Header Ads

LightBlog

Kandoro na ujenzi wa 'matundu' 822


(Makala hii itatoka katika gazeti la MwanaHALISI, Jumatano 26 Septemba 2007)
Na Ndimara Tegambwage

ABBAS Kandoro, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amejitafutia kibarua kikubwa. Naona ni kinene na kizito pia. Anataka kujenga matundu 822.

Kandoro anatafuta msaada kwa wakazi wa Dar es Salaam. Anataka wachange Sh. 10 bilioni ili aweze kukamilisha ndoto yake. Anataka kuthibitisha kuwa ameitikia kwa vitendo wito wa “kukuza elimu.”

Matundu ya Kandoro ni “madarasa.” Anataka kuhakikisha kwamba wanaomaliza Darasa la VII mwaka huu wanapata mahali pa “kuingia.” Anasema madarasa yaliyopo mkoani mwake hayatoshi.

Je, kwa kibarua hiki, Kandoro amepata au amepatikana? Tutajadili. Lakini kwanza tupate nukuu kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere. Alisema yafuatayo:

“Tunapoongelea kupanua elimu ya sekondari tunaharakisha sana kusema kwamba watu watachangia ujenzi kwa juhudi zao. Lakini majengo hayana umuhimu wa kwanza; vitu muhimu katika elimu ni walimu, vitabu na kwa sayansi, ni maabara.”

Je, Kandoro aliishasoma nukuu hii ya Mwalimu? Kusoma kunaweza kuwa kugumu. Je, aliishaisikia popote ikitajwa? Kumbuka hapa si Kandoro peke yake.

Je, Waziri Mkuu Edward Lowassa amewahi kukumbana na nukuu hii? Inawezekana ni zamani sana na sasa amesahau? Je, Baraza la Mawaziri ambako maamuzi makuu yanapita, linajua lolote juu ya matamshi ya Mwalimu?

Je, wataalam washauri katika masuala ya elimu nchini wamewahi kukumbana na kauli ya Mwalimu? Tukubali kwamba hawajawahi kusoma hayo. Je, utaalam walionao haujawahi hata siku moja kuwaelekeza kuwa “matundu” siyo elimu?

Je, inawezekana kadri miaka inavyopita, uwezo wa kufikiri wa viongozi unaendelea kushuka na kupotea kiasi kwamba hawawezi kuona na kuelewa hekima ya wazi?

Kandoro na timu yake wanataka kujenga matundu 822 katika mkoa wa Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa anasema wanafunzi 58,304 wamefanya mtihani wa Darasa la VII na kwamba kati ya hao, 36,557 wanatarajiwa kuingia sekondari!

Mpaka hapa, hata kabla usahihishaji wa mitihani haujakamilika, tayari Kandoro na wenzake “wamepitisha” wanafunzi 36,557 kwenda sekondari; na sekondari zenyewe ndizo anatafutia fedha hivi sasa.

Sasa tujadili. Kuna mambo kadha wa kadhaa ya kuzingatia. Ujenzi wa matundu ambao Kandoro anautafutia fedha hauna tofauti na ujenzi wa awamu ya kwanza hapa Dar es Salaam na mikoani kote nchini.

Ni ujezi wa dharura. Ni ujenzi wa pupa. Ni bandika bandua. Ni kati-pa, kati-bandu! Umakini haba. Baadhi ya matundu yameanza kupata nyufa, miezi mitano tu tangu yajengwe.

Ni ujenzi wa matundu. Yale ambayo wanaoyajenga wanayaita madarasa. Nani hajasikia kilio cha wanafunzi jijini Dar es Salaam hivi sasa kwamba shule zao hazina vyoo na kwamba wanapiga foleni kwenda haja, tena na walumu wao?

Kandoro anasema fedha ziwe zimepatikana ifikapo Oktoba 31 mwaka huu. Ndipo waanze kujenga kwa kasi ya vibarua wa malkia wa nyuki. Mapema mwaka kesho, wanafunzi waanze shule.

Kandoro? Waanze shule bila walimu; alimradi watateua mwalimu mmoja na kumfanya Mwalimu Mkuu. Anachokulia kiko wapi? Bila vitabu. Bila madawati. Bila maabara.

Wiki iliyopita, wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Katende iliyoko Chato, Biharamulo mkoani Kagera, walimfuata Waziri Mkuu ziarani Geita, mkoani Mwanza, kumwambia kwamba tangu waende sekondari hawajapata mwalimu wa kuwafundisha.

Katende ziko nyingi; ziko kila kata, wilaya na mkoa, ambako ujenzi wa shule kwa pupa ya kuongeza idadi ya waenda sekondari umepewa jina la “kukuza elimu.”

Ongezeko la shule haliendani na ongezeko la walimu, vitabu, maabara na hata vyoo. Ni matundu tu ili kukidhi idadi wanayotaka watawala; idadi ya kupigia kampeni ili wapenda elimu waweze kuleta au kuongeza misaada. Basi.

Hii ina maana kwamba hapa hakuna elimu. Zinazoitwa shule panakuwa mahali pa kupigia soga. Ni “vijiwe” vya watoto ambao wangekuwa watu wa manufaa kwa nchi lakini wanashindia hadithi za kwenda “Bondeni” na “Majuu” – Afrika Kusini na Ulaya.

Na takwimu hizi za wingi wa matundu yanayoitwa madarasa, zinasambazwa dunia nzima kiasi kwamba hata juzi, Rais Jakaya Kikwete akiwa Marekani, alikabidhiwa Tuzo na asasi moja ya New York kwa, pamoja na mambo mengine, “mchango wa Tanzania katika kuboresha elimu.”

Akina Kandoro wanamdaganya nani? Mbona uwongo umevuka mipaka kiasi kwamba wao walioutunga, ukiwarudia wanaanza kuuamini?

Watawala wanajua mazingira ya kusoma hayapo na katika shule hizi hawawezi kupeleka watoto wao. Mtoto wa Kandoro hawezi kupelekwa katika shule iliyozungukwa na wavuta bangi kiasi kwamba walimu na wanafunzi wanavuta moshi na harufu ya bangi wakati wote wakiwa shuleni.

Na matundu wanayojenga kwa kasi, bila mazingira ya kuchochea hamu ya kusoma na bila zana, hayana tofauti na magenge ambako kila tabia ambayo jamii inaita “mbaya” inagawiwa bure kwa kila muhitaji.

Kinachoitwa elimu ni maangamizi. Kulundika watoto wa umri kati ya miaka 12 na 20, katika eneo ambako hakutolewi elimu na usimamizi wake hauashirii kuwepo nidhamu itokanayo na kazi, ni kuwaangamiza wakiwa na umri mdogo.

Lakini kinacholeta matumaini ni kwamba hata wazazi wameanza kuelewa. Mwaka jana, wazazi katika mikoa ya Shinyanga na Mara walikataa watoto wao kupanda darasa kwa madai kwamba hawakushinda.

Wakati watawala wanasema watoto wamefaulu, hivyo waendelee na masomo, wazazi wanasema watoto hawakushinda. Wanatoa hoja ambazo serikali haiwezi kuzipangua.

“Utasemaje watoto wetu wamefaulu na sasa waendelee na madarasa ya juu wakati hawajui kusoma na kuandika?” Wazazi wamehoji. Walimu wamebaki wameduwaa. Serikali imeziba macho kwa aibu.

Na Kandoro hataki kulaumiwa peke yake. Anataka wewe na mimi tushiriki maandalizi ya maangamizi kwa kizazi kijacho.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam anasema wakazi wa Dar es Salaam, wachangie ujenzi wa chapuchapu wa matundu 822 kukidhi mahitaji ya wanafunzi ambao tayari amesema lazima watakwenda sekondari.

Mtawala huyu wa Dar es Salaam amelenga hadi kwenye kaya ambako watawala wa serikali za mitaa watapita na kapu kuchangisha fedha kwa ajili ya mradi wake.

Bahati nzuri Kandoro hajataja adhabu atakayotoa au hatua atakazochukua kwa atakayekataa au kushindwa kuchangia mradi wake. Bado anasema ni hiari na watu wote wanajua serikali huwa haina hiari. Hiari iko kwenye asasi za kijamii.
Bali kuchangia ujenzi wa matundu; ambako walimu watakuwa wameokwa kwa wiki sita tu; pasipo na vitabu, madawati, maabara na vifaa vingine; kama ilivyo katika shule zake nyingi; hakika inataka moyo!

ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
Simu: +255 (0) 713-614872

1 comment

Unknown said...

Nakushukuru sana mwaandishi wa makala hii kwa kumkumbusha Kandoro Maneno ya busara aliyotuachia mwalimu Nyerere. Maana hawa viongozi wanakurupuka maamuzi bila kufikiri.

Powered by Blogger.