Serikali inayokimbia wajibu wake
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI serikali ishindwe kuelewa ujumbe wa wafanyakazi wa Mei Mosi kwamba “Ajira Bora, Maisha bora, Uchumi imara na Maendeleo vinawezekana bila ufisadi.”
Huu ni ujumbe wa makusudi kabisa ambao wafanyakazi wameshona kwenye kaulimbiu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni kwamba “Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.”
Katika hili, hatua ya wafanyakazi siyo ndoto. Ni ukweli unaodhihirishwa na yanayotendeka serikalini. Iweje serikali inunue ndege moja kwa Sh. 40 bilioni na kushindwa kulipa mfanyakazi wake mshahara wa Sh. 150,000 kwa mwezi?
Na ndege yenyewe hairuki. Ikiruka haitui viwanja vya ndani ya nchi kwa kuwa vina vumbi na ikipata vumbi inaugua “mafua.” Ni ndege ya madoido katika nchi za wengine.
Ndege yenyewe ni ghali kuhudumia. Ikitumiwa kwenda Zanzibar sharti iruke hadi Madagascar, ndipo irudi kutua Zanzibar, kwani inapokuwa bado haijakaa sawa angani inakuwa imepita Zanzibar kwa masafa marefu sana.
Ni ndege ambayo ununuzi wake uliambatana na kauli za Waziri wa Fedha wakati huo, Basil Mramba kwamba ndege itanunuliwa hata kama wananchi “watakula nyasi.”
Hiyo ni lugha na mazingira ya rushwa kwa wachombezaji hata kama hadi sasa haijagundulika nani alichukua nini.
Iweje serikali ishindwe kulipa mfanyakazi wake lakini ijiingize katika ununuzi wa rada kwa zaidi ya Sh. 70 bilioni, ununuzi ambao baadaye umegundulika ulihusisha mlungula wa mabilioni ya shilingi?
Iweje serikali iruhusu, ishiriki au izembee uchotaji wa kifisadi wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) na ikae kimya hadi inapogunduliwa na wapitanjia, huku mfanyakazi akilia na kusaga meno?
Wanachoshuhudia wafanyakazi ni kusoma takwimu tu: Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., imechota Sh. 38 bilioni; Meremeta imechotewa Sh. 10 bilioni; Tangold imechotewa Sh. 24 bilioni, Richmond na dada yake Dowans wanachotea zaidi ya Sh. 150 milioni kila siku.
Iweje serikali ishindwe kusitisha mikataba ya kinyonyaji ya makampuni ya umeme ya IPTL, Songas, Agreco, Richmond na sasa Tanpower Resources Limited, ili mfanyakazi wake angalau apate mshara unaoweza kumfikisha katikati ya mwezi?
Kama wazalendo walisimama imara, kushamirisha wananchi na kusitisha utawala wa kikoloni, nani anasema leo hii, kwamba haiwezekani kufuta mikataba ya kishetani inayofyonza mabilioni ya shilingi kila siku?
Wafanyakazi wanauliza kipi kizito: kuondoa ukoloni au kusitisha mikataba ya kinyonyaji ya makampuni ya madini ili “watoto wa taifa” hili waweze kuneemeka?
Ujumbe wa wafanyakazi ni mzito. Wanauliza iweje serikali ikae kimya wakati hazina ya nchi inakamuliwa na watu binafsi na makampuni ya kifisadi ambayo serikali inayajua; halafu wao waishi kwa kupiga mihayo?
Mwaka hadi mwaka, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huonyesha fedha zilizotumiwa vibaya, zilizoibwa, zilizopotea au zisizojulikana ziliko. Ni maelfu ya mabilioni ya shilingi.
Mvujo huo wa fedha za umma huwaacha wafanyakazi wakijiuliza vipi serikali inashindwa kudhibiti matumizi lakini inakuwa makini katika kutoongeza mishahara yao na kutoilipa kwa wakati?
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba michango ya wafanyakazi imetumiwa kujenga vitegauchumi vingi na vikubwa vya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo inameremeta kwa wingi wa fedha na ufahari wa miundombinu.
Fedha za mifuko hii hazitoki kuwaondoa wafanyakazi katika dhiki zao. Hata wanapokuwa wanastaafu, bado kuna mshololo mrefu sana wa kupata malipo yao kiasi cha kujuta kwa nini walikuwa katika mpango wa akiba.
Ujumbe wa wafanyakazi unatia moyo. Unaiambia serikali kwamba wafanyakazi wana macho, masikio, akili na hivyo, uwezo wa kufikiri. Wanasema wanajua kinachoendelea.
Ujumbe wa wafanyakazi unaonyesha wameanza kutambua kiini cha wao kupata mishahara kiduchu wakati baadhi ya viongzi wanaogelea katika mabilioni ya shilingi yaliyochotwa kwenye hazina ya umma.
Serikali ina jibu moja ililochonga na kuliweka kabatini. Kila ikiulizwa sawali, basi hulichomoa na kuliweka mezani. Jibu hilo ni, “Serikali haina fedha kwa wakati huu.”
Kila wafanyakazi wanapodai nyongeza ya mshahara, rais, waziri au kiongozi yeyote serikalini huharakisha kuchomoa jibu: “Serikali haina fedha kwa sasa.” Ni jibu lilelile la kizeme ambalo hutumika sana bungeni kila wabunge wanapouliza kwa nini miradi kadhaa haijatekelezwa. Ni jibu la kukimbia wajibu.
Sasa wafanyakazi wameamua kusema wazi: “Ajira Bora, Maisha bora, Uchumi imara na Maendeleo vinawezekana bila ufisadi.”
Ukiangalia mabilioni ya shilingi ambayo imebainika yanachotwa kutoka Hazina na BOT kwenda makampuni ya kifisadi, utaamini kuwa hakika maisha yasingekuwa hivi yalivyo.
Ukiona ripoti ya CAG juu ya hesabu za serikali na fedha ambazo zimetawanyika tu bila maelezo au kwa maelezo finyu lakini yaliyobeba mabilioni ya shilingi, utagundua mengi.
Lakini muhimu zaidi, utagundua kuwa wafanyakazi wa nchi hii wangekuwa na mishahara mizuri kuliko hata wa Botswana ambao mara baada ya kuthibtishwa kazini huruhusiwa moja kwa moja kukopa chombo cha usafiri.
Naafiki kauli ya wafanyakazi ya Mei Mosi. Kwa hiyo serikali ikiendekeza mafisadi itaangamiza wafanyakazi. Lakini ubora uliopo sasa ni kwamba wafanyakazi wameelewa hili na kulitamka bayana. Ujumbe wao umewafikia wengi wenye vilio vya aina hiyo.
Swali moja ni muhimu hapa: Je, wana uwezo wa kusimamia kauli yao ili iwe kitendo? Ikitokea hatutashangaa. Hawatakuwa wa kwanza. Utakuwa mwendelezo unaokubalika.
(Makala hii itachapishwa katika Tanzania daima Jumapili ya tarehe 4 Mei 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments
Post a Comment