SERIKALI INAPOLIA WANANCHI WAFANYEJE?
Serikali inayobubujikwa machozi
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI Waziri Mkuu Mizengo Pinda alie mara ya pili ndani au nje ya bunge. Akilia, hata kama kwa simanzi, ina maana serikali imelia. Serikali ikilia raia wafanye?
Pinda alitokwa machozi bungeni Alhamisi wakati akijibu hoja kwa nini alitoa amri ya kuua wanaoua albino, jambo ambalo linakiuka utawala wa kisheria na haki za binadamu. Aliomba radhi kwa kauli hiyo kwa wabunge na wananchi.
Lakini hoja ya kuua bado ingali mezani. Inahitaji maelezo marefu, muda mwingi wa kueleza, kuelekeza na wakati mwingine kukabiliana katika midahalo na wale wanaokataa kuelewa.
Inawezekana kati ya umati aliohutubia Pinda siku ya kutoa agizo, ni watu ishirini tu waliopata taarifa za kufuta agizo. Waliobaki waweza kuendelea kutekeleza kama alivyoagiza. Zinahitajika juhudi kubwa za utawala ngazi ya wilaya kupindua kile ambacho Pinda alipinda.
Hii ni kwa kuwa maagizo ya kijumla yaweza kuleta mauaji ya wenyewe kwa wenyewe. Bali tunajua mauaji yanayopendwa, yanayosimamiwa na kutekelezwa na dola. Haya hutokana na maamuzi ya mahakama, kwamba fulani kapatikana na hatia na anastahili kunyongwa hadi afe. Hiki siyo kifo cha kawaida.
Mauaji mengine, ni yale yatokanayo na vita vya kugombea madaraka na utajiri wa nchi; ukosefu wa chakula; magonjwa yanayotibika kama malaria, kipindupindu na kuhara ambayo ni mauaji yatokanayo na umasikini; yote haya yaweza kuwekwa chini ya muuaji mmoja: serikali. Hivi siyo vifo vya kawaida.
Ujinga, uzembe, kutojali, kusahau, kudharau na kupuuza, huleta maafa na vifo. Haya yakifanywa na walioko kwenye utawala ina maana ni watawala waliodhamini vifo. Hivi siyo vifo vya kawaida.
Mauaji mengine ni kama haya ya kuua albino na serikali kukaa kimya; au kububujikwa machozi na kuwa sehemu ya walalamikaji; au kushindwa kupata majibu na kuelekeza kuwa anayeua albino hastahili kuishi. Haya yatakuwa mauaji ya shelabela yaliyodhaminiwa na dola.
Katika nchi jirani, wanasiasa walipotaka kumaliza wapinzani wao, tena ndani ya chama kimoja, walipitisha haraka marekebisho ya sheria ya hifadhi za kitaifa na kuweka vipengele vinavyowapa walinzi wa hifadhi uwezo wa kufyatulia risasi “yeyote yule waliyeona ni jangili.”
Ilikuwa rahisi kwa wapinzani wa mwanasiasa mmoja, kumuua na kutupa mwili wake kwenye hifadhi na kisha kupiga kelele siku ya pili kwamba mwili wake uliokotwa kwenye mbuga ya wanyama.
Tume ya Uchunguzi itasema, “…Tume imebaini Mhe. Kasosi Lukuniwe aliuawa na askari wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Ondokeni, baada ya kutotii amri ya kusimama na badala yake kuanza kuwarushia risasi… Ndani ya gari lake walikuta meno kumi ya tembo na ngozi mbichi za twiga na chui…” Basi!
Wito wa kuua walioua albino, waweza kuzaa mauaji ya aina hiyo: Kwamba waliouawa walikuwa wakipanga kuua; walikuwa na picha ya albino; walikuwa wamebeba silaha wakielekea anakoishi albino; kwamba walisikika wakisema lazima wamuue leo; kwamba walitoka kwa mganga wakiapa kuwa watampata tu; kwamba inasadikika waliyemuua ndiye aliua albino jana.
Hapa watakufa wengi ambao hawajawahi kuua. Ndiyo maana sharti juhudi ifanywe ili ujumbe wa kufuta kauli ya Pinda ufike mbali. Katika hili, serikali ina uwezo wa kusambaza taarifa kama ilivyo na uwezo wa kukabiliana na mauaji.
Bali kuna haja ya kukumbushana, kwamba kuua kwa njia ya kutumia wananchi kuvamiana au kwa hukumu ya mahakama, siyo suluhisho. Majaji duniani, wakiwemo wa Tanzania, wamewahi kutamka hadharani kuwa wanapitisha hukumu ya kunyonga lakini hawakubaliani na mantiki yake.
Hapo ndipo unapatikana ujasiri wa kuuliza: Kama serikali ina sheria ya kuua aliyeua ina maana serikali inaua. Je, serikali ikiua nani ataiua?
Kuua ni kuondoa maisha. Kuondoa maisha siyo kutoa adhabu. Nia ya adhabu ni kufanya muhusika kujutia tendo lake; kuadhabika na kujirudi. Ukimuua hatakuwa amefanya adhabu. Hatajuta. Hatajirekebisha. Hii ni kwa kuwa hayupo.
Kuua aliyeua ni kufanya mauaji. Ni kutakasa tendo la kuondoa maisha ya watu. Badala ya kuwa funzo kuwa kuua ni kubaya, linakuwa funzo kuwa maisha hayana thamani. Thamani ya maisha inapatikana katika kulinda uhai wa aliyeua; kumpa adhabu ya kijamii na kumfanya ajutie tendo lake na kurekebika.
Kujutia tendo la kuua kuna mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya maisha kwa aliyeua. Kila anapoona tabasamu la ndugu zake wanaokwenda kumwona gerezani; na kila wanapomuaga wakimwacha akidondokwa chozi la upweke; ndani ya mtima wake kunajengeka thamani ya maisha yake binafsi, ya waliokuja kumwona na hata ya yule aliyemuua.
Kwa msingi huu, muuaji ni muuaji. Anayeua albino ni muuaji na anayeua muuaji wa albino ni muuaji; hata kama ni dola. Hoja hii inapata uzito zaidi pale mauaji yanapokuwa yameelekezwa na viongozi wa serikali au hukumu ya mahakama.
Uhai ni haki ya mtu. Haki hii haiombwi kwa serikali. Ni haki ya kuzaliwa nayo. Kinachofanyika ni kusihi na hata kushinikiza serikali kutunga katiba na sheria zinazolinda haki hii ya kuishi.
Haki ya kuishi ya mtu mmoja haipaswi kuondolewa na mtu mwingine, serikali au mamlaka yoyote ile. Kuwepo kwa serikali kuna maana pia ya kulinda haki ya kuishi ya kila raia. Kushindwa kulinda haki hii ni kushindwa kutawala.
Mkengeuko katika jamii na hatma ya kupatikana mtu anayeua mwenzake, hakuodoi wajibu wa serikali wa kulinda haki ya kuishi ya kila raia, pamoja na aliyefanya uhalifu uliothibitika kwa njia ya mahakama au yoyote ile.
Kwa hiyo, thamani ya maisha ya mtu haikomei pale anapofanya kosa. Inaendelea hadi anaporekebishwa kwa adhabu na hadi anapokumbana na kifo cha kawaida. Dunia imejaa mifano ya wahalifu waliogeuka kuwa wema; wangeuawa wema huo usingekuwa funzo leo.
Dunia imejaa pia mifano ya waliouawa kwa amri za watawala au hukumu za mahakama, lakini ikathibitika baadaye kuwa hawakuwa na hatia. Waliosababisha vifo hivyo huishi kwa kujuta hadi mwisho wa maisha yao.
Kuua kwa njia ya kunyonga au kwa kuagiza watu waue wenzao, kunaelekeza jamii katika kutothamini maisha, hivyo kujenga usugu wa “nitakuua ninyongwe, potelea mbali.”
Sheria zinazolinda mauaji zifutwe. Anayeagiza mauaji akome. Anayeua ni muuaji. Kuna tofauti gani kati ya “jambazi” linaloua na serikali inayonyonga? Tujadili.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii itachapishwa katika toleo la 1 Februari 2009 la Tanzania Daima Jumapili katika safu ya SITAKI)
1 comment
Heshima kwako Mzee Ndimara
Sina hakika na namna viongozi wetu wanavyojishirikisha katika kutafuta maamuzi ama kutafuta suluhisho la matatizo yetu. Na sina hakika kama akili nyingo huondoa maarifa ama maarifa mengi huondoa akili maana maamuzi mengi ya serikali hunifanya nijiulize kama kilichokosekana ni akili ama maarifa. Sina hakika na washauri wa viongozi (kama wanao) lakini mara nyingi tumeshuhudia kauli za ajabu toka kwa viongozi wa juu (na ukifuatilia tangu enzi za Sumaye, Lowassa na sasa Pinda) ofisi hiyo imekuwa na "kauli tata".
Nadhani kutakuwa na tatizo kubwa zaidi ya hili, na pia kupenda kutatua tatizo kwa njia mkato huchangia mawazo haya.
Yote juu ya yote ni kuwa Waziri Mkuu amekuwa na ujasiri wa kuomba msamaha na pengine amesamehewa. Lakini natumai hakuna watakaotekeleza aliyosema maana wengi wana hasira na alipipandikiza "chuki halali" juu ya wauaji wa albino basi kuna ambao hawataweza kuzitoa.
Post a Comment