MAHAKAMA YA KADHI TANZANIA
Kikwete asikimbie hoja
Na Ndimara Tegambwage
RAIS Jakaya Kikwete hataki kuhusishwa na kilichomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 kuhusiana na Mahakama ya Kadhi nchini.
Anasema chama chake na serikali yake havina sera ya kuwa na mahakama ya kadhi. Aidha, anasema hilo siyo suala lake binafsi.
Mahakama ya kadhi ni kilio cha waislamu nchini kwa miaka mingi sasa; karibu tangu mara baada ya uhuru. Waislamu wamekuwa wakiitaka serikali irejeshe mahakama ya kadhi iliyokuwepo nchini kabla ya uhuru na muda mfupi baada ya uhuru.
Kwa ufupi, mahakama ya kadhi hushughulikia mambo ambayo yanahusiana na imani na taratibu za madhehebu ya kiislamu. Kupeleka mambo hayo mbele ya mahakama ya sheria za nchi, hufikirika kuwa muhali.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na hoja kwamba mahakama ambayo ni moja ya nguzo za dola, inakidhi matakwa ya watu wa imani zote, kwani katiba ya nchi haina madhehebu wala dini.
Katika hili, hakuna mwanzilishi wa jana au juzi wa madai ya mahakama ya kadhi. Ni maombi, matakwa na shinikizo la kisirisiri na la wazi, la muda mrefu. Linaibuliwa leo kutokana na kujitokeza kwa hoja ya “kushughulikia suala la mahakama ya kadhi” katika Ilani ya CCM ya mwaka 2005.
Hii ilikuwa mbinu ya kisiasa ya kukumbia kura za walioamini kuwa mahakama ya kadhi ni muhimu na ingekidhi kiu yao.
Sasa Rais Kikwete anakana kusimamia kifungu hicho katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Anadiriki kusema kwamba hakushirikishwa kuandika ilani.
Hakuna anayesema mahakama ya kadhi ni sera ya CCM au serikali. Bali yaliyomo kwenye ilani ni matakwa ya CCM ambayo huweza kutungiwa sera pindi uamuzi wa utekelezaji wake unapokuwa umechukuliwa.
Rais Kikwete hastahili kukimbia ilani ya chama chake. Hata kama hakushiriki kuiandika; huo ndio ukweli au ghiliba ya chama chake. Hayo ndiyo mahubiri yaliyosambazwa kumtafutia urais na akaupata.
Sasa kama Kikwete anasema hakuandika ilani ya uchaguzi ya CCM, wakati kila kukicha anasema nchi nzima inatekeleza ilani ya chama kilichoko madarakani, ni ilani ipi itekelezwe na ipi itelekezwe?
Kauli ya rais ni ya kukwepa wajibu; na kwa kauli hiyo pekee, anapaswa kuadabishwa na chama chake. Atakana mangapi katika ilani hiyo?
Ameishayavulia. Sharti ayaoge.
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la MwanaHALISI la Jumatano, 14 Novemba 2007)
No comments
Post a Comment