Header Ads

LightBlog

Polisi, vitisho na Bi. Stella wa Msewe


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI polisi wa Tanzania wasahau kwamba ni kwa matendo yao, au kwa kutotenda kwao, wanaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Na hivyo ndivyo itakavyokuwa. Hili likitokea, ile dhana ya “Polisi ni usalama wa raia” itakuwa imetoweka. Hakuna atakayewaheshimu kama ambavyo hakuna atakayeweza kurejesha imani ya wananchi kwa polisi.

Ni wiki ya pili sasa, tangu mwanamke mmoja wa kijiji cha Msewe, Ubungo, jijini Dar es Salaam ahame nyumba yake kwa woga wa kushambuliwa na hata kuuawa.

Ni Stella Kajuna. Mfupi, mwembamba, hajai kwenye kiganja; lakini ni mama mmoja jasiri aliyetoa tuhuma dhidi ya mwanaume anayedaiwa kufanya ngono na wanafunzi wa kike katika kijiji cha Msewe na jijini Dar es Salaam.

Stella anataja jina la kijana wa kiume anayehusika. Anataja majina ya wazazi wake. Anataja jina la mwanafunzi muhusika. Anataja jina la mwanafunzi mwingine; na mwingine.

Stella anataja majina ya wazee kijijini ambao wamebughudhiwa na mtuhumiwa. Ana ujasiri wa kweli. Ni mwanamke.

Lakini tangu alipotoa hadharani jina la mtuhumiwa, badala ya polisi kufuatilia mtuhumiwa wa uhalifu, wamekuwa wakimfuatilia Stella.

Kama hiyo haitoshi, mama wa mtuhumiwa anadaiwa kufungua mashitaka kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu kwamba Stella ametishia kumuua.

Licha ya tuhuma za “kuharibu wanafunzi wa kike,” kijijini Msewe, kuna madai ya ujambazi unaofanywa na kufumbiwa macho na utawala wa kijiji. Kuna madai pia ya polisi wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu kushirikiana na watuhumiwa.

Je, baada ya Chato (Biharamulo) na Singida, ambako wananchi wamejichukulia hatua ya kuvamia vituo vya polisi wakivituhumu kutotenda kazi zake, Mbezi kwa Yusufu imesalia wapi?

Ni kwa kuwa Mbezi kwa Yusufu ni Dar es Salaam? Kwa kuwa kituo kipo karibu na ikulu? Kwa kuwa ni langoni kwa Inspekta Jenerali ya Polisi (IJP), Said Mwema? Kwa kuwa watawala hawa hawasikii au wanawalinda wadogo zao Mbezi?

Watawala wamekuwa wakitaka wananchi watoe ushahidi kuhusiana na tuhuma wanazotoa. Polisi nao wamekuwa wakihimiza wananchi kutoa ushirikiano katika kukabili uhalifu na kutoa taarifa za kuwawezesha kufuatilia.

Ingawa ukweli ni kwamba ushahidi sharti utolewe mahakamani, lakini Stella ametoboa kila kitu alichonacho: nini kimefanyika, nani amefanya, nani kafanyiwa, wapi watuhumiwa wanaishi, mazingira ya Msewe kijijini na mengi mengine.

Lo! Zawadi ya Stella kwa kutoa taarifa za kufichua uhalifu, imekuwa kusakamwa kwa vitisho, kutungiwa tuhuma za kutaka kuua na kunyemelewa kama mhalifu.

Stella angekuwa na uwezo wa kutamka neno “kuua,” hakika asingetoa taarifa za uhalifu; angekuwa ametishia au ameua mapema. Kilio cha Stella ni haki kwa watoto wake na jamii. Inaonekana bado ana imani na utawala.

Sasa Stella, kila kukicha, ni kiguu njia. Yuko kwa Kamanda wa Polisi Kinondoni; yuko Ofisi ya Makamu wa Rais; kwa Katibu Mkuu Wizara ya Usalama wa Raia; kwa Mpelelezi Mkuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambako anasema alihojiwa kwa saa tano.

Stella anatuhumu kijana wa kiume kubaka wanafunzi. Anatuhumu polisi kutomtendea haki na kutotenda. Yote yanachunguzika. Vitisho kwa mama huyu vinatoka wapi?

Stella ana kila sababu ya kuwa na woga. Vijana Hija Shaha Saleh na Mine Chomba wako wapi? Wanasadikiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Wako wapi wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathias Lukombe wa Mahenge, mkoani Morogoro; na dereva wao Juma Ndungu. Inadaiwa maisha yao yalisitishwa wakiwa mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam.

Katika hili la Stella, na jinsi ambavyo amesumbuliwa, sharti Rais, Waziri Bakari Mwapachu, IGP, Watanzania wote na dunia nzima, wajue kwamba hapa hakuna utawala bora.

Kwa nini polisi na serikali wasubiri wananchi wa Msewe na viunga vya Dar es Salaam, kumrejesha Stella nyumbani kwake kwa maandamano, huku wakipita kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu na kuwavuta mashavu polisi?

Hilo likitendeka, wakuu wa polisi watalalamika kwamba wananchi wamejichukulia sheria mkononi. Lakini wamsubiri nani, kama wa mwisho aliyetegemewa, ama amekuwa mshiriki wa watuhumiwa au amelala fofofo.

Stella hana uhuru tena. Lakini kurejea kwa uhuru wake kwaweza kuepusha janga na aibu kwa utawala, polisi na taifa. Na bado polisi wanaweza kumaliza hili kwa sekunde tu. IGP Mwema unasemaje? (Picha: Said Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi).

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 28 Oktoba 2007). Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0713 614872; na imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.