Header Ads

LightBlog

SERIKALI INAPODHALILISHA WANANCHI



Serikali na bakuli la ombaomba

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kumkatisha tamaa Waziri wa Muungano, Muhammed Seif Khatib katika utekelezaji wa mradi wake wa kuomba fedha kwa ajili ya sherehe za miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Waziri amenukuliwa na waandishi wa habari akisema serikali itaomba michango kutoka taasisi na makampuni binafsi nchini kwa ajili ya maandalizi na sherehe za Muungano hapo 24 Aprili 2009.

Serikali haina fedha. Haina fedha za maandalizi ya sherehe na sherehe zenyewe. Siyo vibaya hata kidogo kwa serikali kusema ukweli, kama huo ni ukweli, kwamba haina fedha. Lakini hii inaleta tafsiri gani, hasa pale waziri anaposema kwa ufupi tu kwamba hakuna fedha na kwamba wataomba ufadhili?

Kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais, ambako kuna wizara hii, suala la sherehe za kitaifa zilizoko chini yake haliingizwi kwenye bajeti ya wizara? Kwamba fedha zilitengwa lakini zikaibwa? Kwamba zilikuwepo lakini zimeingizwa katika matumizi mengine? Kwamba mwaka huu wamenyimwa fungu?

Inawezekana wizara huwa haina bajeti kwa sherehe hizi, lakini wakati ukifika huwa wanakwangua kutoka kasma mbalimbali. Hapo wizara inakuwa kama “kabwela sina kitanda,” au siku hizi “wasera” wasiojua pa kula wala kulala. Jua likitunga wanaambizana, “Twende mshikaji, tutaambulia chochote hukohuko.”

Hili ni suala linalohitaji maelezo ya kina. Linasemwa kijuujuu tu kwa sababu watawala wamezoea kuomba. Ni kama walivyoomba wakati wa maandalizi na sherehe za miaka 45 ya Uhuru.

Twende pamoja, hatua kwa hatua. Serikali haichangishi fedha kwa ajili ya wenye njaa – huko Bunda, mkoani Mara, ambako njaa imejenga maghorofa; siyo kwa waliopatwa na maafa; wasio na karo ili waendelee na masomo; wasio na makazi ili wapate hifadhi; wasio na mavazi ili wajisetiri. Hapana!

Ni kwa ajili ya kutumbua tu siku ikifika na ndani ya majumba makubwa, meupe, ya zamani, ukingoni mwa Bahari. Ni michango kwa ajili ya mbwembwe na madoido ya watawala; kielelezo kwamba bado wapo; wanadunda katika ufalme wa kisiasa. Basi!
Serikali inapoomba michango ya fedha, kwa ajili ya sherehe, maana yake ni kukiri unyonge mbaya na unyonge wa kujitakia. Je, sherehe heziwezi kuahirishwa? Haziwezi kuachwa?

Hivi taifa haliwezi kufanya kumbukumbu bila sherehe? Kwanza na mara nyingi, si wananchi ambao hufanya sherehe. Wananchi huadhimisha; lakini watawala hufanya sherehe. Wananchi hutembea kwa miguu au hupanda mabasi hadi kwenye mikutano au maonyesho.

Wananchi hukaa juani na kusikiliza hotuba na kuona magwaride; hurudi nyumbani wakiwa hoi na vumbi likiwatimka mgongoni. Hakuna maji, hakuna soda wala “pole kwa uchovu.” Ni hiari katika kukoleza kumbukumbu. Ni maadhimisho ya kweli ya siku ya kitaifa, kama bado ina mantiki ya kizalendo.

Kwa wanaoadhimisha gharama ni nguvu zao. Laiti serikali ingekumbuka mapema kuwa kuna maadhimisho; ikatumia uongozi wa karibu na wananchi; ikawaandaa wananchi kwa taarifa mbalimbali katika serikali zao za karibu na kaya, tena bila kwenda mbali na bila michango ya fedha au chakula.

Hapa wangeadhimisha, wangekumbuka tarehe muhimu katika historia ya nchi yao; wangekumbushwa matukio na maana yake katika maisha yao na taifa.

Hao ni wananchi wanaoadhimisha. Kwa “wakubwa” ambao wanasherehekea: bila kula, kunywa na kusaza, basi patakuwa hapatoshi. Hivi ni lazima mvinyo ya watawala inunuiliwe kwa fedha za kuomba kutoka wafanyabiashara?

Nakumbuka simulizi ya dhifa ya kitaifa iliyovunja ndoa ya miaka 25. Bwana alirudi nyumbani na mwanamke mwingine; akiwa amelewa ndi, huku akitamba, “Utanambia nini wewe Mama Frank? Nimeshika mkono wa rais.”

Kwa hiyo michango ya Muungano, kama ilivyokuwa michango ya “Miaka 45 ya Uhuru,” itabaki michango ya kustarehesha watawala, waheshimiwa waalikwa na mingine kuishia itakakoishia!

Sasa aliyetoa michango atarajie nini? Anaweza kuwa amealikwa kula na kunywa na wakubwa. Basi? Je, yule ambaye hakualikwa na kwenye kapu alimimina mamilioni kadhaa, anatarajia nini? Ufadhili wake kwa serikali unalipwaje?

Katika mazingira ya Tanzania, na hata nchi nyingi ambako demokrasi bado haijashika mizizi na haki za wananchi huweza kuchezewa na hata kuporwa na watawala, ombi la serikali ni kama amri. Aliyeombwa hutarajiwa kutoa, ndiyo maana Khatib anasema wana uhakika watakaoombwa watatoa.

Lakini hii ni ndoa iliyofungwa hadharani – kati ya serikali na wafanyabiashara na taasisi zinazoichangia fedha. Mfanyabiashara siyo mfadhili wa kawaida. Anapenda nipe nikupe. Kama siyo leo, basi kesho au keshokutwa. Hoja ni: Anataka nini hasa?

Ufadhili kwa serikali unaweza kuzaa “mapenzi ya kudai upendeleo” kutoka kwa serikali pale aliyechanga atakapokuwa anahitaji mabavu ya serikali kumtetea.

Ni ufadhili wa aina hii ambao huzaa tabia ya kukiuka misingi na taratibu kwa kutarajia kulindwa na serikali. Ufadhili wa viwango hivi kwa serikali hufanya baadhi ya wanaotoa fedha kuwa na jeuri na kiburi huku wakiizoesha serikali tabia ya kuomba.

Michango ya wafanyabiashara, kwa ajili ya sherehe, na siyo wakati wa dharura na majanga, huweza kudhoofisha serikali kwa matajiri wa kweli, na hata wezi, kujiona ndio wanatawala badala ya walioingia madarakani kwa ridhaa ya wananchi.

Aidha, ombaomba ya serikali hujenga mazingira ya baadhi ya watendaji kujipakulia kiasi wanachotaka kutokana na kutokuwepo uwajibikaji wa kweli katika kukusanya, kuamua matumizi na kutumia.

Matumizi ya serikali sharti yatokane na bajeti ya nchi. Bajeti ni sheria kuu ya mapato na matumizi inayotungwa na Bunge kila mwaka. Matumizi ya nyongeza ya serikali sharti pia yaamuliwe na wawakilishi wa wananchi ambao ni watunga sheria kwa kupitia bungeni.

Hizi fedha za pembeni, za sherehe za uhuru na muungano au sherehe nyingine, zinaweka watendaji serikalini na wanasiasa katika majaribu na kuwazamisha katika ulafi usiomithilika.

Na serikali inapochangisha fedha kwa ajili ya sherehe, licha ya kuvunja sheria ya mapato na matumizi ya kila mwaka, inakuwa imejisalimisha kwa wanaochanga, tena bila sababu.

Michango kwa ajili ya sherehe na utumbiaji, inamomonyoa hadhi ya serikali na kudhalilisha ridhaa ya wananchi walioiweka madarakani.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 22 Februari 2009 chini ya safu ya SITAKI)

No comments

Powered by Blogger.