Header Ads

LightBlog

MJADALA JUU YA RUSHWA NA UFISADI


SITAKI

Rais anayebeba wasiobebeka

SITAKI Rais Jakaya Kikwete apinde hoja. Sitaki rais awe moto na wakati huohuo awe baridi. Hii ni kwa kuwa sitaki wale ambao rais anatawala, wamuone kuwa ni mwongo au mkosefu wa uadilifu.

Hoja iliyoko mezani ni moja: Orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhujumu uchumi wa nchi kwa kutenda, kutotenda au kunyamazia vitendo vya uhujumu.
Kilio cha waliotoa orodha hiyo ni kwamba waliotajwa wachunguzwe na watakaobainika ionekane wazi kwamba wanachukuliwa hatua.

Hicho ndicho kilio cha wananchi wengi; wale ambao wanashuhudia fedha na utajiri mkubwa wa nchi vikifujwa na wachache na kwa njia ya ufisadi, huku viongozi wao wakiongeza tabasamu.

Hayo ndiyo matakwa ya mabalozi wa nchi za nje, waliotoa maoni yao binafsi kuhusu madai ya ufisadi na kuhitimisha kuwa nao wangependa kuona serikali ikijibu tuhuma kwa njia mbili:

Kwanza, ikijibu tuhuma zinazowakabili viongozi wake mmojammoja na serikali kwa ujumla; na pili, ikichunguza na kuchukua hatua.

Hayo ndiyo matakwa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwamba pamoja na dalili za kile kinachoitwa kukua kwa uchumi, kuna haja ya kujibu tuhuma za ufisadi na kuchukua hatua za kuzuia momonyoko.

Katika kauli zake wiki iliyopita mjini Arusha, badala ya kujibu hoja iliyoko mezani, Rais Kikwete alijipa kazi ya kuandama aliowaita “watu wengine.”

Alitumia muda mwingi kukandia wale aliosema wanafanya kazi ya kutuhumu, kukamata, kushitaki na kuhukumu watuhumiwa. Alisema taifa litawekwa pabaya iwapo litadumu kwenye kutuhumiana.

Kauli ya Rais Kikwete inaweza kutafsiriwa kama ifuatavyo: Kwamba hajaketi na kuelezwa yaliyotokea akiwa nje ya nchi. Hajasoma hata taarifa za magazeti na wataalam wake wa mawasiliano hawajapata muda wa kumpa taarifa.

Kwamba rais hajaambiwa kuwa hata yeye ni miongoni mwa waliotuhumiwa; na kwa msingi huo alistahili kujibu sehemu inayomhusu.

Kwamba rais hajakaa na watuhumiwa wengine kutafuta jinsi ya kujibu kwa pamoja au kutafuta msimamo wa pamoja, wa kina na unaoweza kutosheleza matakwa ya taarifa kamili ya serikali inayojali na adilifu.

Kwa ufupi, rais hajajibu hoja kuu ambayo ni tuhuma za ufisadi. Kwa maana hiyo rais amepuuza tuhuma za ufisadi dhidi yake na mawaziri wake.

Kinachoeleweka kutokana na kauli zake, ni kwamba ameamua kuzika hoja muhimu, na kwenye nafasi yake, kuingiza shutuma kwa vyama vya upinzani na viongozi wao ambao ni chanzo cha tuhuma za ufisadi.

Lakini ni Kikwete yuleyule ambaye amenukuliwa akiiambia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake kuwa waziri yeyote atakayesaini mkataba wa madini nje ya makubaliano ambayo yamefikiwa kati ya serikali na kampuni za madini nchini, atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Huko ndiko kuwa moto na baridi kwa wakati mmoja. Rais hajibu tuhuma dhidi yake. Rais hajibu tuhuma za wateule wake. Rais anakandia wapinzani kwa kuwa polisi na hakimu.
Rais anasema waziri wake atakuwa amejifukuzisha kazi. Rais anasema atachunguza na yule ambaye tuhuma dhidi yake zitathibitika, atachukuliwa hatua.

Rais anataka wananchi na “wapinzani” wapeleke ushahidi, kwake au polisi, wa tuhuma zao dhidi ya yeyote ili serikali itumie ushahidi huo kuchunguza!

Hizi zote ni njia za kukimbia hoja kuu. Rais anapofikia hatua ya “kumbakumba;” kukusanya sababu dhaifu hapa na pale ili kulinda wateule wake na serikali yake, ujue kuna mkwamo.

Wote ambao wamekuwa wakifuatilia sakata la tuhuma za ufisadi tangu Dk. Willibrod Slaa asome orodha ya watuhumiwa hadharani, mwezi mmoja uliopita, walitarajia Rais Kikwete kuja na kauli tofauti na hii aliyotoa.

Walisubiri aseme uhujumu wa uchumi ni kitu kibaya sana. Kwamba wananchi wamefanya vizuri kutoa hadharani majina ya wale wanaotuhumiwa. Kwamba tume huru ya wajumbe kutoka asasi za kijamii na watu wanaoaminika kuwa na rekodi safi katika jamii, inaundwa na kuaza mara moja kufanya uchunguzi.

Nchi nzima walitarajia rais aseme anajua kuwa uchunguzi huanzia kwenye mashaka. Mashaka hutokana na tabia, mwenendo na hata mwonekano wa hali halisi wa mambo yanayopingana na kauli, ahadi, kanuni, taratibu na sheria zinazotawala.

Kwa msingi huo, akitokea mtu au kundi la watu, wakawa na mashaka; wakachimba na kuonyesha kiini cha mashaka; hiyo inatosha kupiga kelele ili vyombo vilivyosomea kazi ya upelelezi viweze kufanya kazi.

Wananchi na jumuia ya kimataifa walitarajia rais awe anajua hilo; na hasa awe anajua kwamba ushahidi hautoki kwa “wapiga filimbi,” bali hutokana na uchunguzi ambao ndio wote wanataka ufanyike.

Kudai ushahidi kutoka kwa wananchi maana yake ni kukataa kuchunguza tuhuma za ufisadi; ni kuweka jembe la kukokotwa mbele ya maksai badala ya kuliweka nyuma ili alikokote na kulima.

Na hii siyo kwa bahati mbaya. Ni makusudi. Ofisa mmoja alipotaka kuwanyima kazi vijana wanne waliokuwa na kasi ya kuchapa maneno 120 kwa dakika kwenye taipureta, alitoa zoezi lisilowezekana.

Alisema, “Kwa kuwa nyote ni wataalam, sasa sharti tupate mshindi. Tutaweka taipureta nyuma yako; nawe utapinda mikono yako na kupiga taipureta huko nyuma ili kuonyesha umahiri wako. Nafasi iko wazi.”

Waliona haiwezekani. Hawakujaribu. Walijua jambo moja, kwamba hizo zilikuwa njama za ofisa kuendelea kuajiri ndugu yake ambaye hakuwa mjuzi. Kumlinda. Ndivyo rais anavyotaka kufanya. Hapana. Ndivyo alivyofanya.

Sitaki rais awe na fikra kwamba alionao katika baraza lake la mawaziri ndio pekee wenye akili na uwezo wa kutenda. Wako wengi nje ya baraza. Vilevile si Kikwete pekee awezaye kuwa rais katika nchi hii. Wamekuwepo. Wametoka na weningine wengi wapo.

Kwa nini Rais Kikwete anashindwa kuelewa kuwa kwa nafasi aliyoko, anaweza kutenda maajabu na kuwa shujaa mwingine wa nchi hii kwa kuwatosa wasiobebeka na kusonga mbele?

Sitaki rais ambaye haoni kuwa hata yeye anaweza kujikuta mmoja wa wasiobebeka na akatoswa na wale ambao angekuwa amewatosa mapema. Itakuwa habari kuu kwa gazeti letu.

Mwandishi wa makala
hii ambayo itachapishwa
Tanzania Daima Jumapili,
14 Oktoba 2007 anapatikana
kwa simu +255 (0)713 614872; baruapepe:
ndimara@yahoo.com

1 comment

Ansbert Ngurumo said...

nimeipenda SITAKI na ile ya tambiko la wazee. Imekuja wakati wake. Asante.

Powered by Blogger.