Header Ads

LightBlog

Wahujumu wa mbuga ya Serengeti

SITAKI

SITAKI watawala na matajiri wachache kutoka nje waangamize maliasili za Watanzania na jamii ya kimataifa, kwa kugeuza mbuga za wanyama kuwa miji.

Huu ni mpango wa kuua au kuhamisha au kufukuza wanyama, ndege, wadudu na hata kuharibu mazingira katika mbuga za wanyama.

Wasomaji, kupitia safu ya barua, katika magazeti mbalimbali, wamekuwa wakiuliza, “barabara za lami za nini katika mbuga za wanyama.”

Tujadili mbuga ya wanyama ya Serengeti. Mbuga hii ni tajiri sana wa wanyama. Humu kuna aina nyingi za wanyama na na baadhi ambao hawapatikani kokote kwingine duniani.

Serengeti ni maliasili ya taifa na dunia kwa ujumla; ni urithi wa vizazi na vizazi unaotokana na nguvu za asili. Bali, na ndivyo ilivyo, ni kivutio kikubwa cha watalii na chanzo cha mapato ya fedha kwa Tanzania.

Watu wa mafaifa mbalimbali wamekuwa wakija nchini kuona wanyama katika mbuga hii; na kila anayetoka huko anakuwa balozi wa Serengeti na Tanzania.

Sasa serikali imeamua kuruhusu matajiri kutoka nje kuingia Serengeti na kujenga hoteli kubwa kwa madai ya kuhudumia watalii.

Kuna walioanza kujenga hoteli. Kuna wenye mipango ya kujenga barabara za lami. Serikali imesema itaita matajiri wengine kuwekezaji katika hoteli katika mbuga.

Kana kwamba hiyo haitoshi, matajiri wanasemekana kuwa wameanza kujenga viwanja vya ndege ndani ya mbuga. Wanadai kuwa hiyo itarahisisha usafiri kwa wamiliki wa hoteli na watalii.

Huu ndio msiba mkubwa. Mbuga yetu, Serengeti, imevamiwa. Wanyama, ndege, wadudu na mandhari ya Serengeti, vimevamiwa.

Ni serikali iliyoruhusu uvamizi wa urithi wa Tanzania na dunia nzima. Kwa hatua hiyo, chanzo kingine cha mapato ya taifa kimevamiwa pia.

Matokeo ya uvamizi uliohalalishwa na serikali ni haya: Wakati wa ujenzi wa hoteli kunakuwa na mwingiliano mkubwa kwenye mbuga.

Magari makubwa, yaliyobeba vifaa vya ujenzi hupiga kelele nyingi na zinazofika mbali. Kelele hizi huwastua wanyama, ndege na hata wadudu waliomo katika mbuga.

Kelele hizi hutishia amani ya wanyama na uhai wao; husababisha watawanyike kwa hofu, na huweza kwenda mbali na hata wasiweze kurudi katika maeneo yao ya asili.

Kelele za binadamu, wale wajenzi wa hoteli ambao mara nyingi hupenda kufanya kazi zao kwa kuimba au kutoa sauti kubwa katika kuhimizana, ni tishio kwa wanyama.

Ujenzi wa barabara za lami huchukua muda mrefu. Kwa kipindi chote, huwa kuna mwingiliano wa magari na kelele zisizo za kawaida.

Shughuli zote hizi za ujenzi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya ndege husababisha wanyama kutawanyika na wasiweze kurudi walipokuwa.

Hawawezi kurudi walipokuwa awali kwa vile sasa kuna watu, kuna hoteli, kuna barabara zenye wingi wa magari; kuna wingi wa wasafiri na mazingira yamebadilika kabisa.

Lakini kuna tishio kubwa zaidi. Hili ni mingurumo ya ndege wanaotua kwenye viwanja. Kelele kali wakati wa kutua na kuondoka, hutishia wanyama na kuwasambaza zaidi wasiweze hata kurudi katika maeneo ya awali.

Uvamizi huu kwa wanyama na makazi yao unasababisha washindwe kutulia na kustawi; washindwe hata kuingiliana ipasavyo na kuzaliana. Hili linaweza kuchangia katika kupungua kwa idadi yao.

Ukweli mwingine ni kwamba wanyama wanaweza kutawanyika na kwenda nchi nyingine ya jirani; na Tanzania ikawa imepoteza, mara moja na milele, utajiri wake wa asili.

Hoja kubwa hapa ni kwamba watalii kutoka nje ya nchi wamekuwa wanakuja nchini kuona wanyama. Hawaji kulala kwenye hoteli kubwa na za kisasa kama zile zilizoko mijini.

Hapa kuna njama. Watawala na wawekezaji wanaharibu mifumo ya maisha ya wanyama; wanawatishia na kuwaondoa kwenye makazi yao; wanawahamishia hata nchi nyingine; halafu wanadai kuwa wanaendeleza utalii.

Waongo! Hakuna utalii. Kuna uharibifu wa makazi ya wanyama na mazingira kwa ujumla. Na hii haiwezi kuwa bure.

Mtu analazimika kuuliza, “Watawala wamelipwa nini na kwa kiasi gani ili waharibu maliasili ya nchi na dunia kwa ujumla?”

Sitaki kuamini kwamba penye barabara za lami; hoteli nyingi na kubwa na viwanja vya ndege na mingurumo angani, bado panaitwa mbuga ya wanyama.

Sitaki kuamini kuwa penye mwingiliano wa watu wengi wanaofanya shughuli mbalimbali, na siyo kuona wanyama katika utulivu wao, bado panaweza kuitwa mbuga ya wanyama.

Serikali na wawekezaji waroho wanaua maliasili ambayo ni urithi wa binadamu wote.

Kuna haja ya kuwaambia hapana! Sababu zipo: Wanayama hawahitaji barabara za lami, magari wala hoteli. Na watalii hawaendi Serengeti kuona barabara za lami, hoteli wala ndege. Wanakwenda kuona wanyama.

Kinachofanyika ni ukatili kwa wanyama, uchafuzi wa mazingira na uhujumu kwa maliasili ya Tanzania na binadamu wote. Tukatae hili.

(Itachapishwa Sept. 23 2007 katika Tanzania Daima Jumapili katika safu ya SITAKI)

1 comment

Ansbert Ngurumo said...

Nakupongeza tena kwa hili. Nimeona Mkono alivyoogopa kwenda mahakamani. Heri angekaa kimya maana aliyosema yamefunue mengine yaliyokuwa yamefichika. Ngoja tuone kila mmoja atakavyojitokeza kujitetea. Stori zipo nyingi. Tusubiri.

Powered by Blogger.