Header Ads

LightBlog

Polisi wakigoma itakuwaje?

Polisi wanaogomea serikali

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI askari polisi na askari magereza waanze kufanya maandamano na migomo wakidai serikali iwasikilize na kuwalipa mishahara inayolingana na kazi yao. Sitaki!

Hata Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheki ameelezwa kuwa askari nao hawataki kugoma wala kuandamana kama wafanyavyo wafanyakazi wengine wa serikali.

Tatizo hapa ni kama Kagasheki amesikia; na kama amesikia, ameelewa na kama ameelewa, yeye na serikali yake, kama wana nia ya kubadili maisha ya askari polisi na magereza.

Fikiria unaamka asubuhi. Unakutana na msululu wa askari polisi na askari magereza waliobeba mabango. Wanakwenda ama kwa Waziri wa Mambo ya Ndani au Ikulu. Moja ya mabango waliyobeba linasomeka hivi: “Kwa kuwa sisi hatugomi ndio maana hatuongezwi mishahara!”

Kufumba na kufumbua unasoma mabango mengine. Hili linasema, “Tukiamua kugoma nchi itakuwa katika wakati mgumu,” na jingine linasema, “Tukistaafu, kazi pekee ni ukorokoroni.”

Haya ni maandamano, bado mgomo. Je, maandamano haya yameombewa kibali au yametolewa taarifa? Lakini taarifa itolewe wapi wakati wapokea taarifa ndio waandamanaji?

Hawa watu wenye magwanda wameruhusiwa na nani kuingia mitaani? Je, nani analinda waandamanaji? Au mara hii raia wanalinda maandamano ya askari? Hapo ndipo utashangaa. Unaweza kudhani unaota. Nani atamkamata nani na nani atamfunga yupi – polisi na magereza!

Lakini hakuna la kushangaa. Tayari maandamano yameanza. Yameanzia mjini Bukoba. Askari polisi na askari magereza walimwambia Naibu Waziri Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheni mapema wiki hii kwamba serikali inapaswa kuboresha mishahara yao.

Mishahara ndiyo inaamua kiasi cha maslahi pale mfanyakazi anapostaafu. Sasa wanasema kutokana na maslahi kiduchu, wanalazimika kufanya kazi za korokoroni “kwenye maduka ya Wahindi,” mara baada ya kustaafu ili kulea familia zao.

Msemaji wa askari hao (tofauti kabisa na Msemaji wa Polisi), alimwambia waziri umuhimu wa serikali kuongeza mishahara yao bila kusubiri migomo kama wafanyakazi wengine.

Ili kuongeza uzito kwenye maelezo yao, msemaji wao aliongeza kuwa askari anafanya kazi kati ya siku 320 na 350 kila mwaka wakati wafanyakazi wengine wanafanya kazi kwa siku 196 (Mwaka moja una siku 365)!

Askari wanalalamika: Hawana nyumba. Hawana mishahara ya maana. Magereza wanatumia gari lililonunuliwa mwaka 1978. Kwa usafiri wako ulimwengu wa 10. Yote hayo yanamwagwa kwenye kikao na naibu waziri alipoamua kusikiliza kero za “usalama wa raia.”

Usalama wa raia utatoka wapi katika mazingira haya? Asiye salama atalindaje maisha ya raia? Kwa udhaifu huu, asiye salama atalindaje mwajiri wake na wabia wake wa ndani na nje?

Asiye na mahali pa kuishi au anayeishi katika kibanda cha ovyo, huku akichekwa na wananchi, kama askari alivyomweleza waziri, atalindaje maisha ya watu, serikali na mali zao?

Lakini hapa kuna mambo muhimu ya kuzingatia. Askari polisi au magereza amevaa sare ya dola – shati na suruali au blausi na sketi. Amevaa kofia yenye nembo ya mwajiri. Amevaa mkanda wenye rangi za taifa. Ni “chombo cha dola” kwa maana zote.

Huyu ndiye askari anayechekwa. Anayezomewa kwa kuwa katika hali mbaya ya maisha. Ndiye anasubiriwa kustaafu ili aanze kazi mpya ya kumlinda mfanyabiashara kwa kuwa hana njia nyingine yoyote ya kuziba pengo pale ambapo mshahara kiduchu uliacha makorongo.

Ni askari huyu anayepaswa kukimbiza wezi waliopora fedha, mikufu, shanga, saa na mali nyingine za raia. Ndiye huyuhuyu anayepaswa kulinda ofisi za serikali hadi ikulu. Ni huyuhuyu anayepaswa kupeleleza wizi wa kawaida na ufisadi uliofanywa na watumishi serikalini. Ataweza?

Mtu aweza kubisha kwamba polisi wa upelelezi wa mambo makubwa wanalipwa mishahara mizuri na wanaishi katika mazingira ya nafuu. Lakini nani asiyejua kwamba polisi wadogo ndio wako karibu sana na vyanzo vya taarifa kuliko walioko ghorofani?

Kuna wakati niliandika juu ya polisi wa laini ya Temeke, jijini Dar es Salaam; jinsi walivyokuwa wakipita madirishani kuingia ndani ya nyumba zao za vigae zinazovuja.

Nakumbuka kuandika juu ya polisi waliokuwa wakiishi katika mabanda yaliyojengwa kwa suti ya mabati matupu. Wakati wote ni jahanamu: Joto likija wanaungua na baridi ikija wanatetemeka kama vifaranga vya kuku.

Niliwahi kuandika juu ya askari walioishi katika mabanda yasiyo na vyumba kiasi kwamba pazia ndiyo ilitenganisha familia moja na nyingine. Nakumbuka sana.

Hili la Bukoba limenikumbusha yote hayo na nina uhakika kwamba Kagasheki atakuwa amepigwa na butwaa. Kama alikuwa anajua hali hiyo tangu zamani, basi alikwenda kukidhi haja ya matembezi ya waziri na kupata angalizo la baadaye kwa rais wake.

Waziri amenukuliwa akisema anasikitishwa na hali wanayokabiliana nayo na kwamba atawasilisha kero zao mahali panapohusika.

Hivi ni wapi huko panapohusika ambako wahusika hawahusiki kwa miaka 47? Na askari polisi na magereza hawawezi kugoma wala kuandamana. Ni “watoto wa nyumbani” kwa mzee.

Walie lita ngapi za machozi; wapige mayowe yaendayo umbali gani au wanyamaze kimya cha mauti na kunyanyasika ndipo waonwe na malaika wa huruma.

Na je, wanastahili huruma au haki yao? Kagasheki ataweza kusimamia hili? Wewe, mimi na askari, tunasubiri kuona mabadiliko.

(Makala hii itachapishwa katika toleo la 11 Mei 2008 la gazeti la Tanzania Daima Jumapili. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.