Header Ads

LightBlog

Rushwa inapokuwa mbeleko CCM

SITAKI kuamini kwamba rushwa ndiyo imekuwa mbeleko ya kubebea wagombea katika uchaguzi unaoendelea wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ngazi zote.

Taarifa za vyombo vya habari zimejaa ripoti za utoaji rushwa kuanzia ngazi ya chini kabisa ya uongozi katika chama kilichoko ikulu, hadi nafasi za juu.

Kinachoendelea hivi sasa katika uchaguzi ni “nipe-nikupe” au “mzee kanituma” au “pokea salaam za Waziri au Waziri Mkuu” au “Mwenyekiti wa Taifa kanituma.”

Kwa hali ilivyo, hata wanaoogopa kuulizwa ushahidi, wanaweza kutoa kauli iliyo salama kabisa kuwa, “Tunaona wanachama, wagombea na mawakala wao wakigawa fedha katikati ya pilikapilika za uchaguzi.”

Lakini hakuna haja ya kukimbia neno “rushwa” kwani hutolewa na kupokelewa kwa aina na njia mbalimbali.

Rushwa inaweza kuwa kauli kwa njia ya ahadi; takrima kwa njia ya chakula na pombe; zawadi kwa njia ya nguo, baisikeli au hata gari; na fedha kwa maelekezo ya kujikwamua kiuchumi.

Yote haya yameonekana. Yamethibitika. Yamelalamikiwa. Mahali pengine yamezomewa na kulaaniwa. Ni rushwa.

Kilicho kigumu kuamini ni iwapo wanaotafuta uongozi kwa njia hii ya milungula, ndio haohao wanaotaka kuendelea kukaa ikulu na kutawala nchi hii. Hicho ndicho sitaki kuamini.

Nani hajasikia majigambo ya CCM, kila kukicha, kwamba “sera tunayotekeleza ni ya Chama Cha Mapinduzi ambacho kilipata ushindi wa kishindo?”

Tuulize taratibu, nani sasa, baada ya taarifa za kuaminika juu ya matumzi ya rushwa, ataweza kuchagua uzao wa mlungula kwa kishindo na kuukabidhi utawala?

Nani hajasikia CCM, sema viongozi wake, wakijigamba na kujitutumua mbele ya halaiki, kuwa watapambana na rushwa na kukariri msemo “rushwa ndiyo adui wa haki?”

Leo na kesho, baada ya ushahidi wa wazi, na ule wa kimazingira, juu ya utoaji na upokeaji wa rushwa, nani ataamini tena kuwa CCM inakiri kuwa “rushwa ndiyo adui wa haki?”

Na kukiri hakutoshi, kwani kunaweza kuishia kwenye kauli. Katika mazingira haya, nani atategemea CCM itende kufuatana na kauli yake ya kupambana na rushwa?

Kama uongozi wa chama kilichoko ikulu, utapatikana kwa njia ambayo wanachama na viongozi wake wengi wanajua au wanaamini, kuwa ni kwa rushwa, nani atatarajia mabadiliko kwa maana halisi ya maendeleo ya wananchi?

Nani atatarajia amani katika minyukano ya kupora raslimali za taifa; kuuza maliasili za wananchi na kunyang’anyana madaraka katika kuhudumia wawekezaji wa nje?

Kilio cha sasa cha rushwa hakitoki nje ya CCM. Kinatoka ndani ya chama hicho. Wenye nacho au wenye wajomba, wanatamba na kutesa. Wasionacho na mashabiki wao, wamenywea kama gugu lililong’olewa wakati wa kiangazi.

Na huu ni wakati mbaya sana kwa chama kilichoko ikulu kupata hata harufu ya rushwa. Hii ni kutokana na madai ya rushwa yaliyozagaa katika mikataba ya serikali, utendaji na maamuzi makuu ya watendaji serikalini.

Kwa uchaguzi uliojaa madai ya rushwa na hivyo kuleta watuhumiwa wakuu wa rushwa, nani sasa atachunguza IPTL, ule mradi ambao kutajwa kwake tu, hufanya waliokuwa wizarani na ikulu wakati huo, kupata tumbo la kuhara.

Kama viongozi waliochaguliwa na wanaoendelea kuchaguliwa wanapatikana kwa mtindo wa rushwa, nani atachunguza baba, mama na dada wa Richmond?
Nani, miongoni mwa watakaokuwa wamepatikana kwa rushwa anaweza kupendekeza uchunguzi juu ya matumizi mabaya ya ikulu; kule kuigeuza “meza ya sokoni?”

Nani, kati ya waliopatikana kwa mlungula, anaweza kupendekeza uchunguzi katika ununuzi wa ndege za jeshi zisizo za kijeshi; rada ya ndege iliyozeeka na ndege ya rais iliyoko “likizo?”

Atatoka wapi, miongoni mwa hao, ambaye atachunguza harufu ya rushwa katika mikataba ya madini, iliyosainiwa ndani na nje ya nchi?

Yuko wapi, miongoni mwao, atakayechunguza matumizi ya serikali, madai dhidi ya Benki Kuu (BoT), miliki ya maliasili kama misitu na mbuga ambavyo vyote vinaonekana kuwa mikononi mwa watu kutoka nje?

Nani atanyosha kidole kumtetea mkazi wa mwaloni Mwanza, Bukoba na Musoma ambaye hawezi kupata samaki kutoka Ziwa Viktoria, bali anaambulia mapanki?

Kilio cha wana-CCM wengi dhidi ya rushwa ndani ya chama chao, kina ujumbe mkubwa; kwani hakuna kilicho cha wana-CCM peke yao. Uporaji uliorasimishwa na uongozi uliotokana na rushwa, utaua wote – waliomo na wasiokuwamo.

Kinacholeta matumaini ni kwamba sauti nyingi za wanaolia, wanaolalama, wanaosuta na kulaani kinachotendeka sasa katika uchaguzi unaoendelea, ni za wanachama wa CCM.

Kwenye mtaji huu, ukiongeza sauti zilizoko nje ya chama hiki, hoja ya kukataa rushwa inaimarika katika jamii. Panapatikana mahali pa kuanzia kusema “Hapana” kwa rushwa na waliopatikana kwa rushwa.

Sitaki mtu adharau hatua hii kwa kusema ni ndogo tu. Ndio, ni ndogo, lakini ni hatua; tena hatua kwenda mbele.

(Imechapishwa katika Tanzania Daima, Jumapili 02 Septemba 2007)

No comments

Powered by Blogger.