Header Ads

LightBlog

UHURU WA KUJIELEZA

Uandishi silaha dhidi ya ufisadi

JUMAMOSI iliyopita, 3 Mei 2008 Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-Tan), ikishirikiana na IPP Media, UNESCO, na Ofisi ya Habari ya Umoja wa Mataifa (UN) iliandaa kongamano la wadau katika hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam, kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Mshauri wa mambo ya habari nchini, NDIMARA TEGAMBWAGE, alitoa salaam zifuatazo ambazo zimetafsiriwa kutoka Kiingereza.

*************************************

SIKU ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani hutupa fursa nyingine ya kurejea na kuthibitisha msimamo wetu kuhusu Uhuru wa Kuwa na Maoni.

Uhuru wa kuwa na maoni una maana pana kwetu sote tulioko hapa na kwa binadamu kwa ujumla. Uhuru wa maoni una maana ya uhuru wa kufikiri na kuzalisha mawazo na maoni. Uhuru wa kusema kilichoko moyoni. Uhuru wa kukusanya/kutafuta habari/taarifa. Uhuru wa kugawana habari hizo na mtu/watu wengine. Uhuru wa kuwa na mawazo/maoni tofauti na mtu mwingine au hata utawala.

Lakini ili uhuru wa kuwa na kutoa maoni uwe kamili na ufurahiwe kikamilifu, sharti maoni hayo, mawazo hayo yatamkwe; yawe hadharani; yachapishwe katika magazeti na kutangazwa katika redio na, au televisheni. Hii ina maana kuwa maoni ambayo hayajawasilishwa kwa njia yoyote ile: kutamkwa, kuchapishwa au kutangazwa, yanabaki utumwani kama aliyo yule aliyeyatoa. Kwa hiyo, leo ni siku ya kuahidi tena kuendeleza msimamo wetu wa kukuza uhuru wa kuwa na maoni na kuulinda.

Hata hivyo, tukio la leo linakuja wakati muwafaka katika historia ya Tanzania. Ni wakati kuna ufunuo kwamba mfanyabiashara na ofisa wa serikali wako bega kwa bega katika “dansa la rushwa.”

Tukio la leo linakuja wakati taifa limezama katika mshangao kutokana na uporaji uliopindukia wa mabilioni ya shilingi kutoka hazina ya umma kwa ajili ya kukidhi matakwa na ulafi wa watu binafsi. Tukio linakuja wakati wale waliopo kwenye ngazi za juu za utawala wanatuhumiwa, na wengine wamethibitika kuwa wabunifu wakuu na wazoefu wa mikondo ya kugushi na wizi ambao umekomba hazina ya umma.

Kwa hiyo, tukio la leo linakuja wakati kuna mijadala mikali na ubishi juu ya kipi kifanyike kurejesha fedha za umma katika hazina; kurejesha fedha zilizokwapuliwa kutoka katika mabenki na nyingine kupitia makampuni bandia na mikataba ya kishetani.

Hakika, huu ni wakati ambapo taarifa zimetamalaki kutoka sehemu mbalimbali, zikieleza nani ameiba nini, lini, wapi na kwa ushirikiano na nani; na nani “alizikwa” (hakupewa mgawo wake) katika kukatiana maelfu ya mabilioni ya shilingi ambazo kwa wingi wake, zingefanya serikali iache ombaomba nchi za nje.

Ni wakati ambapo hata sauti za mabubu zinasikika kwenye vilele vya milima; wakati kila mwenye taarifa ana kitu cha kuchangia katika zogo hili, wakati raia nwanadai majibu kwa maswali ambayo yalikuwa hayajawahi kuulizwa hapo awali na wanataka serikali ichukue hatua.

Bahati nzuri, huu ni wakati ambapo vyombo vingi vya habari vimeamua kutopepeza kope ili visije vikapoteza mkondo wa matukio na taarifa za kashfa zisizomithilika kutokana na rushwa kubwa ambazo zimeacha uchumi wa nchi ukivuja kwa kiwango cha kutisha.

Nikiwa mwalimu katika nyanja ya kupambana na rushwa, ninajua kwamba ili kukabiliana na rushwa, sharti rushwa ianikwe kwa kutoa taarifa muhimu na njia nyingine za uwezeshaji kwa wananchi. Hii ina maana kwamba, taarifa zinazotolewa sharti ziwe pana na kamilifu; na zihusu maisha ya umma. Taarifa kama hizo, siyo tu zinaibua mijadala na kuchukuliwa kwa hatua, bali pia zinatoa elimu ya kudumu juu ya rushwa na njia za kupambana nayo.

Ni wajibu wa vyombo vya habari vilivyo makini, kuwapa raia taarifa na takwimu zisizo na shaka za kuwawezesha kupanua upeo na kuimarisha uelewa wao juu ya rushwa na jinsi ya kuikabili. Aidha, ni vyombo vya habari ambavyo, bila huruma, vinaweza kuanika ushirika wa watawala katika rushwa, uzembe au, na hata udhaifu wao katika kukabiliana na rushwa, hadi kuwatoa usingizini.

Kwa kuzingatia mazingira ya sasa nchini, hasa “uchafu” unaotokana na matumizi ya ovyo ya maelfu ya mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa kiwepesi kutoka hazina ya umma; aina hii ya rushwa inayofukarisha haraka taifa na watu wake; rushwa inayodhoofisha serikali na kugeuka kuwa chanzo kikubwa cha migogoro, Mei 3 ya mwaka huu sharti ituache na ahadi ya kuifanya Tanzania kuwa “Taifa linaloongea.”

Taifa linaloongea ni taifa lenye taarifa. Linajua kinachotendeka na kwa nini. Linajua kitu gani kunaunganisha wafanyabiashara na maofisa au watawala na nani anasaidia kusimika miliki ya rushwa na ufisadi. Bali kwa taifa, tuseme wananchi wake kuendelea kuongea, sharti viwepo vyombo halisi na huru ambamo watatekelezea na kufurahia uhuru wa kuwa na maoni.

Rushwa na hasa rushwa kubwa, haiwezi kudumu iwapo umma utakuwa umeeleweshwa aina na viwango na matumizi mabaya ya madaraka. Hapa, vyombo vya habari vinaweza kukubali, kwa uaminifu kabisa, kuwa njia ambamo raia wanaweza kupitia ili kuwasiliana na uongozi wa nchi; kuingiza mawazo mapya katika jamii, kuwasilisha matakwa na madai yao na hatimaye kuwezesha kufikiwa kwa mabadiliko bora.

Hata hivyo, ni bahati mbaya kwamba Siku ya Uhuru wa Maoni Duniani mwaka huu imekuta baadhi ya vyombo vya habari vimegawanyika. Sehemu moja inatafuta kwa dhati kuanika rushwa na ufisadi wakati sehemu nyingine inatoa udenda ikitafuta kusaidia wale ambao wamebainika kuwa wakwapuanji wakubwa wa fedha za umma. Hii ni hali mbaya na ya kusikitisha.

Kana kwamba hiyo haitoshi, uhuni wa kisiasa nao umeota mizizi; unatumika kushambulia, kutoka sehemu zote, wahariri na wafanyakazi wa vyombo vya habari ambavyo ni makini – kwa kauli za vitisho, kutishia au kufungua mashitaka mahakamani, kuunda vikundi vya kihuni na vya kupiga na kujeruhi watendaji, na kutoa maelekezo jinsi vyombo vya habari vinapasa kufanya kazi zake.

Pamoja na yote hayo, hakuna kulegea wala kukata tamaa; angalau huo ndio ujumbe ambao tayari umepelekwa kwa walimwengu.

Tunavyoahidi kubaki imara katika kutetea uhuru wa maoni kwa manufaa ya taifa na raia wote wa dunia, basi na tuahidi pia kuunga mkono, kwa kauli na vitendo, wale wote walioapa kuanika rushwa na ufisadi kwa gharama yoyote ile.

Mwisho

No comments

Powered by Blogger.