Header Ads

LightBlog

Uchumi wa Tanzania utakua lini?

SITAKI kuamini sababu za watawala wa Tanzania za kutotaka kuingia haraka katika Shirikisho la Afrika Mashariki.

Ni kwa sababu hizo Uganda inasema wanaotaka na walio tayari waendelee na shirikisho. Hii ina maana kwamba wenye woga, mashaka na kutojiamini, watajiunga na shirikisho hapo baadaye.

Na sababu za Tanzania kutojiunga na shirikisho katika mpango wa kasi ni dhaifu sana. Eti Tanzania “inapenda sana kujiimarisha kwanza kiuchumi” ndipo isonge mbele.

Maswali: Nani alichelewesha Tanzania kuimarika kiuchumi? Nani ana uhakika kwamba uchumi wa Tanzania utaimarika leo, kesho au keshokutwa? Kuimarika kiuchumi kuna maana gani; ni kufikia viwango vya Kenya au Uganda?

Lakini swali na suala kubwa hapa ni: Nani anajua kuwa uchumi wa Tanzania haujawa imara? Ni rais na mawaziri wake au hata wananchi kwa ujumla wao wanajua hivyo?

Je, wananchi wanajua nchi yao ilipofikia katika maendeleo kwa kulinganisha na Uganda na Kenya au wanaambiwa na rais na wanasiasa, tena kwa kauli zinazotafuta kuungwa mkono?

Je, katika kura ya maoni, wananchi waliposema hawataki shirikisho lije haraka, walikuwa wanajua shirikisho la kisiasa ni nini au maoni yao yalikuwa juu ya kukataa kile ambacho hawakijui?

Nani alitegemea wakazi wa miji midogo na vijiji, ambao hawajui wala hawajawahi kuelezwa lolote juu ya jumuiya, kukubali kuingizwa katika kile ambacho walikuwa hawajui?

Je, si kwa kukataa shirikisho kwa njia ya haraka, wananchi walikuwa wanawaeleza watawala kuwa watawala hawajafanya kazi ya kuelimisha umma juu ya shabaha na matunda ya shirikisho?

Nani atakataa kwamba maoni juu ya shirikisho ulikuwa mtihani wa watawala kwa watahiniwa, ambao ni wananchi; lakini wanaoleta mtihani walikuwa hawajawahi kufundisha hata kidogo?

Kama hujafundisha, lakini umetunga mtihani, kwa nini usieleweke kuwa umedhamiria watahiniwa wote washindwe isipokuwa wale waliokuwa na mawasiliano nawe au wenye uwezo wa kupata elimu kwa njia tofauti?

Lakini katika hili, mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete walizunguka nchi nzima kueleza umuhimu wa kuingia katika shirikisho haraka.

Je, mawaziri waliokuwa wakiendesha kampeni kuwataka wananchi wakubali mpango wa haraka, hawakubaliani na Rais Kikwete?

Je, mawaziri hao hawajui au hawakujua hali ya uchumi wa Tanzania kiasi kwamba wanapingana na rais wao? Na kama mawaziri wanapigana na rais, wanatafuta nini katika nafasi zake za uteuzi?

Kama kweli Rais Kikwete anajua, anaamini na kukiri kuwa sharti Tanzania ijiimarishe kwanza kiuchumi ndipo iingie shirikisho, kwa nini bado anakumbatia mawaziri waliokuwa wanapingana naye?

Au tudadisi zaidi, ni lini Kikwete alijua kwamba Tanzania haijaimarika kiuchumi; kabla ya kuagiza maoni na kutoa ajira kwa wakusanyaji maoni au baada ya maoni kutangazwa?

Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa Afrika Mashariki walioketi na kuamua wananchi waulizwe juu ya shirikisho la haraka au la polepole.

Kama kweli utawala wake unasema kile unachoamini, kwa nini hakujua au hata kushauriwa mapema, kwamba uchumi wa Tanzania haujaimarika na hivyo hakuna haja ya shirikisho kwa njia ya haraka?

Ukichunguza kwa makini, utaona kwamba kuna sababu nyingine, na tofauti kabisa, za Rais Kikwete kukataa shirikisho kwa njia ya haraka. Zipo. Aziseme mwenyewe. Hakuna wa kumsemea.

Tuulize tena: Hivi kigezo kikuu cha kuingia Shirikisho la Afrika Mashariki ni kuwa na uchumi ulioimarika na siyo kuunganisha wananchi na hali zao za kiuchumi za wakati uliopo?

Shirikisho la kisiasa hujenga mazingira sare kisiasa kwa wanachama husika ambayo huchochea uhuru, utashi na kutoa fursa sawa kwa watu na taasisi zao kujituma na kujiendeleza ili kujenga na kuimarisha uchumi.

Shirikisho, katika hali yoyote ile ya kiuchumi, linaweza kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi na watu wake, wakati jeuri ya uchumi imara peke yake inaweza kuleta mgawanyiko.

Hapo ndipo Rais Yoweri Museveni wa Uganda anaona arudie maoni yake ya awali kabisa, kwamba walio tayari kwa shirikisho waanze; wasio tayari watakuja baadaye.

Sitaki wanaotaka shirikisho wasubiri wale ambao hawana kalenda ya kuwa na uchumi imara.

Mara baada ya vita dhidi ya dikiteta Idi Amin Dada, rais alitangaza miezi 18 ya “kufunga mikanda” ili kurejesha uchumi katika hali nzuri.

Miezi hiyo ilipomalizika, serikali ikatangaza miezi mingine 18. Hali iliposhindikana kubadilika, watawala wakaacha kusema lolote juu ya miezi ya kufunga mikanda. Mikanda ikafungwa hadi leo.

Katikati ya ubadhilifu, ufujaji wa maliasili na raslimali za nchi, mikataba ya kinyonyaji, wizi wa moja kwa moja wa fedha za umma, rushwa na ukosefu wa ajira, hakuna awezaye kutabiri lini uchumi imara utapatikana.

Acha wanaotaka haraka Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki waanze. Wenye mikongojo wataingia siku watakapowasili mjini, mradi milango iko wazi, lakini huenda kwa gharama zaidi.

Na ubishi kuhusu hili unaweza kupandikiza mbegu ya chuki miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki na hatimaye uhasana ambao utakuwa mgumu kuung’oa.

(Safu ya STAKI huandikwa na Ndimara Tegambwage na huchapishwa na Tanzania Daima, Jumapili. Makala hii ilichapishwa 16 Septemba 2007)

Mchango wa msomaji
Hongera sana kwa makala. Swali la nyongeza: Wakati Tanzania inaimarisha uchumi wake je, Kenya na Uganda watakuwa wamekaa wanaisubiri ijiimarishe? Je, ni haki uzembe wetu uwacheleweshe wao? Je, uchumi wetu usipoimarika mapema itakuwaje? Na je, uchumi wetu ukipanda wa kwao ukashuka, itakuwaje?

By Maswi, Bunda, Mara
Simu: +255 (0) 784477900

2 comments

SIMON KITURURU said...

Viongozi walioko jikoni sasa hivi Tanzania wasiwe na wasiwasi sana , kwa sababu bado tunaongea tu: Na kwasababu tuko pamoja nao,wanajua tuna mchezo wa kusahau kirahisi. AU?
Kikubwa ni kwamba wengine hatuongei tu na tunafuatilia, tafakari hifadhi na jkama hawajastukia tunakuja kubadilisha.
Kwa sasa hivi Nawaelewa kwanini hawastukii. Hawajastukia leo hii ,Komredi namba mbili wa khmer Rouge wa Cambodia ndio anapelekwa lupango baada ya madhambi watu walionalili mara ya mwisho mwaka 1979?Sisi wa sasa je, tuwanukuluo kwa simu kamera na......

Chris said...

Nilikuwa najiuliza maswali mengi sana ambayo hadi hivi sasa sijapata majibu yake niliposikia ya kuwa Serikali imeunda tume/kamati kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kujiunga na shirikisho la Afrika ya Mashariki. Miongoni mwa maswali hayo ni wananchi wa aina gani ambao kamati iliwahoji na kisha kukusanya maoni yao? Je ni wananchi wangapi wanajua umuhimu wa shirikisho hili? Je serikali ama tume iliwaandaaje wananchi kuhusiana na suala zima kwa ujumla? Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo uchumi wa Tanzania unavyozidi kudidimia! Sasa sijui utakuwa lini na kwa kasi ipi? Na hali halisi kwa hivi sasa ikoje? Najua kuna mseomo wa kwamba, "wengi wape," Lakini hii haimaniishi kwamba wengi daima huwa sahihi, wanaweza kukosea hasa kwa kutokujua kwa maana ya kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya suala husika. Kwa mtizamo wangu ni kwamba serikali pamoja na maoni ya wananchi lakini ndo ingeweza kucheza kete ya mwisho na kuwaelimisha wananchi ni nini kinachoendelea. Nina imani kabisa wananchi waishio mipakani hasa hususani Kagera, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, n.k. wanafahamu fika umuhimu wa shirikisho hili na huenda wamekwishaonja matunda yake. Kwa kutokuendelea zaidi ninaiomba serikali ilichunguze na kulisoma zaidi suala hili.

Powered by Blogger.