Header Ads

LightBlog

MAJADALA KUHUSU UFISADI


SITAKI
Mkapa bado mwanasiasa, ajibu tuhuma

SITAKI Benjamin William Mkapa, yule rais mstaafu, aseme asiulizwe juu ya lolote linalohusu utawala wake kwa madai kwamba amestaafu.

Sitaki aseme kwamba hataki vyombo vya habari na wadadisi wamjadili au wamfuate, au wafuatilie yale aliyotenda akiwa madarakani.

Hii ni kwa sababu Mkapa hajastaafu siasa na hawezi kustaafu siasa. Kwa mujibu wa katiba na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkapa bado ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Ni Halmashauri Kuu ya chama hicho inayotunga na kusimamia sera zinazotawala hivi sasa. Akiwa mjumbe, bado ni mwanasiasa wa nafasi ya juu.

Hatua ya rais aliyestaafu kuendelea kuwa mjumbe wa vikao vya juu vya chama chake ambacho bado kinaendelea kushika utawala, ina maana kwamba bado anaheshimika na kuthaminiwa.

Ina maana ubongo wake bado unahitajika katika kukuza, kulinda na kuimarisha utawala wa chama hicho; uwe mzuri au mbaya.

Ina maana Mkapa bado ni tegemeo, kwa kiasi kikubwa, la chama chake katika kurithisha fikra, kuzalisha mpya na kuandaa viongozi wapya wa kukiendesha chama hicho.

Si hayo tu. Aliyofanya Mkapa ndiyo nguzo ya yanayofanyika leo, ndani ya chama chake na ndani ya serikali. Hii ina maana kwamba kuna mwendelezo wa aliyofanya; naye anaendelea kuyanawirisha kwa njia ya ujumbe katika vyombo vya chama kilichoko ikulu.

Hapa Mkapa hawezi kusema wala kusemewa kwamba amestaafu siasa. Ndiyo hasa anaanza siasa; na mara hii akiwa na mali na muda zaidi wa kukisaidia chama chake.

Wanaomfuata Mkapa, kwa maswali au kwa hoja, hawajakosea. Akiwajibu kuwa amestaafu siasa, tutamtilia mashaka kama kweli akili yake ingali sawa baada ya kustaafu urais na uenyekiti. Tutasema kapungukiwa.

Wakitokea wanaomsemea kuwa amestaafu siasa kwa hiyo aachwe kudadisiwa, hao tutasema ama hawajui watendacho au wametumwa kufanya bwabwaja na wanalipwa kwa kupiga kelele; lakini wanadharauliwa na anayewatuma kwani yeye anajua ni wajinga tu.

Hii ni kwa kuwa Mkapa bado ni mwanasiasa. Na katika siku chache zijazo anaweza kuteuliwa kubeba Sh. 6.5 bilioni za “kiongozi bora wa Afrika” kwa mujibu wa watoa nishani ya Mo Ibrahim.

Hiyo ni tuzo ya kisiasa. Naye Mkapa, pamoja na kushutumiwa kwa muda mrefu sasa, kwa kukiuka maadili ya utawala akiwa ikulu na kuwekwa orodha ya “mafisadi,” amekaa kimya ili kauli zake zisisikike na kurekodiwa na labda kuathiri nafasi yake katika kuwania tuzo hiyo.

Mkapa anaendesha Mfuko wa Mkapa wa kupambana na UKIMWI. Viongozi wa Tanzania wanajua vema kwamba walisukumwa na nchi wafadhili kuingiza UKIMWI katika ajenda za taifa na hiyo ikawa ajenda ya kisiasa kwa kila jukwaa.

Anachofanya katika taasisi yake ni mwendelezo wa jukwaa la kisiasa na utekelezaji wa azima ya kisiasa ambayo Rais Jakaya Kikwete anaendeleza pia kwa kuhimiza upimaji wa afya.

Mkapa angali anapata marupurupu yake ya kisiasa hadi mwisho wa uhai wake. Juu ya hayo, imetungwa sheria ya kumlinda rais mstaafu na hata kuzuia asikejeliwe. Ni siasa tupu. Ni siasa hadi kifo.

Hata bila kutaja siasa, Mkapa ni “mtu wa umma.” Nafasi aliyofikia; ile ya mwenyekiti taifa na rais wan chi, inamweka jukwaani kwa kila mmoja kumjadili, kumdadisi na kumchunguza kama kweli alistahili au alibambikwa tu.

Lakini hapa kuna sababu nyingine ya kumfuata Mkapa. Ametoka ofisini. Wengine wameingia. Sasa sharti wadadisi wajue ameacha nini pale, kwa njia ya tabia na mwenendo wa kisiasa na mfumo wa utawala.

Mkapa alifanya biashara akiwa ikulu kwa kutumia muda wa wananchi. Mkapa alihudumiwa na vyombo vya fedha na vingine bila shaka kwa kasi ya “wanaohudumia rais” na siyo mteja wa kawaida. Rais alijua na alinyamazia ufisadi uliotendwa chini ya utawala wake.

Mkapa ni mtuhumiwa mbele ya mahakama ya wananchi kupitia njia mbalimbali za kumwasilishia mashitaka; kwa mfano vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.

Hivi majuzi, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amemtuhumu Mkapa kwa kubinafsisha CCM kwa matajiri, kushindwa kuongoza chama hicho na kubadili kanuni zake bila kufuata taratibu.

Yote haya ni kutaka Mkapa aseme. Ajibu. Ili Watanzania waanze kujiweka tayari kukabili utawala ulioingia ikulu na kuzuia usifanye vituko, vitimbi na ufisadi; mambo ambayo yanaongeza mzigo kwa wananchi na hata kuchafua roho zao.

Kimya cha Mkapa, siyo tu kinaonyesha jeuri na ubabe, bali kinadhihirisha amekabidhi yaleyale yanayolalamikiwa kwa wale waliochukua nafasi yake.

Kama hivyo ndivyo, basi huo ni msiba mkubwa. Kama sivyo, wananchi wanatarajia hata Rais Kikwete ashirikiane nao kudai majibu kutoka kwa Mkapa juu ya tuhuma zinazomwandama.

Kama alivyo Ali Hassan Mwinyi, Mkapa bado ni mwanasiasa. Mema na mabaya yake bado yanamfuata hata nje ya ofisi. Asipotaka kujibu tuhuma atahukumiwa kama anavyoonekana. Na hivyo ndivyo alivyo.

(Makala hii ya Ndimara Tegambwage ilichapishwa katika safu yake ya SITAKI katika gazeti la Tanzania Daima toleo la 21 Oktoba 2007.)

No comments

Powered by Blogger.