Header Ads

LightBlog

VITA DHIDI YA RUSHWA TANZANIA


Ndesamburo: Taarifa ndiyo silaha dhidi ya rushwa


Mahojiano kati ya Mheshimiwa Philemon NDESAMBURO, Mbunge wa Moshi Mjini na mwandishi wa habari Ndimara Tegambwage, siku 10 baada ya Ndesamburo kujiuzulu kutoka Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka, hapo 10 Januari 2007. Ndesamburo alijiuzulu kutokana na madai kwamba wabunge wamehongwa katika suala la madai ya Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi dhidi ya Adam Kighoma Malima, Mbunge wa Mkuranga, Pwani. Sababu nyingine aliyotoa ni kwamba utawala (executive) unaingilia Bunge (Mahojiano haya yalihifadhiwa kwenye blogu ya Ansbert Ngurumo. Nayaweka kwenye blogu yangu kurahisisha upatikanaji wake. Asante Ansi kwa kuyahifadhi)

Swali: Wakati ukiongea na waandishi wa habari juu ya kujiuzulu kwako, ulisema kwamba una umri mkubwa, zaidi ya miaka 70. Je, kwa umri huu bado unaweza kushiriki mapambano dhidi ya rushwa?

Jibu: Nani amekwambia kuwa umri ni kikwazo? Niliwaambia waandishi wa habari kwamba hata nikifa, nimeishazidi miaka 70. Basi. Ni umri mkubwa lakini siyo kwamba sina uwezo wa kuchukua maamuzi; tena hapa ndipo nastahili kuwa jasiri zaidi katika kukataa rushwa au tendo lolote la kifisadi. Kupambana na rushwa, kwanza ni dhamira, na pili, ni hatua mahsusi za kukataa kutoa au kupokea rushwa; kukataa kuhusishwa na rushwa na kufanya kila unaloweza kuzuia kitendo cha rushwa. Hapa suala la umri linatoka wapi?

Swali: Bado niko kwenye umri. Nasema ungeanza mapema harakati hizi. Siyo leo. Na kwa msingi huo hakutakuwepo wa kuziendeleza kwani umri wako sasa ni mkubwa.

Jibu: Kupambana kunahitaji kuanzia pale ulipo. Kuanzia pale ulipopata fursa. Nasema suala la uzee haliingii hapa. Wenye umri mkubwa watafanya kile wanachoweza kwa wakati wao. Wataachia wengine wanaowafuata na vizazi vingine.
Hata hivyo, siyo mimi niliyeanzisha mapambano dhidi ya rushwa. Wananchi wengi hawataki rushwa. Kuna asasi mbalimbali ambazo zimekuwa zikipambana na rushwa. Zilianza zamani. Mimi sikuanzisha chochote. Nilisema kuna madai kwamba wabunge wamehongwa. Madai yenye shina katika ofisi kubwa ya serikali – Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa kuwa nami nilikuwa mmoja wa wanaoshughulikia shauri muhimu katika Kamati, nikasema sikupokea rushwa, na kwa msingi huo, hata kama wenzangu watakaa kimya, mimi siwezi kubaki kwenye Kamati na kuyapa nguvu madai ya rushwa. Nikajiuzulu.

Swali: Lakini hayo yalikuwa madai tu. Kwa nini usingesubiri uthibitisho?

Jibu: Uthibitisho kutoka kwa nani? Unataka kuleta mambo ya rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Alikuwa akisema kwamba wanaomtuhumu mtu kula rushwa sharti waje na uthibitisho. Nakwambia, kwa utaratibu huo, hutakamata mtu. Tuhuma peke yake ni msingi wa kutosha wa kufanyia uchunguzi. Sasa kama hutaki hata kufanya uchunguzi, ina maana unaneemesha rushwa, hata kama hukupokea rushwa. Katika suala langu hili, msingi mkubwa ni kwamba aliyesema kuna rushwa ni Waziri Mkuu. Huyu ni mtu mzima. Hawezi kuchomoka na kusema tu. Lazima awe na uhakika. Ni kiongozi katika serikali inayosema inapambana na rushwa na imeamua kwamba, hata ushahidi wa kimazingira ni muhimu katika kukabiliana na rushwa. Kwa hiyo, siyo sahihi kupuuza kauli ya Waziri Mkuu. Siyo sahihi kukataa kufanya uchunguzi. Siyo sahihi kuendelea kuwa katika Kamati ambayo hata Waziri Mkuu anajua wajumbe wake wametuhumiwa kula rushwa.

Swali: Sasa unadhani vita hii unayochochea ukiwa uzeeni itasimamiwa na nani?

Jibu: Nimekwambia kuna asasi nyingi zinazopambana na rushwa. Kuna taratibu kadhaa za serikali zikiwa pamoja na sheria mpya inayopelekwa bungeni hivi karibuni. Sijasema nimejitwisha jukumu lote. Mimi naitikia pale nilipo; na wewe na mwingine afanye vivyo hivyo huko alipo. Ni jukumu la kila mmoja. Bali kuna kitu kimoja muhimu. Nacho ni hiki: Kuna haja ya kuweka kwenye mitaala ya shule za msingi hadi vyuo vya juu, mafunzo juu ya rushwa. Wajue rushwa ni nini? Aina za rushwa. Mifumo ya rushwa. Nani wanadai rushwa, nani wanatoa rushwa na nani wanapokea rushwa. Kwa nini kuna rushwa? Mazingira gani yanarutubisha rushwa? Madhara ya rushwa kwa mtu, jamii na utawala. Haya ni muhimu kujulikana kwa kila mmoja, tangu utotoni, ili kuandaa jeshi kubwa la kupambana na rushwa. Ukianzia darasa la nne unajua rushwa ni nini na ukajenga chuki dhidi ya rushwa, utakulia katika mapambano ya kweli ya kuondoa kansa hii. Hapa utakuwa umewapa watoto na vijana, pamoja na jamii kwa ujumla, misingi ya kukataa kufanyiwa vitendo vya rushwa. Chuki itazaa ujasiri na watapinga rushwa.

Swali: Lakini hiyo itamaliza…

Jibu: Sikiliza kwanza. Fikiria hali hii. Mtoto akue akijua kwamba rushwa inamkosesha au inampunguzia huduma za kijamii; inamwondolea haki ya kutoa mawazo na kushiriki kikamilifu katika jamii; inadhoofisha utawala; inajenga mazingira ya mifarakano na hatimaye chuki na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Huyo mtoto atakuwa imara sana katika mapambano dhidi ya rushwa. Ni vema elimu hii ianze mapema.
Nazungumzia elimu inayoweza kusaidia kuonyesha uhusiano kati ya uduni wa maisha ya wananchi na mabilioni ya fedha yanayochukuliwa kwa njia ya mikataba feki au katili. Uhusiano kati ya ukosefu wa elimu na wizi wa mali ya umma. Uhusiano kati ya kushamiri kwa ghafla kwa biashara mbalimbali, ikiwa pamoja na biashara ya madawa ya kulevya (mihadarati), na fedha haramu ambazo hazitoki kwenye mzunguko halali na wa kawaida wa fedha katika nchi. Ulitaka kuuliza iwapo hatua hizi zitamaliza rushwa? Sizungumzii kumaliza. Nazungumzia kuzuia na kupunguza. Hatua hizi zitakuwa zimepunguza rushwa kwa kiasi kikubwa na zimejenga msingi mkubwa wa kuchukia na kupambana na rushwa.

Swali: Kuna madai ya kupokea rushwa katika mikataba mingi nchini. Mbona hujajiuzulu ubunge kwa tuhuma hizo?

Jibu: Sijaona popote ambako Bunge, kwa ujumla wake limehusika katika kupitisha mikataba yenye rushwa ndani yake. Hakuna tuhuma dhidi ya Bunge. Bali kuna matakwa ya wabunge na Kamati za Bunge ya kutaka kujua undani wa mikataba iliyoingiwa na serikali. Haya ni matakwa sahihi.

Swali: Ikitokea zikaletwa tuhuma kwamba Bunge zima limehongwa ili lipitishe muswada au mkataba fulani, utajiuzulu ubunge ili kulinda uadilifu wako binafsi? Je, hiyo itakuwa imemsaidia nani?

Jibu: Labda nianze na hilo la pili, kwamba nikijiuzulu nitakuwa nimemsaidia nani. Na mimi nauliza: Je, nikibaki mbunge na kushiriki ufisadi, nitakuwa namsaidia nani? Hakuna ninayemsaidia. Ninanyonga kila mtu; kila mwananchi.
Lakini hebu turudi kwenye swali la msingi. Siyo rahisi kuhonga Bunge zima. Ni rahisi kuhonga watu wachache ambao watatumia nafasi zao kushawishi wabunge wengine, na bila kuwaambia ukweli wote kuhusu mradi wa ufisadi. Nasubiri kupinga hilo kama litatokea, na kama nitapata taarifa. Mimi siyo mtu wa kutumika hivihivi. Unafahamu ndugu yangu, hatua zozote ambazo mbunge atatumia, ikiwa ni pamoja na kujiuzulu, ni nyenzo tu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi, watawala na dunia nzima. Ni ushahidi wa kukataa kuwa sehemu ya ufisadi. Sasa ngoja niseme: Nasema nikigundua kuna ufisadi, nitajiuzulu. Na hii haitakuwa kwa uadilifu wa binafsi, bali kwa uadilifu wa wote wasiotaka rushwa; wasioamini katika rushwa na wanaopinga ufisadi. Kitu muhimu hapa ni kutambua kuwa Bunge ni chombo cha wananchi cha uwakilishi. Kina nafasi yake kama nguzo mojawapo ya dola. Kina hadhi yake inayotokana na ridhaa ya wananchi waliotupeleka humo. Hivyo ni sahihi kabisa kulinda hadhi yake ili kiendelee kuheshimika na kufanya kazi zake. Kwa hiyo ninapojiuzulu, kama nilivyofanya, kutoka kwenye Kamati, nimelinda haki za bunge. Nimelinda hadhi na heshima yake. Nilifanya hivyo, pamoja na sababu nilizotaja hapo awali, ili kuendelea kulipa Bunge heshima linayostahili.

Swali: Kuna taarifa kwamba madai ya Mbunge Adam Kighoma Malima hayakuwa na hadhi ya kusikilizwa na Bunge bali mahakama; maana anadai kukashifiwa. Hilo mliliona kabla hujajiuzulu?

Jibu: Sasa hayo ni mambo ya kumuuliza Spika, Mheshimiwa Samuel Sitta. Siyo mimi. Au jaribu kwa wajumbe wengine. Ninachojua ni kwamba kuna utaratibu wa kufanya kazi katika Kamati, na mwisho wa kazi kila kitu kitawekwa wazi. Bali kunapotokea kikwazo cha kufanya kazi mliyopewa, ndipo unashughulikia kikwazo; kama nilivyofanya.

Swali: Lakini mimi najua kwamba Kamati haina uwezo wa kushughulikia kashfa na kama waliita wataalam wa kuwasaidia watakuwa waliwaambia hilo.

Jibu: Kama unajua hivyo, basi unajua hivyo. Mimi siwezi kukuzuia kujua unavyojua.

Swali: Lakini unakubaliana nami kuwa hivyo ndivyo ilivyo?
Jibu: Kwa nini unataka nikubaliane na wewe?

Swali: Nataka kujua kama umenielewa na unakubaliana nami au una uelewa tofauti. Hili ni suala la kisheria na wewe ni mtunga sheria.

Jibu: Nakumbuka ulipotaka kunihoji uliniambia kwamba utashughulikia suala la kujiuzulu kwangu kutoka kwenye Kamati. Na katika kujiuzulu kwangu hakuna popote ninapojadili mambo ya ndani ya Kamati. Nadhani hilo swali siyo mahali pake hapa. Hata hivyo nina mawazo binafsi juu ya mambo mengi, siyo hilo peke yake.

Swali: Kamati haikuwaita Waziri Mkuu Edward Lowassa wala Reginald Mengi, watu muhimu katika madai yako…

Jibu: Siyo hivyo. Kamati haikuzingatia maelezo yangu kuhusu madai ya rushwa. Haikuyashughulikia. Ingeyashughulikia, lazima watu hao wawili wangehojiwa; popote pale walipo.

Swali: Unataka kusema, kwa kufanya hivyo, Kamati haikulinda hadhi ya Bunge?

Jibu: Nasema haikulishughulikia. Wewe na yeyote yule, mnaweza kujazia hapo. Kama haikulishughulikia, basi ilifanyaje?

Swali: Haikulinda hadhi ya bunge.

Jibu: Huyo ni wewe. Muulize na mwingine. Mimi sina hukumu kwa yeyote. Nasema baada ya tuhuma kwamba wabunge wamehongwa, dhamira yangu iliniongoza katika kutaarifu wenzangu; na kulipokuwa na kusita, nikajiondoa kwenye Kamati. Basi.

Swali: Ili watu waweze kuchukia na kupinga rushwa, wanahitaji taarifa. Wanahitaji kujua serikali inafanya nini na wapi; imefanyaje hayo inayoyafanya. Kama serikali haikubali kutoa taarifa, je, wananchi watawezaje kupinga rushwa?

Jibu: Hilo siyo katika rushwa peke yake. Ni katika mwenendo mzima wa serikali na idara zake. Wananchi wanahitaji kujua serikali inafanya nini. Wananchi wanapaswa kuwa wasimamizi wa serikali yao kupitia bunge na asasi za kijamii. Kama wananchi watakuwa hawapati taarifa kamili na sahihi juu ya utendaji wa serikali, basi hawawezi kuisimamia, kama vile ambavyo hawawezi kuiwajibisha.
Suala la kupatikana kwa taarifa za utendaji wa serikali ni muhimu sana. Bila taarifa huwezi kuhoji; huwezi kupendekeza; huwezi kukataa kitu bila kukielewa; huwezi kuunga mkono chochote. Sharti upate taarifa. Hivi sasa kuna sauti nyingi juu ya mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari. Nadhani kilio chao ni hicho. Wanataka vyombo vya habari na wananchi wapate taarifa ili waweze kuisimamia vizuri serikali. Kinyume cha hayo hawatakuwa na mchango wowote katika usimamizi. Lakini hili linahusu rushwa pia. Bila taarifa juu ya mapato ya serikali na juu ya mifumo ya bajeti na matumizi ya serikali, rushwa itakaa pembeni ikichekelea kwa kuwa wengi hawajui kinachotendeka. Iwapo wananchi, ambao ni wasimamizi wakuu wa serikali yao, watabaki gizani, juu ya sera na mipango ya serikali katika maeneo yote, basi hawataweza kuihoji serikali. Hawataisimamia. Lakini vilevile hawataweza kuipongeza kwa kazi nzuri hapa na pale, kwa kuwa hawana taarifa. Nakubaliana nawe kwamba serikali inapaswa kuweka wazi taarifa zake. Bila uwazi rushwa itaota mizizi. Ukosefu wa taarifa juu ya mwenendo wa serikali na watendaji wake; na ukosefu wa taarifa juu ya mikataba kati ya serikali na makampuni na mashirika ya ndani na nje, huchochea rushwa kwa kiwango kikubwa. Rushwa hufanyika gizani, kwenye uficho, pembeni. Hata kama itakuja kujulikana baadaye, wahusika hukutana na kupeana gizani. Kwa hiyo, kama hakuna uwazi juu ya mikataba, juu ya mapato ya serikali kutokana na madini, vito vingine vya thamani na maliasili za nchi, basi hesabu za mapato hazitafahamika kwa wananchi. Hapo ndipo rushwa itaota mizizi.

Swali: Uliwahi kupewa adhabu na Bunge kwa kile kilichoitwa “kushindwa kuthibitisha kauli” zako bungeni. Leo, baada ya kujiuzulu kutoka kwenye Kamati, kuna walioanza kukushutumu kwa kile wanachoita “kuingiza siasa” bungeni. Unahusishaje matukio haya mawili?

Jibu: Sikiliza bwana. Haya mawili hayana uhusiano bali yote yamenikuta Ndesamburo. Lile la Bunge la 2000-2005 nililithibitisha. Sema hawakukubaliana nami. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alihutubia mikutano mjini Moshi na kuwaambia wafanyabishara, kweupe kabisa, kwamba anayetaka kufanikiwa katika bishara yake, sharti apeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hili nililithibitisha kwa kadri ya uwezo wangu; useme tu kwamba kuna waliokuwa wamelenga kumlinda Waziri Mkuu. Sasa hili la kujiuzulu kutoka Kamati, kwanza sijui kwa nini unalirudiarudia. Lakini ni hivi: Kwanza, kudai kwamba ninapeleka siasa bungeni, ni kupotoka. Tuko pale bungeni kutokana na utaratibu wa kisiasa. Tumetokana na vyama vya siasa na mfumo maalum wa siasa. Pili, kazi tunayofanya ni ya kisiasa. Ni siasa ambazo zinaelekeza utawala wa nchi. Ni kukwama kwa siasa ambako kutaliangamiza taifa hili. Sheria zinazotungwa sharti zielekezwe na zijibu hoja kuu ya siasa za nchi. Sasa kusema kwamba Ndesamburo anapeleka siasa bungeni, ama ni kutaka kupotosha watu au ni kutojua kwamba bungeni ndiko hasa mahali pa siasa.
Bali suala la kujiondoa kwenye Kamati halina huyu anatoka chama kipi. Ni suala la uadilifu. Mimi na wenzangu tumetuhumiwa kula rushwa. Mimi sikula rushwa. Sasa kwa nini nisionyeshe kwa vitendo kwamba sikuhongwa? Ni haki yangu.

Swali: Mwenyekiti wa Kamati, anasema ulishiriki zaidi ya asilimia 90 ya vikao, kwa hiyo maamuzi ya mwisho yanakuhusu pia. Unasemaje kuhusu hili?

Jibu: Sina sababu ya kuzozana na mwenyekiti wangu wa zamani. Anaelewa vema nilichosema kuhusu kutohusishwa. Namheshimu mwenyekiti na wajumbe wote. Bali nasema, lile hitimisho; yale maoni ya mwisho ya Kamati, na vyovyote yatakavyokuwa, ambayo yanakata shauri lililokuwa mbele ya Kamati, hakika sikushiriki na sitaki kuhusishwa.

Swali: Kama hivyo ndivyo, kwa nini hukujiuzulu mapema?

Jibu: Hapo ndipo wengine hawataki kuelewa. Nadhani ni makusudi. Na mimi nawauliza: Ni lini nilipata taarifa za wabunge kuhongwa? Unachukua hatua pale unapokuwa umepata taarifa. Kama hukupata taarifa, utachukuaje hatua? Utaendelea kama kawaida. Ukipata taarifa, unatumia taarifa hiyo. Taarifa inaweza kugeuza kabisa mkondo wa fikra na utendaji. Nilichukua hatua pale nilipoambiwa kwamba kuna madai kuwa wabunge wamepokea rushwa. Ningezipata mapema nisingeingia hata kikao cha kwanza. Basi.

Swali: Katika hali zote mbili: kuadhibiwa na Bunge na kujiuzulu; ni mambo yanayoonyesha umekuwa katika misokosuko. Je, unajisikiaje kuwa katika misukosuko ya aina hiyo?

Jibu: Sioni kama ni misukosuko. Naona ni changamoto. Hakuna kinachofanywa kwa maigizo. Kila tukio linakuja kwa njia yake na wakati wake. Nami nayakabili kwa kadri yanavyojitokeza.

Swali: Unadhani kuna wabunge wa CCM ndani na nje ya Kamati yako ya zamani ambao wanakuunga mkono katika hili la kujiondoa kwenye Kamati?

Jibu: Hiyo siyo hoja. Hoja ni kutenda kwa kuamini kwamba unachofanya ni kweli na sahihi. Kwamba unadhihirisha uadilifu wako; kile kilichoko moyoni mwako bila kujali nani anakuunga mkono. Bali naweza kusema kwa uhakika, kwamba kila mwenye nia njema na mwadilifu, ndani au nje ya Bunge, atakuwa anaunga mkono hatua niliyochukua. Je, wewe huungi mkono?

No comments

Powered by Blogger.