Header Ads

LightBlog

UHURU WA HABARI KITANZINI

Hali Halisi Publishers Limited

VITA VIPYA VYA KUUA UHURU WA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
27 Septemba 2007

MwanaHALISI, gazeti linalochapishwa na Hali Halisi Publishers Ltd., lina taarifa juu ya kuwepo njama, za mtu mmojammoja na, au makundi, za kuangamiza uhuru wa wananchi wa Tanzania wa kutoa na kupokea habari.

Kuna mienendo ya chinichini, ya kusambaza vitisho kwa vyombo vya habari, hususan MwanaHALISI, wachapishaji wake, wahariri, waandishi na wachangiaji makala na taarifa mbalimbali.

Kwa MwanaHALISI, hilo halikuanza jana. Kwa karibu mwaka mmoja sasa kumekuwa na vitisho kwa njia ya barua za kutukemea, ama kutoka serikalini au kwa watu binafsi, ambao wamekuwa wakitishia kutupeleka mahakamani. Hao tumekabiliana nao kwa kuendelea kuandika ukweli na kutamka kwamba tunashikilia kile tulichoandika na bila kutetereka.

Lakini tangu wiki iliyopita, hasa baada ya vyama vya upinzani kutuhumu viongozi 11 kushiriki ufisadi, njama za kutaka kuangamiza “mdomo” wa wananchi zimekuwa wazi zaidi.

Kwa kuwa gazeti hili lilifanya kazi yake kitaaluma, ile ya kutaja majina ya watuhumiwa wote kwa majina na tuhuma zao kama zilivyowasilishwa na upinzani, sasa karibu kila mmoja anayetaka kujikosha au “kujitetea,” anatishia kushitaki aliyesoma majina hadharani (Dk. Willibrod Slaa), gazeti la wananchi la MwanaHALISI na kampuni ya uchapaji ya Printech.

Mlolongo wa ahadi, na huenda azma, za kweli au za kutishia tu gazeti na wachapishaji wake, ni njia mpya ya kutaka ujengeke woga miongoni mwa wachapishaji na wachapaji, ili kadri mambo yanavyoendelea kufumuka, pasiwepo wa kuyaweka wazi kama tuhuma zilivyowekwa wazi.

Hawa wanashindwa kuelewa kwamba ni chombo hikihiki ambacho kitaandika ukweli mweupe pale madai yatakapokuwa yamethibitika au yamekanushwa. Kukipoteza chombo hiki ni msiba mkubwa kwao na jamii; lakini bahati mbaya hawajui.

Afadhali wakili Nimrod Mkono amesema hatashitaki MwanaHALISI kwa kuwa hatuna fedha za kumlipa. Hapa yeye aliishajiamulia kushinda na sisi kushindwa hata kabla hajaenda mahakamani. Lakini ukweli unabaki palepale, kwamba hatuna fedha za kuwapa wenye fedha. Fedha tulizonazo ni kwa ajili ya kuendeleza haki na uhuru wa wananchi wa kupata habari.

Hatua ya haraka ambayo inaweza kuzima uhuru wa chombo cha habari, na katika hili najadili MwanaHALISI, ni kuliwekea gazeti pingamizi ili lisichapwe.

Tayari uongozi wa Printech umepokea vitisho kwa njia mbili: Njia ya kwanza ni kuambiwa moja kwa moja kwamba kiwanda chao kitafungwa. Njia ya pili ni kutishiwa kushitakiwa mahakamani. Yote hayo mawili yanaikabili pia MwanaHALISI.

Kuna mambo mawili muhimu katika kuangalia hali hii: Kwanza, Printech siyo kiwanda cha serikali wala cha watuhumiwa. Ni kampuni inayojitegemea. Imepewa na wafadhili mitambo ya uchapaji kwa shabaha moja kuu ambayo ni: Kukuza vyombo vya habari katika Tanzania na Afrika.

Pili, siyo siri kwamba mashine za uchapaji kama iliyoko Printech, ziko pia katika nchi za Zambia, Lesotho, Botswana na Zimbabwe. Mipango iko njiani kuweka mashine kama hizo nchini Msumbiji.

Mradi huu muhimu wa kuinua uwezo wa wachapishaji wachanga kwa shabaha ya kukuza demokrasia, uko chini ya uangalizi wa Mfuko wa Kuendeleza Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (SAMDEF – Southern Africa Media Development Fund).

Kwa vyovyote vile, Printech siyo mradi wa kutishiwa na yeyote anayetaka kufanya hivyo. Tunachapa MwanaHALISI katika kampuni hiyo kwa kuwa tunathamini msaada wa wanaothamini uhuru na ubora wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla.

Wafadhili wa Printech, akiweno George Soros ambaye ni mwanzilishi wa asasi ya Open Society Institute (OSI), yenye matawi mengi duniani, watashangaa nchi hii kuona inataka kuharibu hata msaada mzuri kama huu, uliolenga kuleta ustawi na maendeleo kwa watu wote.

Katika MwanaHALISI tunajitahidi kunukuu jamii na watu wake kama wanavyotamka; kama wanavyoambiwa na kama wasemaji walivyosikika. Na katika hili hatuoni ubaya, kosa wala jinai. Tunaona fahari na faraja.

Ni matumaini yetu kwamba Printech haitayumba katika kufanya kazi iliyoundiwa na kutekeleza wajibu wake bila woga wala upendeleo.

Tuna mkataba wa kuchapa gazeti Printech. Tuna kanuni kwamba yaliyomo humo siyo lazima yawe maoni ya wachapaji. Msingi huo ukizingatiwa, na MwanaHALISI ikazingatia taaluma, ukweli na uaminifu, hakuna wa kuweza kutuyumbisha.

Nafarijika na kauli ya Meneja wa Printech, Richard Seni aliyoitoa kwa MwanaHALISI jana (26/09/2007), kuhusiana na vitisho kwake kutokana na kuchapa gazeti letu. Alisema kwamba hatasikiliza vitisho katika kutekeleza wajibu wake.

Hata hivyo bado hivi ni vita vikubwa kati ya pande mbili: Wale wanaotaka kuzima habari juu yao, wakati wakiwa katika ofisi za umma; na wale walioapa kuweka kwenye rekodi kila kinachosemwa ili wananchi wasome, waelewe, watafakari na waamue wenyewe. Katika hili, tukiungwa mkono pia na jamii, tutashinda. Ujumbe wetu kwa kila mmoja ni kwamba hatutaki chombo chenu kife.


Saed Kubenea
Mkurugenzi Mtendaji
Hali Halisi Publishers,
Dar es Salaam.

Nakala kwa:
- Meneja Mkuu Printech
- Mtendaji Mkuu SAMDEF – Botswana
- Mkurugenzi – MAELEZO
- Baraza la Habari Tanzania
- MISA-Tanzania
- Vyombo vya habari
- Ofisi za mabalozi wa nchi za nje
- Asasi za kijamii

1 comment

projestus rwegarulila said...

Mzee Ndimala,
Shikamoo! Nimependa jinsi ulivyo tuelimisha kuhusu uhuru wa kujieleza.
Napenda kukuhakikishia kuwa tunako elekea uwazi na uhuru wa kuongea utakuwepo na kama vyombo tunavyo vitumia ni vya kisasa zaidi kila kukicha,basi kumzuia mtu kuongea itakuwa sio rahisi.Mfano ni huu wa blog yako. Angalia jinsi unavyo miliki blog yako unaweza kuandika unacho jisikia.

Powered by Blogger.