‘Kochonkocho’ dhidi ya ufisadi
Vijiko, uma, sufuria silaha muhimu
Na Ndimara Tegambwage
WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa katika vyombo vya habari juu ya vijana waliokamatwa kwa madai ya “kumtukana” rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Kutukana ni kosa la jinai. Siyo kwa kumtukana rais au aliyekuwa rais peke yake, bali mtu yeyote. Lakini habari hizo hazikusema ni matusi yapi alitukanwa kiongozi wa zamani anayelindwa na askari na sheria za nchi.
Katika baadhi ya nchi duniani, rais aliyemaliza muda wake huendelea kuitwa rais; hata neno mstaafu halitumiki. Ni heshima ya kudumu. Marais hufa na urais wao hata baada ya kumaliza vipindi vyao vya utawala.
Hayo ni mema unayoishi nayo hadi kuzimuni. Lakini ukilikoroga, umati ukakuona, “aha, ni fulani kama mwingine,” basi utadonolewa kama ndege wadonoavyo hindi.
Taarifa za vyombo vya habari zinasema waliokamatwa walikuwa wakiimba, “Fisadi! Fisadi! Fisadi! (mara tatu) wakati rais mstaafu akipita eneo walikokuwa.
Hakuna maelezo iwapo walikuwa wameelekeza “nyimbo” hizo kwa Mkapa au walikuwa wakiziimba kabla hajafika au walikuwa wakifanya mazoezi kwa ajili ya kusanyiko tofauti.
Lakini katika mazingira ambamo rais mstaafu amekuwa akitajwa kukiuka maadili ya uongozi na amekataa kujitokeza kujibu tuhuma; basi inawezekana, nasema huu ni uwezekano tu, kwamba walikuwa wanapeleka ujumbe.
Ni suala la kusubiri hadi mahakama itoe uamuzi. Hiyo ni kama watashitakiwa.
Na ujumbe huu ni maoni binafsi. Hata kama ulikuwa umemlenga Mkapa, mtu haadhibiwi kwa maoni yake, tena ambayo yamejengeka kwa kipindi kirefu na bila ya kusahihishwa, kurekebishwa, kubadilishwa kwa kauli au vitendo, vya yule anayetuhumiwa.
Hata kutaja majina, ingawa taarifa hazisemi vijana hao walitaja jina la mtu yeyote, hakuna uzito. Katika mazingira huru, na mara hii wakati wa wiki ya uhuru wa kufikiri na kuwa na maoni, tendo la vijana hao linazusha mjadala wa maana kwa ustawi wa uhuru na haki ya kuwa na maoni na kujieleza.
Nchini Venezuela kuna mapambano kama yaliyopo nchini Tanzania. Ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Na rushwa na ufisadi wa Venezuela umejikita serikalini na katika biashara kubwa.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimefanya kazi ya kuwataja watuhumiwa na wala rushwa na mafisadi wenyewe. Majina yao yanafahamika. Majina yao yanaimbwa asubuhi, mchana na usiku.
Hapa ndipo mwanzo wa “kochonkocho.” Kaeni ndani ya mgahawa au hoteli. Wakati ukiwa pale, acha aingie mtuhumiwa au yule ambaye amethibitika kuwa mwizi serikalini, katika jeshi au mwanasiasa mkwapuzi. Utashangaa.
Caracas, ambako ni mji mkuu wa nchi hiyo, ndiko kuna vimbwanga. Akiingia fisadi, wale wanaomtambua huanza mara moja mchezo wa kochonkocho. Huanza kugonganisha vijiko, uma na visu.
Ghafla, kila mmoja hustuka na kuuliza kuna nini. Ndipo zogo hukolea. Wengine huanza kugonga glasi, sahani na meza kwa kutumia vijiko, uma au visu.
Mchezo huu, ambao hasa siyo mchezo bali kazi takatifu, hufanywa kwa ustadi, bila kelele nyingine za mdomo na humfanya mtuhumiwa, ambaye ni mlengwa, ama kukaa kimya na “kuzimia kiofisa” au kutoka nje ya mgahawa au hoteli.
Zogo hilo ambalo huanzishwa na wenyeji wa miji husika, huungwa mkono mara moja na wageni katika mahoteli na migahawa ambao huwa wameambiwa kinachoendelea.
Mambo hayaishii hapo. Kuna kindumbwendubwe cha mitaani. Mtuhumiwa wa wizi au mwizi kweli aliyethibitika; mtuhumiwa wa ufisadi au fisadi aliyekubuhu aliyethibitika, hupata wakati mgumu.
Pindi mtuhumiwa au mthibitika anapoonekana mitaani, akina mama hupeana taarifa harakaharaka. Hutoka nje wakiwa na sufuria, madebe, ndoo na vikaango. Kazi huwa moja.
Akina mama hao hugonga vyombo hivyo kwa nguvu. Vyombo vitupu. Hakuna sauti ya mtu. Nkochonkocho ya vyombo hujaa mtaa mmoja; huenea hadi mtaa mwingine; husambaa mitaa mingine ambako mtuhumiwa au mthibitika anapita.
Hatua hiyo ambayo nchini Venezuela inaitwa Cacerolazo, ina shabaha ya kuonyesha kwamba muhusika ni mtu aliyekataliwa na jamii; asiyetakiwa, mwenye kasoro; aliyejaa hitilafu na duni kimaadili.
Huu ni mzigo mkubwa. Ni adhabu ya kijamii. Ni utashi wa jamii iliyochoka matendo ya wizi na ufisadi. Ni kumkataa mtu, familia yake na wote ambao wanatuhumiwa kushirikiana naye katika wizi na ufisadi.
Nchini Venezuela wazomewaji ni pamoja na mawaziri, wakurugenzi na maofisa wa ngazi ya juu serikalini, viongozi wa majeshi, watendaji wa ikulu na rais mwenyewe. Ukitajwa unaandamwa.
Nguvu ya umma ya mtaani ina uwezo mkubwa nchini Venezuela kuliko vyama vya upinzani. Vyama vikiandamana kueleza kutoroshishwa na serikali na vitendo vya ufisadi, wafuasi wa rais hufungulia kila silaha mitaani.
Silaha ambayo hadi sasa ni kubwa katika kukabiliana na wizi, rushwa na ufisadi; angalu inayowanyima usingizi watuhumiwa au wathibitika, ni umma ulioko mitaani; ukitumia vijiko, uma, visu, sufuria, ndoo na vyombo mbalimbali vya nyumbani.
Hii ni kazi moja ya kuzomea na kupeleka ujumbe mfupi wenye maana ndefu, kubwa na pana: Kwamba tayari tunawafahamu. Siku ya kuamua kuwasaka, tujaua mahali pa kuwapata.
Yawezekana Tanzania, na hasa Dar es Salaam na miji mingine inaelekea Caracas, Venezuela. Sauti za uma, vijiko na visu ni sauti za watu.
Sauti za sufuria, vikaango, glasi na sahani, siyo tena za vyombo vinavyovunjikia jikoni. Ni sauti ya umma usio na mahali salama pa kupitishia kauli zake.
Kukomaa kwa wizi na ufisadi kunazaa njia nyingine za mawasiliano za kupambana nao. Leo ni magazeti, televisheni na redio vinavyotangaza. Kesho huenda redio ikazimwa na televisheni ikawa mikononi mwa fisadi na magazeti kuangamizwa kwa ala.
Umma ulio hai mitaani, hata kama una njaa na kero kabakaba, ndio kimbilio la mwisho kuzomea na kusambaza kisirani kwa wezi wakubwa na mafisadi; kuwakosesha raha na kuwaahidi kimbunga cha mwisho ambapo sunami utakuwa mchezo wa ndimu.
Hakuna ajuaye kwa sasa iwapo vijana waliokamatwa walikuwa wakitukana rais mstaafu au walikuwa kwenmye kindumbwendubwe cha kutumia haki na uhuru wao wa kujieleza kusema kilichoko rohoni mwao. Tunasubiri dimba. Kitaeleweka tu.
(Makala hii itatoka katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 14 Mei 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

1 comment
Best Corporate Video Production Company in Bangalore and top Explainer Video Company, 3d, 2d Animation Video Makers in Chennai
Nice blog
Post a Comment