Header Ads

LightBlog

YESU ANAPOPANGIWA TAREHE YA KURUDI

SITAKI

Na Ndimara Tegambwage


Mahubiri yanayoua akili


SITAKI kuamini kwamba Yesu Kristo, hata kama “atarudi” duniani, atapitia Kyela, mkoani Mbeya na katika vichaka vilivyoko katikati ya vijiji vya Tenende na Lukuju ambako baadhi ya waumini wanamsubiria.

Kwa wiki nzima sasa baadhi ya waumini wamekuwa wakiishi katika vichaka mkoani Mbeya wakimsubiri Yesu Kristo ambaye wameambizana kuwa “atarudi” kati ya 28 na 30 Machi mwaka huu.

Hiyo ndiyo “neema” ya kuwa na uhuru wa kuamini na kuabudu. Wasabato wachache mkoani Mbeya, wakichochewa na mwenzao kutoka mkoani Mara, wameamua kuamini zaidi ya imani ya pamoja ya waumini wenzao.

Wameamua kuandika kalenda ya ujio mpya wa Yesu Kristo na kuitangaza. Kuna tatizo dogo hapa. Hawakutangazia dunia nzima iende Kyela kumpokea “Bwana.” Hapana. Ni wao tu, katika uchache wao.

Wasabato wa Kyela hawakuweza kutangazia dunia ujio huu mpya. Labda hawakuwa na uwezo wa kusambaza habari kwa njia za kisasa za kutawanya habari haraka.

Bali pia inawezekana waliamua kuwahi. Misemo ya vijana ni “Ujanja kuwahi!” Inawezekana pia kwamba walikuwa wana mategemeo tofauti. Labda Yesu angekuja na vifurushi na waliopo ndio wangenufaika.

Ni mithili ya Parapanda? Waliosikia sauti ndio wameitikia?Wamechomoka kutoka miongoni mwa wengi? Hapana.

Tofauti na Parapanda ni kwamba hawa wa Kyela wameitana. Hawakuchomolewa mmoja mmoja, kila mmoja kwa nafasi yake mbele ya anayemuita. Hawa wa Kyela wamekutana, wakajadili, wakachocheana, wakaamua kujiita, wakaamua kujiitika na kujipeleka Tenende la Lukuju.

Tofauti na wale wasemwao kuitikia Parapanda, waumini wa Kyela wanaosema Yesu Kristo lazima arejee mwezi huu, wamebeba baadhi ya mali zao. Wamebeba baisikeli, vitanda, magodoro na vifaa vingine vinavyobebeka.

Je, Wasabato hawa wamechoka kusubiri? Wamesoma Biblia mpaka zikachanika: Yesu harudi. Baadhi wameomba utajiri wa mali, wameambulia umasikini. Wamesubiri hukumu kwa wawatendeao mabaya; wameona wabaya wanaendelea kuneemeka.

Wameamua kupanga mahali na tarehe ambako lazima Yesu Kristo atashukia; kuja kuwachukua walio wake.

Je, yawezekana Wasabato hawa hawapati mahubiri sahihi juu ya kuja kwa Yesu Kristo kwamba “hakuna ajuaye siku wala saa?” Au yawezekana hilo haliwaingii akilini hasa katika mazingira ya sasa ya teknolojia ya hali ya juu?

Kwa teknolojia ya sasa na uwezo wa Mungu, ndipo Wasabato wa Kyela wakaamua kuamini kuwa mbinguni hakuna vitanda, baisikeli, magodoro wala nguo. Sharti waende na vifaa hivyo muhimu, kwani Yesu “anarudi kuwachukua” na pakacha lake lazima liwe na uwezo wa kubeba vitu vingi.

Hata kama hawaendi kuvitumia; au hata kama baadaye wataambiwa na Yesu kwamba havihitajiki, angalau Bwana avione na atambue kwamba walijitahidi kuwa na mali ya kiwango hicho; kiwango chao.

Tajiri atakwenda na utajiri wake na masikini atakwenda na umasikini wake. Ni mtindo wa kwenda foleni, kila mmoja akionyesha alichovuna.

Mwadilifu na uadilifu wake; fisadi na ufisadi wake. Mtawala na mabavu yake; mtawaliwa na unyonge wake. Mnyenyekevu na udhaifu wake; mwasi na harakati zake za kujikomboa.

Bali kuna tatizo moja linalojitokeza katika uhuru wa imani na kuabudu. Viongozi wa madhebu wameshikilia sana na wamewapulizia waumini ndoto nyingi za “maisha baada ya kifo.”

Kule kutenga maisha ya duniani; yale yanayoshikika; yanayoeleweka kwa kila mmoja na yale ya baada ya kifo, ndiko mgogoro wa imani unapoanzia.

Ndilo chimbuko la unafiki uliokithiri wa “tenda ninavyokwambia na siyo ninavyotenda.” Ndio mwanzo wa uzandiki wa kuombea wahuni na mafisadi ili waendelee kutawala.

Mahubiri yanayowashirikisha waumini katika kutukuza waovu walioko majumba ya sala na katika utawala, ndiyo chimbuko la hasira ya baadaye hadi hatua ya baadhi ya waumini kupanga siku ya kurudi kwa Mwana wa Mungu na mahali atakapofikia.

Labda wakati umefika kwa wahubiri wa madhebu yote duniani, kuoanisha imani na hali halisi ya waumini katika mazingira yao.

Kinachohitajika sasa ni kutoa mahubiri, fafanuzi za maandiko matakatifu, katika lugha ya vitendo. Hii ni lugha shirikishi ambamo waumini wanaelekezwa jinsi ya kupambana na udhalimu unaowakabili.

Kuhubiri ahadi ya kwenda mbinguni kumepitwa na wakati. Mbingu yetu ni hii hapa tulipo na kila mmoja anapaswa kuishi kama anavyotarajiwa na jamii yake – kwa uadilifu na hata kwa harakati za kuangamiza walafi ambao wamefanya maisha ya wengi yawe mafupi zaidi.

Hatutegemei makanisa na misikiti kuhubiri jinsi ya kuishi baada ya kifo; bali jinsi ya kuwa askari mpigania haki katika mazingira ya sasa ambayo ndiyo maisha tuliyo na uwezo wa kuyatawala na kuyaelekeza.

Mahubiri ya kukimbilia mbinguni, kila mmoja na godoro lake, bakuli lake na mswaki wake, ni kasumba inayoteteresha akili. Hayatufai Kyela na hata popote duniani.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 23 Machi 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

1 comment

Anonymous said...

Hello. This post is likeable, and your blog is very interesting, congratulations :-). I will add in my blogroll =). If possible gives a last there on my blog, it is about the Notebook, I hope you enjoy. The address is http://notebooks-brasil.blogspot.com. A hug.

Powered by Blogger.