Header Ads

LightBlog

CCM NA WANASIASA WAKE WASIOKOMAA



Sheria inayofunga rais, wabunge

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake wajidai kuwa wamekomaa katika siasa. Kumbe wingi wa miaka; nasema umri, siyo hoja!

Kitendo cha kupeleka muswada bungeni; kuzuia rais, mbunge, diwani na hata mwenyekiti wa kijiji, kuhama chama chake na hapohapo kubakia na nafasi yake ya kuchaguliwa, ni tusi kwa umri wa serikali na chama.

Juzi, Ijumaa, bunge lilipitisha Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo pamoja na mambo mengine, yanaendeleza utaratibu mbovu kuwa aliyehama chama chake basi anapoteza hata nafasi yake ya urais, ubunge au udiwani.

Kwamba rais akiona wenzake katika chama chake “hawaendi,” basi awaachie nchi; akae pembeni na wao waendelee na kuuza hata nyasi, ardhi na anga, wakati yeye alipewa dhamana na wananchi!

Kwamba mbunge, aliyechaguliwa na wananchi, akiona chama chake kimeboronga; hakina mwelekeo na hakimsikilizi; basi akihama apoteze ubunge wake.

Vivyo hivyo kwa diwani na mwenyekiti wa kijiji. Kwa mujibu wa muswada uliopitishwa juzi, na kama ilivyokuwa awali, anayehama anapoteza nafasi yake. Huku ndiko kutokua.

Kipengele hiki cha muswada kilichoshabikiwa na wabunge wengi wa CCM, ni mahabusi kwa wabunge haohao. Asitokee mtu akasema wote waliomo ndani ya chama hicho wanakubaliana na mambo yanavyokwenda.

Hiki ni moja ya vipengele vingi vya sheria ambavyo ni katili; vinavyoziba mifereji ya fikra na vinavyomweka mtu utumwani; hasa yule anayekiri, “bora mkono kinywani.”

Ukikaa na baadhi ya wabunge wa CCM utasikia wakisema, “Bingu Wamutharika ni kiboko. Anahama chama chake na kuunda kingine na kuendelea na urais.”

Bingu wa Mutharika ni Rais wa Malawi. Alikaa. Akaona chama chake kimetekwa na walafi na kwa kauali yake mwenyewe, aliona kimetekwa na wala rushwa. Akatafakari. Akaamua. Akaunda chama nje ya chama. Akahama cha awali. Akaingia kipya. Akaendelea kuhudumua wananchi wake kama rais.

Chama ni moja ya ngazi za kuingilia uongozi. Ngazi haikai hewani. Inasimikwa kwenye ardhi na kuegeshwa kwenye ukuta au mgamba ili muhusika apandie.

Kwa mantiki hii, ardhi, ukuta na mgamba ndio wananchi kwa wingi wao. Ndio umma. Ngazi ni chombo tu cha kufikia kule ambako wananchi wanataka uwe. Ngazi basi, ambayo ni chama, haina amri kwa ardhi, ukuta wala mgamba.

Hii ina maana kwamba ngazi ikichakaa, unaitupa na kutumia nyingine iliyopo; kama haipo, basi unatengeneza nyingine. Uwezo wa kuunda ngazi mpya daima uko mikononi mwa wananchi.

Wananchi hawatumikii ngazi. Rais hatumikii ngazi. Mbunge, diwani na mwenyekiti wa kijiji hawatumikii ngazi. Wanapaswa kutumikia wananchi ambao ndio chimbuko la mamlaka.

Je, kama rais ameona, kama alivyoona Bingu wa Mutharika, kuwa hatawatumikia wananchi vema kupitia chama alimopitia kupata urais, kwa nini asiasi na kujiunga na wenye mwelekeo wa utumishi? Vivyo hivyo kwa wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji.

Hoja za wabunge wa CCM zilikuwa kwamba unapotafuta ubunge “unatumia sera za chama,” hivyo ukitoka kwenye chama hicho kwenda kutekeleza sera ya chama kingine, unakuwa umeasi. Kwa hiyo, wakaamua, vi vema wabaki kifungoni.

Kikubwa ni nini: wananchi au sera? Na sera zenyewe ziko wapi? Nchi hii ina mkanganyiko mikubwa. Changamoto zinaitwa matatizo na taratibu na mipango ya serikali yoyote ile inayotoza kodi vinaitwa “sera.”

Vyama vingine vimeingizwa kwenye ukasuku huu na malumbano juu ya “sera yetu kuhusu barabara, kilimo, elimu” hadi neno lenyewe limepoteza maana kwani linatumika zaidi kwa ushabiki kuliko maana na mantiki halisi.

Utaratibu wa kuzuia wabunge na wachaguliwa wengine kuhama na kujiunga na upinzani au walioko upinzani kujiunga na walioko madarakani unaweza kulindwa kwa nguvu ya vyama vyenyewe; hasa kuhusu misimamo yake juu ya mambo muhimu yanayohusu haki na maendeleo ya wananchi.

Chukua mfano huu. Kwa nini akina Dk. Willibrod Slaa hawatamani kurudi CCM? Jibu: Kwa kuwa huko waliko sasa, wako huru zaidi kuliko walivyokuwa wakifikiri. Jibu: Kwa kuwa wanajiona, na ndivyo ilivyo, kuwa karibu zaidi na wanaowatumikia – wananchi.

Wanafikiri bila mipaka. Wanafikiwa zaidi na wananchi. Wanapelekewa mambo mengi na wale wenye uchungu na nchi hii. Wanakuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi na hawajafungwa midomo wala akili.

Asitokee mtu akasema wachungu kama akina Dk. Slaa hawapo ndani ya CCM. Hapana. Wamo, na huenda wengi. Lakini wako mahabusi. Ni mateka walioswekwa mahabusi. Wamebakia kuwa mashabiki wa wengine pindi mjadala unapoisha.

Mchango wa wabunge wa upinzani umekuwa wa maana sana kwa jamii hata kama unatoka upande wenye wabunge wachache. Kwa hiyo kufunga wabunge makini na hata mashabiki kutoka CCM kujiunga na upinzani, ni kuziba mifereji ya fikra.

Tena kufanya hivyo kwa kutumia Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ni kuingilia utashi wa kisiasa, lakini pia na muhimu zaidi, ni kuingilia uhuru wa kuchagua na kujiunga na wengine kwa shabaha maalum ya manufaa ya nchi.

Hatua hii yaweza kuchochea maasi ndani ya CCM. Wale wanaosema, “Bora kushiba ukiwa kifungoni kuliko kuwa na njaa ukiwa huru,” wakapingana na wale wanaosema “Bora uhuru katika umasikini kuliko shibe katika utumwa.” Matokeo yake yaweza kutabirika.

Sheria zimeshindwa pale utashi mkuu uliposimama upande wa haki ambao ndio upande wananchi. Kauli ang’avu inasema hivi: “Wananchi wanataka maendeleo ambayo ni kuondokana na ufukara, kuishi kwa amani na kuwa na uhuru na utashi wa kuamua juu ya mambo yanayowahusu.” Sheria hii inapingana na uhuru huo.

Bali kwa waliodhamiria, sheria hii yaweza isiwe kikwazo. Wakati imelenga kufungia wabunge wa CCM inaweza kubomoa chama hicho. Vipi?

Wabunge wanaweza kuachana na ubunge. Wakaenda upande mwingine. Wakagombea na kushinda au kushindwa; lakini wakawa upande wa wanaoaminika kutetea wananchi. Hata rais aweza kufanya hivyo. Hatakuwa wa kwanza.

Huo ndio utakuwa mwisho wa visingizio dhalili vya sera ya chama.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 8 Februari 2009 chini ya safu ya SITAKI)

No comments

Powered by Blogger.