Header Ads

LightBlog

SERIKALI IONJESHWE UANDISHI WENYEWE

WAANDISHI WA HABARI WASIOHITIMU

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI waandishi wa habari wafundishwe jinsi ya kuandika habari kwa muda wote wa maisha yao. Ifike mahali wajue kuandika na waanze kuwafundisha wenzao wanaoingia katika kazi hii.

Kasheshe iliyozuka wiki hii kati ya ikulu na gazeti la Mwananchi inatokana na kutokomaa kwa waandishi katika taaluma yao. Hili linawahusu waandishi walioko kwenye magazeti, redio, televisheni, mashirika ya umma, makampuni binafsi na hata ikulu.

Mwananchi waliandika kichwa cha habari (3 Machi 2008), “Kikwete ajitosa sakata la umeme.” Maelezo yakasema Kikwete amesema Sheria ya Manunuzi ya Umma “isiwe kikwazo” katika miradi mikubwa ya umeme.

Gazeti likaongeza kuwa hilo limetokea wakati “suala la ununuzi wa mitambo ya ufuaji umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited limekuwa gumzo kubwa.”

Kesho yake, Mkurugenzi wa mawasiliano ikulu, Salva Rweyemamu akasema gazeti hilo limeonyesha “Rais Kikwete amejiingiza kwenye suala la ununuzi wa mitambo ya umeme ya Dowans.”

Kwa idhini yenu wasomaji, naomba turudi darasani. Tutumie vifungu sita vya taarifa ya ikulu (a, b, c, d, e na f). Shabaha iwe kuonyesha kwanza, jinsi ikulu isivyokuwa na sababu ya kulalamika; na pili jinsi Mwananchi lilivyowanyima wananchi uhondo wote katika taarifa ya ikulu.

Kifungu (a): “Kwamba sekta ya madini isimamiwe kikamilifu kwa kuhakikisha kuwa wenye leseni za kutafuta na kuchimba mafuta wanazitumia kwa masharti yaliyoombewa na kuwa wasiozitumia leseni hizo kwa kuzingatia masharti ya leseni hizo wanyang’anywe leseni hizo badala ya kuzitumia kuendesha ulanguzi tu.”

Kumbe gazeti lingeandika kwamba mkutano wa tathmini ya utendaji wa serikali umegundua kuwa:
(i) Sekta ya madini haisimamiwi kikamilifu
(ii) Wenye leseni za kutafuta na kuchimba madini wanazitumia kuendesha ulanguzi tu.

Ujumla wa yote haya ni kwamba waziri muhusika na watendaji hawafanyi kazi yao na kwa hiyo hawastahili kuwepo. Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kifungu (b): “Kwamba zichukuliwe hatua za haraka kukomesha kabisa wizi wa mafuta ya transfoma ambao umesababisha hasara kubwa kwa taifa na kuvuruga mtandao wa kusambaza umeme kwa wananchi.”

Kumbe gazeti lingeandika kuwa tathmini ya utendaji wa serikali imegundua kuwa:
(i) Wizara na polisi wameshindwa kudhibiti wizi wa mafuta ya transfoma, tena kwa muda mrefu
(ii) Uzembe huo umesababishia hasara kubwa kwa taifa (hapa wangetafuta takwimu)
(iii) Uzembe huo au kutotenda kumevuruga mtandao wa kusambaza umeme nchini nzima.

Ujumla wa yote haya ni kwamba waziri muhusika na watendaji hawafanyi kazi yao na kwa hiyo hawastahili kuwa kwenye nafasi hizo. Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kifungu (c): “Kwamba Kamishna wa Madini Nchini, kwa kutumia madaraka na mamlaka yake kisheria, achukue hatua mara moja kukomesha uchimbaji wa kokoto katika maeneo yasiyostahili, na hasa katika eneo la Kunduchi/Tegeta, Dar es Salaam ambako serikali ilikwishakupiga marufuku uchimbaji wa kokoto, lakini baadhi ya wachimbaji wamerudi katika eneo hilo kuendesha uchimbaji.”

Kumbe gazeti lingeandika kuwa tathmini ya utendaji wa serikali imegundua kuwa:
(i) Kamishna wa Madini hajui au ameshindwa kutumia madaraka yake kisheria na hivyo ameshindwa kazi
(ii) Amri ya serikali haina uzito au inapuuzwa katika eneo la kuchimba kokoto la Kunduchi/Tegeta
(iii) Au amri inapindwa na baadhi ya watendaji serikalini kwa manufaa binafsi.
Ujumla wa yote haya ni kwamba watendaji wizarani wameshindwa kazi, kwa hiyo waondolewe; au serikali imekosa nguvu, hivyo iweje? Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kifungu (d): “Kwamba ziongezwe juhudi katika uzalishaji wa umeme nchini kwa sababu programu ya taifa ya uzalishaji umeme bado iko nyuma na liko pengo kubwa kati ya mahitaji halisi ya umeme nchini na umeme unaozalishwa kwa sasa.”

Kumbe gazeti lingeandika kuwa tathmini ya utendaji wa serikali imegundua kuwa:
(i) Watawala hawakuwa na taarifa, hadi wiki hii, kuwa programu ya taifa ya uzalishaji umeme bado iko nyuma
(ii) Wizara na serikali kwa ujumla haikujua, hadi leo, kuwa kuna pengo kubwa kati ya mahitaji halisi ya umeme na umeme unaozalishwa
(iii) Wahusika katika kufanya utafiti/kutoa taarifa watakuwa wamezembea.

Ujumla wa yote haya ni kwamba watawala na watendaji, kwa miaka yote, wanafanya wasichojua; kwamba hawastahili kuwa madarakani. Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kifungu (e): “Kwamba dhana ya tenda na Sheria ya Manunuzi isiruhusiwe kuwa kikwazo katika miradi mikubwa mikubwa ya miundombinu ya nishati hasa ile ambako wawekezaji wamejitokeza katika maeneo ambako taifa linahitaji uwekezaji mkubwa na wa haraka na ambako nchi inaonekana ilichelewa kuwekeza.”

Kumbe gazeti lingeandika kuwa tathmini ya utendaji wa serikali imegundua kuwa:
(i) Serikali imedhamiria kuvunja sheria za nchi kwa maslahi ya wawekezaji
(ii) Utaratibu mzima wa kuitisha tenda sasa ni upuuzi mtupu pale wawekezaji watakapokuwa wamejitokeza
(iii) Sasa ni mwendo holela kwa wawekezaji – wakiishajitokeza na kuwa nchini, basi sheria ya manunuzi iende likizo
(iv) Nchi sasa itavamiwa na kuwa “uwanja wa fujo”

Ujumla wa yote haya ni kwamba Sheria ya Manunuzi ya Umma haina maana tena na kwamba kitakachotumika ni “ujanja kuwahi” kwa upande wa wenye miradi mikubwa na hasa ya umeme. Aidha, huu waweza kuwa mwanzo wa “uwanja wa fujo” katika kila sekta ya uwekezaji. Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kifungu (e): “Kwamba kasi iongezwe katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoahidiwa umeme yanapatiwa umeme bila ucheleweshaji usiokuwa na sababu.”

Kumbe gazeti lingeandika kuwa tathmini ya utendaji wa serikali imegundua kuwa:
(i) Wizara husika imeshindwa kwenda kwa kasi inayohitajika katika kusambaza umeme
(ii) Maeneo yaliyoahidiwa umeme yanacheleweshwa kupata umeme
(iii) Hakuna sababu zozote za msingi za kuchelewesha usambazaji umeme.

Ujumla wa yote haya ni kwamba uzembe umekithiri; waliopewa madaraka wameshindwa kazi na kwamba wakati ukifika serikali itaumbuka kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake. Rais aliyekuwa kwenye kikao ni shahidi.

Kwa usahihi zaidi, gazeti lingeandika kuwa wajumbe wa mkutano wa tathmini, walijiumbua mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwa kujadili mambo ambayo walipaswa kuwa wameyafanya.

Au, rais atakuwa alishangazwa sana na kauli za wajumbe katika kikao cha kujadili utekelezaji katika Wizara ya Nishati na Madini ambako imedhihirika, kwa mujibu wa taarifa ya ikulu, “karibu hakuna kinachoendelea.”

Huo ndio ungekuwa uandishi wa kuhitimu. Hata kama gazeti lingekabwa koo, kungekuwa na sababu kuwa limefikisha ujumbe kwa wananchi. Kwamba siri ya uzembe ndani ya ofisi za serikali, sasa imefichuka.

Huu ndio uandishi wa aina ya “uchambuzi fafanuzi,” ambao ni muhimu sana katika vyombo vya habari ambavyo vinatumikia wananchi katika kada zao nyingi.

Walichofanya Mwananchi ni kuripoti moja kwa moja kilichosemwa kwa kuongeza kidogo tu, mazingira ambamo hayo yametendeka. Halijakosea. Hata hivyo, hii haitoshi kukomea ambapo gazeti hilo lilikomea – kwa gharama yoyote ile.

Nenda mbele. Nenda ndani zaidi. Chukua mifano ya fafanuzi zilizowekwa kwa kila kipengee cha ikulu. Ikulu na serikali kwa ujumla, watazoea. Wataheshimu. Watavumilia. Tuwazoeshe wao na waandishi wao. Tuhitimu nao. Inawezekana.

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 8 Machi 2009)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

1 comment

Reggy's said...

mheshimiwa nimesoma makala yako kwa umakini mkubwa na kubaini kuwa kilichomchukiza salva Rweyemamu hakikuwa cha kina, na wala hakuwa na sababu ya kuchukia...natarajia aitishe press conference nyingine aibwatukie safu ya sitaki...au labda ameridhika na uandishi

Powered by Blogger.