Header Ads

LightBlog

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI



SITAKI Na Ndimara Tegambwage
(Kuchapishwa Tanzania Daima 7 Oktoba 2007)

Waziri anapokemea mabalozi

SITAKI mabalozi wa nchi za nje walioko Tanzania wamshangae Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kwa kuwakemea.

Ni Ijumaa iliyopita, jijini Dar es Salaam, Membe alikemea Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Ubelgiji (kwa niaba ya mataifa ya Ulaya), kwa kile kilichoitwa “kujadili siasa” za Tanzania.

Nchi hizo ndizo zilizokuwa zimejitokeza hadharani hivi karibuni, kutaka serikali ichunguze, bila kujenga chuki, tuhuma zote zilizotolewa na kambi ya upinzani kuhusiana na rushwa miongoni mwa viongozi wa siasa na taasisi kuu za fedha.

Mabalozi walimsikiliza waziri akiwakemea; akiwaambia wakae kimya au wafuate “misingi ya itifaki.” Ni nchi hizi ambazo zimeshiriki kujenga jeuri ya watawala na Membe anawageuzia kibao.

Tuliwahi kuziambia baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, wakati tukipigania kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi (1985 – 2002). Tuliziambia kwa Kiingereza kwamba, “You are fueling the machinery of oppression.”

Kwamba “Mnakoleza mitambo inayoendesha ukandamizaji nchini.” Nchi chache ambazo ni Uholanzi, Sweden, Denmark na Norway zilielewa ujumbe wetu na kusaidia mkutano wa kwanza wa mageuzi jijini Dar es Salaam (11 – 12 Juni 1991).

Wengine walikuwa wakiona kinachoendelea; wakisikia kauli za ukaidi wa serikali na kilio cha wanaotaka mabadiliko; lakini walichagua moja: Kugonganisha bilauri za mvinyo na shampeni na maofisa wa serikali.

Na mitambo ya ukandamizaji iliendelea kulainishwa; iliendelea kukoboa na kusaga uhuru na haki za wananchi, kwa kuwanyima hata fursa za kushiriki katika siasa za nchi yao.

Hiyo ni miaka 20 iliyopita. Leo, mambo yamekuwa tofauti. Mabalozi wamesoma mwenendo na kusema, kwa njia ya ushauri, kwamba serikali ijibu tuhuma za rushwa na ufisadi.

Mabalozi ni watu waliofungwa na taratibu na kanuni za kutoa kauli. Membe anawakumbusha, ama waandikie serikali au wafanye vikao na serikali. Lakini wasitoe kauli moja kwa moja kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Lakini ubalozi siyo tu kunywa mvinyo na shampeni. Siyo tu kukinga meno na kupigiana makofi kinafiki. Siyo kukinga serikali ambamo balozi anawakilisha nchi yake. Hapana.

Ubalozi hauondoi uhuru na haki ya balozi ya kuwa na maoni binafsi. Kwa kuwa mabalozi ni watu, wana uhuru na haki ya kutoa maoni juu ya jambo lolote lile; ndani ya nchi zao, ndani ya nchi waliko na nje ya nchi hizo.

Na kauli ya balozi haiwi na shuruti hadi pale inapopewa kiambishi. Ni kweli, ina uzito kwa kuwa ni maoni ya mtu wa nje na mwakilishi wa taifa la nje; lakini haina shuruti.

Kwamba serikali inaweza kuogopa kauli za mabalozi, zilizotolewa katika nafsi zao na bila kusindikizwa na angalizo, shinikizo au amri ya nchi husika, ni ushahidi tosha kwamba kuna kiwewe.

Membe anapata wapi ujasiri wa kunyamzisha mabalozi? Hoja kwamba kauli binafsi za mabalozi ni uchochezi wa kisiasa zinatoka wapi?

Mabalozi wana maslahi katika maendeleo ya nchi hii. Nchi zao zinamwaga mabilioni ya shilingi kila mwaka katika kile watawala wanaita “ushirika kimaendeleo.”

Mwaka huu peke yake, zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali inatarajiwa kutoka nchi za nje. Hizi ni fedha zinazotokana na kodi za wananchi katika nchi wanakotoka mabalozi.

Sehemu kubwa ya fedha hizo ndizo zinaliwa kama njugu mitaani. Mikopo na misaada ndiyo inatajwa kununulia magari na kujengea nyumba za kuishi za kifahari.

Kwa hiyo, kama washirika kimaendeleo, mabalozi wakiwakilisha walipa kodi na serikali zao huko watokako, hawawezi kukosa la kuchangia katika mjadala wa wazi na mpana kuhusu rushwa na ufisadi.

Kuwakemea mabalozi na kutaka wakae kimya au wawasiliane na serikali kwa mikutano na maelezo kwenye kabrasha tu, ni ishara ya kukosa uvumilivu. Lakini zaidi, ni ishara ya kukosa majibu.

Busara inaonyesha kwamba kitu cha kujadili kwa njia ya mikutano ya ndani na kabrasha ni misimamo maalum kati ya serikali mbili, juu ya kuimarisha uhusiano, kuongeza misaada au hata kusitisha misaada.

Lakini hata hayo yaweza pia kujadiliwa, tena hadharani. Inafikia mahali, serikali husika zinakuwa kero kwa wananchi wake na wale wanaowasidia; zinajaa rushwa na ufisadi na kufanya watoa misaada kukosa uvumilivu. Hapo hulazimika kupasua jipu.

Lakini mabalozi walioko Tanzania wameitaka serikali isipuuze tuhuma walizobebeshwa baadhi ya viongozi kuhusiana na ufujaji wa fedha na maliasili za nchi. Ni ushauri mwanana.

Sasa kuwataka mabalozi wafunge midomo juu ya kinacheondelea nchini, ni funzo kwa mabalozi hao na nchi zao.

Mabalozi na nchi zao waelewe basi, kilio cha wananchi cha uhuru na haki za msingi nchini.
Wasilalamike. Wajifunze. Wachukue hatua.
Mwandishi wa makala hii
anapatikana kwa simu:
0713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com na webu: http://www.ndimara.blogspot.com/

No comments

Powered by Blogger.