UVUNJAJI HAKI ZA BINADAMU UNAPOKITHIRI
Walimu wanapopigwa viboko
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI walimu wa shule za msingi Bukoba wawe kondoo wa kuswagwa na mkuu wa wilaya; tena kwa kiboko kwa madai kuwa mkuu huyo anawaadabisha.
Katika karne ya 21. Mwalimu. Mtu mzima. Mwajiriwa. Anatandikwa viboko. Kwenye viganja na makalioni. Halafu anatakiwa kuendelea kufundisha wanafunzi walioona au waliosimuliwa alivyocharazwa.
Taarifa za vyombo vya habari zinasema Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali, mapema wiki hii aliwachapa viboko walimu katika shule za msingi za Kansenene, Katelero na Kanazi. Baadhi vinamnukuu akikiri kijasiri kufanya hivyo.
Imeelezwa kuwa mkuu huyo wa wilaya amewapiga viboko walimu kwa kile alichoita uzembe na kushindwa kufundisha na hivyo kusababisha wilaya yake kuwa ya mwisho katika mkoa wa Kagera katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.
Tuseme hivi: Mkuu wa wilaya kakaa chini, kafikiria, kajiandaa, kaandaa polisi, kachonga fimbo, kajaza mafuta katika gari la serikali, kafunga safari kwenda shuleni, na kuamuru yule aliyemwita “polisi wangu” kuwapiga walimu.
Hili haliingii akilini. Kama Albert Mnali ametenda hilo, basi ajue hicho ni kitendo cha kale mno na cha kishenzi ambacho hakipaswi kutendwa na mtawala. Ni ukatili wa aina yake. Ni ulevi wa madaraka. Angekuwa na nafasi ya juu zaidi katika utawala angezua maafa na hata vita.
Chama cha Walimu nchini kinasema kinakusanya ushahidi juu ya suala hili. Waziri wa Elimu na Mafunzo anasema ameagiza mkuu wa mkoa wa Kagera kuandaa taarifa ili ipelekwe kwa Waziri Mkuu. Kauli hizi zinaashiria mstuko na kutoamini kilichofanyika.
Kama hilo limetendeka na unataka kuelewa vema uzito wa kosa hili, sharti ufuatane nami taratibu na kwa makini zaidi.
Mkuu wa wilaya ni kiongozi wa kisiasa. Ni mteule wa rais. Ni mwakilishi wa rais. Ukitaka, basi mwite “rais wa wilaya.” Kwa hiyo katika mazingira haya na leo, huyo ndiye “Rais Jakaya Kikwete” wa wilaya ya Bukoba.
Hautakuwa umekosea ukisema, kwamba rais amepiga walimu viboko mbele ya wanafunzi wao. Huo ndio usahihi. Kwamba rais ametumia askari polisi kucharaza walimu viboko. Kwamba rais ametumia gari na mafuta – vilivyonunuliwa kwa kodi za wananchi – kwenda kupiga walimu.
Kwamba rais amedhalilisha walimu; siyo tu waliopigwa bali hata wale ambao hawajapigwa lakini wanapigika na siku moja wanaweza kuinamishwa mbele ya watoto na kurandwa bakora makalioni.
Hili lisiposemwa hivyo halitaeleweka. Uzito wake hautaonekana. Rais, ambaye ni mkuu wa nchi nzima, hataelewa kuwa “tu-rais twake” tulioko ngazi za chini tunadhalilisha wananchi, walimu na kudhalilisha nafasi ya rais.
Rais wa nchi nzima asipoelezwa kuwa “tu-rais twake” tunavunja haki, kunyakua uhuru na kubaka demokrasi; tunavunja haki za binadamu na kudhalilisha wananchi; hataweza kuchukua hatua.
Rais wa nchi nzima asipojua kuwa “tu-rais twake” tunamchafulia kazi, mipango na hadhi yake, hawezi kuchukua hatua muwafaka ya ama kutuondoa, kutufukuza kazi au kutupeleka shule.
Hapana. Rais asipochukua hatua wananchi watasema hakuona au amepuuza upofu unaomzonga “rais” wake wa wilaya. Hiyo ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi nzima. Ni hatari kwa sababu tutawaelimisha walimu jinsi ya kupinga kupigwa. Jinsi ya kukataa kupigwa. Jinsi ya kujitetea pale watakapopigwa.
Ni vema ifahamike kuwa njia ya haraka ya watawala kuleta machafuko nchini ni kuanza kuwapiga walimu na wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba ameanza kwa walimu. Kesho kwa wazazi. Keshokutwa kwa wanafunzi. Nashindwa kufikiria wimbi la upinzani ambalo baada ya kumg’oa yeye, linaweza kuenea nchi nzima.
Linaweza kuenea nchi nzima – kupinga manyanyaso ya kisultani na kikoloni – ili kuutakasa utawala uliopo au kuutokomeza. Huyu, mkuu wa wilaya, ni adui wake mwenyewe na adui wa utawala wa Rais Kikwete.
Masikini mkuu wa wilaya! Hajui kuwa uongozi wake, na sasa yeye, ni sehemu ya tatizo la walimu, wanafunzi, wazazi na elimu. Hajui? Hapana. Anakataa kuelewa.
Mwanasiasa huyu. Mteule wa rais. Mwakilishi wa rais; tuseme “rais” wa wilaya; anafanana “Wasabato Masalia.”
Masalia wanataka kwenda kuhubiri imani zao nchi za nje. Wanaaga familia zao. Wanakutana uwanja wa ndege Dar es Salaam. Hawana fedha mfukoni. Hawana pasipoti. Hawana vibali vya kwenda waendako (visa). Hawana tiketi za ndege. Wanataka kwenda tu. Watarukaje?
“Rais” wa wilaya ya Bukoba aangalie shule zake. Anataka ushindi wa kumeremeta darasa la saba. Hajui walimu wamelala wapi. Wamekula nini. Wamelipwa lini mishahara yao. Wana matatizo gani ya binafsi na kijamii. Hajui. Hataki kujua. Anataka ushindi.
Huyu “rais” wa wilaya anajua walimu walioko katika shule hizo ni wa viwango gani? Wana vifaa gani vya kufundishia? Wana mahitaji gani? Anajua matatizo ya shule hizo? Lini alizitembelea au amekwenda kupiga walimu tu?
Hata kama shule hazina vifaa kwa maana ya vitabu vya kiada na ziada, chaki, maktaba na madawati; hata kama uwezo wa walimu ni mdogo; hata kama walimu wanachelewa kwenda madarasani; fimbo ya rais wa wilaya inaweza kurekebisha hayo?
Hata kama kupiga kungekuwa suluhisho, nani apige yupi na nani wa kupiga kwanza? Utawala ni chimbuko kuu la adha na udhalilishaji wa walimu nchini. Tusisahau mgomo wa walimu wa hivi majuzi tu wa kudai malipo na haki zao nyingine ambazo utawala umekuwa ukikalia kwa muda mrefu. Mkuu wa wilaya ni sehemu ya utawala huo.
Hata hivyo, katika maelezo ya kazi zake, hakuna mahali popote ambako mteule huyo wa rais anapewa jukumu la kupiga walimu au mtu yeyote. Kitendo cha kupiga walimu ni joto la binafsi. Ni masalia ya ujima.
Sasa imefahamika kwamba kwa muda mrefu mkuu wa wilaya amekuwa akitafuta kuacha kazi lakini alikuwa hajapata kisingizio.
Hii ni kweli kwa sababu, walimu wamegoma. Serikali haikuwapiga. Imelilia mahakama. Sasa huyu bwana mdogo, “mlinzi wa amani” wilayani, anapata wapi ujasiri na haki ya kupiga walimu?
Kitendo cha mkuu wa wilaya cha kupiga walimu kinastahili kueleweka kwa usahihi wake: Kwanza, kuwa ni kukiri kushindwa kazi. Pili, kuwa ni ombi rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, la kutaka amfukuze kazi.
Rais Kikwete tayari amesikia ombi la mteule wake. Lakini haitoshi kupoteza kazi. Afikishwe mahakamani.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili Toleo la 15 Februari 2009 katika safu ya SITAKI)
NB: Katika toleo hilo, maneno yaliyokuzwa - yaliyoko para ya mwisho kasoro moja, hayakuchapishwa. Aidha, kwenye para ya mwisho, gazeti liliongeza neno "Tunashukuru" ambalo halikuwa la mwandishi, haliwezi kutetewa na kwa jinsi lilivyotumika; na mwandishi analikana na kuliita abiria asiye na tiketi wala kiti katika ndege iliyojaa.
No comments
Post a Comment