Header Ads

LightBlog

SERIKALI INAYODUMU KWA VISINGIZIO

Na Ndimara Tegambwage

Waziri anayedanganya wananchi

SITAKI Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja apotoshe wananchi au awafiche ukweli. Angalau atambue basi kuwa si wote waliopumbazika au wasio na uwezo wa kufikiri.

Ngeleja anasema kupanda kwa gharama ya umeme nchini kunatokana na hatua ya serikali ya kusitisha ruzuku kwenye nishati hiyo kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008 na kuagiza kuwa shirika la umeme (Tanesco) sasa liendeshe.

Tutakwenda hatua kwa hatua. Kwa nini serikali iliamua kuipa ruzuku Tanesco? Ni kwa kuwa iliona gharama ya umeme ilikuwa juu sana kiasi kwamba wananchi wengi wasingemudu kutumia nishati hiyo.

Kwa nini gharama ya umeme imepanda kiasi cha kutisha, kufikia hatua ya serikali kuamua kutoa ruzuku kwa Tanesco ili kukata makali kwa walaji?
Hii ni kutokana na gharama ya uzalishaji umeme kuwa juu.

Kwa nini gharama ya uzalishaji umeme imepanda kiasi cha kufanya watumiaji wake kufikiria kurejea kwenye vibatari? Ni kutokana na serikali kuingia mikataba na “mumiani wa kibiashara” walioamua kufyonza neema yote ya wananchi kwa kulipia umeme peke yake.

Nani alilazimisha serikali kuingia mikataba ya kinyonyaji, kama ule wa IPTL na mingine ya kuzalisha umeme, huku ikijua ni kulifukarisha taifa na kuwafunga wananchi katika utumwa mpya? Ni viongozi wote ikulu na wizarani, waliohusika na ukamilishaji mikataba.

Miongoni mwa washirika wao ni viongozi wa Tanesco, ambao walijua kinachofanyika na athari zake, lakini walilazwa usingizi au walizimwa, kwa njia mbalimbali, ili wasiseme, wasikemee, wasistue taifa bali watulie na kuneemeka wao na waliowapa kazi.

Kwa hali hiyo, waliosuka kitanzi cha gharama ya umeme ni baadhi ya viongozi serikalini. Ukitaka kulielewa hili vizuri, wahusika ni watawala, waliotumia watumishi wao ndani ya serikali na Tanesco.

Kuongezeka kwa gharama ya umeme kulikinzana na kauli na ahadi za watawala za kusambaza nishati hii ili kuliondoa taifa gizani; kuwezesha taifa kuzalisha kwa wingi na kwa njia za kisasa, kufanya maisha kuwa bora na hatimaye kuleta “maendeleo.”

Hapa, maslahi binafsi kwa wote waliokabidhiwa majukumu ya kutawala na kumulikia taifa yalizidi, kwa uzito, maslahi ya umma na ahadi lukuki wakati wa kutafuta ofisi za kisiasa.

Kwa hiyo, uamuzi wa serikali wa kutoa ruzuku kwa Tanesco kwa shabaha ya “kukata makali” ya gharama za umeme kwa mlaji, haukuwa na hauna uhusiano na serikali kuwahurumia wananchi. Hapana!

Huo ulikuwa uamuzi uliotokana na watawala kuona kuwa wameumbuka na wataendelea kuumbuka iwapo hawakuleta chochote cha kupoza, angalau kwa muda tu, makali ya gharama ya umeme kwa mlaji.

Ruzuku ya maana inaweza kutolewa kwa matarajio kwamba juhudi zinazofanywa zitazaa matunda na hali itakuwa nzuri. Ziko wapi juhudi hizo? Kilichopo ni kuendelea kuingia mikataba mipya ya kinyonyaji na kuendelea kumwangamiza mtumiaji wa umeme.

Sasa Waziri Ngeleja anasema Tanesco imekuwa ikipata hasara ya kati ya Sh. 107 bilioni na 189 bilioni kila mwaka tangu 2004 hadi 2007.

Anasema hiyo inatokana na kuuza umeme kwa Sh. 96 kwa yuniti wakati gharama ya kuzalisha na kusambazwa umeme hadi kwa mlaji ni Sh. 164 kwa yuniti moja. Hivyo Tanesco inadaiwa kupata hasara ya Sh. 68 kwa yuniti.

Lakini kinachoitwa hasara ya Tanesco kiliundwa na watawala na Tanesco yenyewe. Ni hawa walioingia mkataba wa IPTL, Songas, Agreco, Richmond na Dowans na TanPower Limited.

Kwa mikataba hii ya kinyonyaji, ambapo mitambo ya makampuni haya, iwe inatoa umeme au imesimama, sharti yalipwe, ndimo Tanesco imekwama kama inzi kwenye mtandao wa buibui.

Ni wazi sasa kwamba Tanesco ina mapato ya Sh. 37 bilioni kila mwezi; lakini malipo kwa makampuni tata ya “kuzalisha umeme” ni Sh. 29 bilioni kila mwezi. Tanesco inabakia na Sh. 8 bilioni tu kila mwezi kwa shughuli zake.

Watawala walioingia mikataba mumiani wanajua unyonyaji huu. Tanesco na wataalam wake wa ufundi na uchumi, wanajua ulafi ulioshonana na biashara ya umeme. Miaka inakuja na kuondoka na hakuna anayebadili mfumo huu unaokamua wananchi.

Mfumo haubadilishwi kwa kuwa miongoni mwa waliopaswa kuubadili au kuufuta kabisa, kuna wanaonufaika na ukwapuaji huu. Na asitokee mtu akadai kuwa hanufaiki au amekashifiwa!

Sasa hatua ya serikali ya kufuta ruzuku, nayo ni ishara ya mchoko; ni ghadhabu tupu – olukana – inayotokana na kugundua kuwa wananchi wameelewa kinachoendelea na watawala “wamekamatwa wakiwa uchi.”

Uchi? Si wachawi, si vichaa. Wameumbuka. Wako tayari kukana sura zao; kila mmoja akisema “siyo mimi,” kumbe ni yeye – yuleyule mfuga nyoka ndani ya chumba cha kulala.

Uwezo wa kuondoa adha ya gharama kubwa za umeme – kuanzia kuunganisha hadi kulipia matumizi – umo mikononi mwa watawala ambao, bahati mbaya, kila kukicha, wanaleta mkataba mpya wa umeme na kampuni ya kinyonyaji.

Hadi hapa Waziri Ngeleja hana budi kujua kuwa umeme siyo ghali. Umeme unafanywa kuwa ghali ili zipatikane fedha za kugharimia miradi ya watoa maamuzi na watia saini kwenye mikataba ya kinyongaji.

Bahati mbaya sana kwa waziri, wananchi tayari wanajua yote haya. Hawakubaliani na kilio chake kinachojaribu kuficha ukweli wa chanzo halisi cha gharama kubwa ya umeme. Ataumbuka.

(Makala hii ilichapishwa katika Tanzania Daima Jumapili ya tarehe 27 Aprili 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.