Header Ads

LightBlog

WATAWALA WANAVYOJARIBU KUKIMBIA UWAJIBIKAJI

Spika anayetetea uhalifu wa serikali

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali, kwa ushirikiano wa Spika Samwel Sitta, ifikiri kuwa wananchi wote ni wajinga wa kutupa. Hii ni katika suala la Kampuni ya kupakua Makontena Bandarini Dar es Salaam (TICTS).

Hoja ilijengwa bungeni kwamba hatua ya kuongeza miaka 15 kwenye mkataba wa TICTS kufikia miaka 25, hata kabla mkataba wa kwanza wa miaka 10 haujamalizika ilikiuka sheria.

Sasa Spika analiambia bunge kuwa amethibitishiwa na ikulu kwamba “Mkataba wa TICTS ulifuata taratibu zote za kiserikali,” akizingatia kauli za awali za mwenye TICTS, Nazir Karamagi kuwa mkataba uliongezwa muda na Baraza la Mawaziri.

Nani alikuwa anabisha kuwa mkataba haukufuata taratibu za serikali? Nani alikuwa anapendekeza kuwa mkataba ulifuata “taratibu chache” na siyo zote za serikali? Hoja hiyo inatoka wapi? Wewe na mimi tunajua mkataba ulifuata taratibu za serikali. Na hapo ndipo kuna hoja kuu.

Hoja kuu siyo uthibitisho wa ikulu kuwa zilitumika taratibu zote za serikali. Hoja ni hii hapa: Kwanza, kwamba taratibu za serikali zilipindwa au zilivunjwa, tena kwa makusudi au kwa kichocheo au motisha maalum na wa aina yake.

Hii inatokana na serikali na viongozi wake kutamba na kujinoma kuwa ni wasafi; kuwa wanawajibika kwa umma na kuwa wana utawala wa sheria.

Penye majigambo ya aina hii, sharti tutegemee uadilifu. Kama kuna lolote lisilofanana na uadilifu, basi kutakuwa na kikwazo au motisha uliowageuza wahusika wakatenda kinyume na mahubiri yao.

Pili, sehemu nyingine ya hoja hii ni kwamba serikali imevunja sheria ya nchi ya kutoa zabuni – Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004.

Watawala na maofisa wao – wale wanaoitwa serikali – wakitumia tataribu za serikali kama walivyojiwekea, walivunja sheria iliyotungwa na bunge.

Ni hivi: Kwamba serikali imevunja Sheria ya Manunuzi Serikalini kama ilivyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na kusainiwa na Rais Benjamin Mkapa; ambaye serikali yeke mwenyewe ndiyo ilivunja sheria hiyo badala ya kuisimamia.

Kilichosemwa na Spika Sitta basi, ni kukiri kuwa serikali ilitumia taratibu zake kuvunja sheria; kwamba bunge limeshindwa au limelegalega katika kuisimamia serikali; kwamba sasa serikali na Spika, wanatumia ubabe kueleza kuwa hoja imejibiwa na “hakuna zaidi.”

Ni muhimu kuelewa kuwa, pale penye sheria, rais hana mamlaka ya kuagiza kilabu cha pombe au choo kichafu mjini kufungwa; au basi la daladala kubadilisha njia yake. Si kazi yake. Si mahali pake.

Bibi na Bwana Afya wa mtaa, kitongoji au Kata watafanya nini kama kazi zao zitafanywa na rais? Mamlaka za usafiri zitafanya nini iwapo rais au baraza lake la mawaziri watajihusisha na kupanga njia za magari?

Vivyo hivyo, penye sheria iliyo wazi na iliyotungwa kudhibiti rushwa na upendeleo mchafu, hakuna “taratibu za kiserikali” zenye mamlaka ya kupendelea mtu yeyote na kumwongezea miaka 15 kwenye mkataba wa awali na ulioingiwa kisheria.

Taratibu hizo za kiserikali zinakuwa zimekufa, hasa pale serikali inapokuwa imepeleka muswada bungeni na muswada ukatungiwa sheria na rais akasaini sheria hiyo kuanza kutumika. Hii ni bila kujali kama rais ni rafiki wa kampuni au wakurugenzi wake.

Ni hivyo pia kwa Baraza la Mawaziri ambalo kiongozi wake ni rais. Baraza halina uwezo wa kuvunja sheria ya nchi, tena wakati hakuna dharura yoyote, na kupendelea mtu au kampuni kwa madai kuwa “limefurahishwa na utendaji.”

Katika mazingira ya Tanzania, ambako miswada karibu yote inatoka serikalini, mabadiliko yoyote ya sheria ambayo rais na baraza lake wanataka kufanya, yaweza kuja kwa njia ya muswada wa marekebisho na siyo maagizo ya “kutoa zawadi” za pembeni.

Spika asiingize taifa katika mjadala usio na mafao wa kutumika kwa “taratibu zote za kiserikali” kuvunja sheria ya nchi. Hoja ni kwa nini serikali imevunja sheria.

Katika mazingira ya kuwa na taratibu za kiserikali zinazovunja sheria iliyowekwa rasmi kukabiliana na rushwa, lazima zitajitokeza tuhuma kwamba wahusika walihongwa. Nani anaweza kuepa tuhuma hizo?

Kama serikali inavunja sheria, nani ataonyesha mfano wa kufuata sheria? Kama spika wa bunge atakubaliana na serikali kutoa majibu ya kijuujuu, iko wapi nafasi ya bunge ya kushauri na kusimamia serikali?

Hapa kuna waliotenda uhalifu; kwa kuvunja sheria. Kuna serikali iliyetenda uhalifu na ambayo inaendelea kulinda uhalifu na wahalifu. Somo tunalopata ni kwamba serikali nzima inaweza kuwa na wahalifu watupu.

Huo ndio mwanzo wa wananchi kulia na kusaga meno; lakini pia ndio mwanzo wa kuanza kujiuliza ni hatua gani wachukue kujiondoa zimwi mgongoni.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 13 Julai 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.