Header Ads

LightBlog

BAJETI YA TANZANIA 2008/2009

Hili la mafuta, serikali imefeli


Na Ndimara Tegambwage

NINI maana ya bajeti hii ya mwaka 2008/2009? Tuangalie eneo moja: Bei ya mafuta ya taa, dizeli na petroli.

Kuna kauli kwamba serikali “imefanya vizuri kwa kutogusa bei ya mafuta.” Kwamba serikali haikupandisha bei ya bidhaa hiyo katika bajeti ya mwaka huu.

Huu ni uwongo au ni upogo wa mawazo. Serikali imeongeza bei ya mafuta, tena kwa kiwango kikubwa. Haikutaja mafuta kwa kuwa inaona wananchi hawataielewa. Wataisuta. Wataikasirikia. Watataka kuikanya na hata kuikana.

Sasa tujadili. Kwamba serikali haikutaja kuwa haikuongeza bei ya mafuta haina maana kwamba haikuongeza bei hiyo. Ukweli ni kwamba kimya hicho kina maana kwamba serikali imebariki kupanda kwa bei na bila ukomo.

Kwa hiyo hali ni kama ifuatavyo: Serikali imewasilisha bungeni bajeti ambayo inaweza kutibuliwa wakati wowote.

Mtibuaji mkuu ni mafuta ambayo serikali iliishajivua udhibiti wa bei yake na anayeumia zaidi ni mwananchi anayenunua huduma na bidha ambazo tayari bei zake zimeathiriwa na usafiri ghali.

Kuna matumizi makubwa katika shughuli za serikali. Hayo ni mbali na misafara ya viongozi mijini na vijijini na misururu ya magari hadi 20 hata 30 wakati wa misafara ya rais, makamu wa rais na waziri mkuu. Kwa hayo, ongeza matumzi binafsi ya mafuta katika safari za viongozi.

Hali ndivyo ilivyo pia katika sekta binafsi. Lakini huko pia kuna suala kubwa la uzalishaji. Mitambo ya kuzalisha umeme pindi umeme wa jumla unapokatika, inategemea mafuta yaleyale. Lakini pia usafirishaji wa bidhaa unategemea mafuta.

Angalia wenye mabasi makubwa yaendayo safari za mijini na nje ya mipaka ya mikoa yao. Hutumia mafuta mengi. Hivi sasa tayari wamiliki wengi wameanzisha kasheshe kwa kutoza viwango vya nauli wanayotaka bila hata kusubiri mamlaka husika kuridhia.

Wasafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi hutumia bidhaa hii ya mafuta, tena kwa kiwango kikubwa. Imefikia hatua dizeli, mafuta ambayo yanatumiwa zaidi na magari makubwa ya usafiri na usafirishaji, imekuwa na bei kubwa kuliko petroli.

Katika mazingira ambamo serikali iliishasema kuwa “inajivua biashara,” na kuacha bei za mafuta ziende kwa mtindo wa soko huria na holela, sasa umekuwa “uwanja wa fujo.” Katika uwanja huu, anayeumia zaidi ni mwananchi, tena wa ngazi ya chini katika jamii.

Bila udhibiti au juhudi zozote za kulinda watumiaji, kila mwenye chombo cha usafiri amekuwa “kambale” – ameota ndevu – kwa maana ya kufanya atakalo huku akijua hakuna wa kumuuliza.

Katika mazingira haya, kwa serikali kutosema lolote juu ya mafuta ya taa, dizeli na petroli maana yake ni rukhusa kwa wafanyabiashara kufanya watakalo; ikiwa ni pamoja na kuinyonga bajeti ambayo serikali imetangaza kwa mbwembwe.

Maana yake ni kuwasukuma wananchi langoni kwa “jehanamu,” kwani kila huduma ya usafiri na usafirishaji itapanda na matokeo yake ni gharama kumshukia mtumiaji wa vyombo vya usafiri na bidhaa iliyosafirishwa.

Inafika mahali wananchi wanaanza kujiuliza, “Nini hasa sababu ya hatua ya serikali ya kunyamazia gharama ya mafuta?”

Yawezekana siyo visingizio vya awali kwamba inajitoa kwenye biashara. Yawezekana kabisa ni hatua madhubuti ya kutetea waliomo katika biashara hii na huenda hata baadhi ya waliomo serikalini ambao wana maslahi katika biashara ya mafuta.

Ukimya wa serikali basi kuhusu bei ya mafuta, ni wa kishindo. Hatua za sasa za serikali kutaka kujua taratibu za wafanyabiashara na mifumo yao ya kuagiza na kuuza mafuta, hazitoshi kumhakikishia mwananchi na hata serikali, kwamba bei haitapanda.

Ukweli ni kwamba bei zitaendelea kupanda. Kitu ambacho serikali ingefanya na kuonekana kuwa inajali na inajua wajibu wake, ni kama ifuatayo:

Kwanza, kukubali kuwa sera yake ya kuachia mafuta kuwa mikononi mwa wafanyabiashara binafsi na ambako serikali haina usemi, ni dhaifu, ya kukurupuka na inayotoa mwanya kwa wafanyabiashara hii kukamua uchumi wa nchi.

Hapa tunaweza kusema, kwa chembechembe za ukahika, kwamba waliobinafsisha eneo hili, ama waliona ubinafsishaji ni “fasheni tu” ya wakati huo, au ni kwa kuwa walikuwa wanajenga viota vya maslahi yao.

Pili, kufanya uamuzi mzito wa kuweka mkono wa serikali katika biashara ya mafuta au kuichukua kabisa na kuiendesha na kuacha kukimbia wajibu wake wa kusimamia eneo nyeti linalohusu maisha ya taifa na watu wake.

Tatu, kuunda mfuko maalum wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta. Mfuko huu unaweza kutumika kupunguza makali pindi yanapojitokeza, kwa kufidia pengo litokanalo na mfumuko.

Kwa mfano, kwa kutambua kuwa bei za mafuta zinapanda, bila idhini wala utashi wa wananchi na serikali; na bila kuwa na uwezo wa kubadili mkondo huo kuanzia kule ambako mafuta yanatoka; basi unaundwa mfuko maalum wa kupunguza makali ya bei na gharama nyingine za ugavi wa mafuta.

Nne, hata inapokuwa biashara ya mafuta imerejeshwa mikononi mwa serikali, makampuni au mashirika yake, sharti kuwepo na uadilifu wa kiwango cha juu kwa watawala na watendaji serikalini.

Kinacholeta mgogoro mkubwa na ambacho kinaweza kusababisha sera zote kushindwa, ni baadhi ya watawala na watendaji serikalini kuwa na ubia au maslahi ya kifedha katika biashara hii.

Huku wana ubia katika makampuni hayohayo yanayoagiza mafuta. Huku wanalia kuwa bei za mafuta zimepanda. Huku wanaketi na wenzao serikalini kutafuta ufumbuzi. Huku wanatafuta jinsi ya kukwepa kodi. Huku wanachelekea kama nyani kileleni mwa mwamba uliochongoka.

Katika hali hii hakuwezi kupatikana ufumbuzi. Miongoni mwa waagizaji wa sasa, ama hakuna mwenye uwezo kifedha au mwenye maslahi ya nchi moyoni, wa kuweza kufikiria hata nafasi ya kuwa na “ghala” kubwa la mafuta ya kutumia kwa muda mrefu.

Kama inavyobidi kuweka akiba ya chakula kwa muda mrefu, iwe wakati wa neema, njaa au vita, ndivyo pia serikali yenye mipango mizuri inavyopaswa kufikiria suala la kuwa na akiba ya mafuta.

Kutegemea mafuta kuwa ajenda ya kisiasa ya kuhalalisha kutofanikiwa kwa mipango ya serikali, ni kukiri kushindwa wajibu; ni kuomba kufukuzwa kazi.

Katika hili la bei ya mafuta, serikali kwa kutolitaja kwenye bajeti au kuonyesha jinsi ya kulikabili, imelibariki na imeshiriki kujenga mazingira ya maangamizi ya watu wake, bila woga wala aibu.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano, 17 Juni 2008.Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.