mbele ya bunge? Kikundi kidogo cha nje ya nchi kuingizwa ofisini kwa kutumia FFU! Kwa maslahi ya nani?

Nani hatasikia joto la kupasua misuli ya kichwa pale majina ya wahusika wakuu wa Richmond, ile kampuni hewa, ilivyoshinda zabuni na baada ya kushindwa kuitekeleza ikaiuza kwa kampuni ya Dowans?

Hewa itatoweka kabisa pale serikali itakapobanwa kwa nini haijafikiria kununua makampuni haya ya umeme na kuweka mwisho wa unyonyaji wa kikatili uliokuja kwa njia ya mlango wa nyumanju.

Je, itakuwaje pale serikali itakapotakiwa kueleza nani mmiliki wa kampuni ya uchimbaji madini ya Meremeta? Joto tupu.

Je, watakapotaka kujua mapato ya Meremeta kwa miaka sita ya biashara yake yalikuwa kiasi gani na nani alinufaika nayo? Kama wahusika hawakutoka bungeni kwa mbio, lazima watazimia tu.

Fikiria pale serikali itakapobanwa kueleza nani wamiliki wa kampuni ya Tangold iliyochotewa mabilioni ya shilingi kutoka BoT. Kuna kuzimia.

Na Tangold bado ina utata mkubwa. Serikali ina ndimi mbili juu ya kampuni hii. Huku inasema ni kampuni inayomilikiwa na serikali moja kwa moja, na huku kuna taarifa kwamba ilianzishwa nje ya nchi.

Vipengele vya kampuni inayodaiwa kuwa ya serikali vinaonyesha kuwa inaweza kurithishwa kwa ndugu. Ni serikali gani hiyo? Kama wahusika watahijaka kutajwa bungeni, hakina hewa itapungua.

Bado kampuni ya kuchimba madini ya Barrick imezongwa na utata. Iwapo vituko vya kusainia mkataba nje ya nchi vitaibuliwa; utiaji saini mwingine nchini kufanywa usiku na wahusika kukiri kuwa hawakusoma mkataba; basi sharti serikali itoe majibu vinginevyo hapatatosha.

Jaribu kuona hili. Ni akaunti moja ya EPA ya BoT iliyokaguliwa kwa shabaha ya kugundua wizi. Kuna akaunti zaidi ya 10. Je, wabunge 10 wakiibana serikali ionyeshe uchunguzi ndani ya akaunti nyingine, kwa nini wahusika wasizimie mbele ya spika?

Kuna madai ya gharama za kughushi kwenye majengo mawili ya BoT – Minara Pacha – jijini Dar es Salaam. Wawakilishi wakitaka kila senti ihesabiwe, iko wapi pumzi ya kuhimili vishindo?

Mlungula katika kampuni ya maodita ya Alex Stewarts, nyongeza ya muda wa miaka 10 kwa kampuni ya makontena ya TICTS na udhaifu ndani ya kampuni ya ukaguzi wa mizigo bandarini – TSCAN. Yote yanakula hewa.

Mengine ni pamoja na ubinafsishaji wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira katika mazingira ya uficho; uuzwaji wa mgodi wa thamani ya maelfu ya mabilioni ya shilingi kwa “bei ya bure” ya Sh. 700 milioni. Ni kiasi cha Sh. 70 milioni tu zilizokwishalipwa. Hapa lazima mtu azimie.

Hata haya ni machache. Kuna mengi zaidi. Lakini kama wabunge watakuwa thabiti na kudai majibu kama Anne Kilango Malecela; kama serikali haitatoa majibu hayo, hakika ukumbi wa bunge patakuwa hapatoshi.

Na basi pasitoshe. Lakini sharti serikali itoe majibu sahihi kwa maswali ya wabunge. Anne ameanza na mawili: EPA na mikopo. Fedha zirudishwe. Wahusika watajwe. Mengine yadaiwe hatua kwa hatua.

Ukweli ukiwekwa wazi na majibu sahihi kutolewa, joto ndani ya bunge litapungua au hata kuisha. Patakalika. Pataheshimika. Hata Anne ataona panatosha.

(Makala hii itatoka katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili tarehe 22 Juni 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.