Header Ads

LightBlog

UCHAGUZI MDOGO MBEYA VIJIJINI

Mhanga wa bundi Mbeya Vijijini

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI bundi wa Mbeya waendelee kukenua. Safu hii ilionya wiki iliyopita kwamba bundi wanachekelea mitini na kwamba kwa mazingira yaliyopo lolote laweza kutokea, hata kwa mashujaa wa Tarime.

Ndivyo ilivyokuwa. Mhanga wa kwanza wa mkenuo wa bundi amekuwa wakili Sambwee Shitambala, mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye hakufaulu mtihani mdogo wa kujaza fomu. Ametupwa nje.

Kenuo la kwanza la bundi limenufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aliyeonekana kuwa mpinzani mkuu wa chama tawala sasa ameondolewa kwenye ulingo.

Sasa mshindani wa maana aliyebakia, dhidi ya CCM, ni Chama cha Wananchi (CUF). Hebu tuliweke sawa. Mshindani pekee dhidi ya CCM sasa ni vyama vya upinzani. Labda tuliweke vizuri zaidi.

Mshindani pekee aliyesalia ni wananchi – wanachama wa vyama vya upinzani na wanachama wa CCM ambao wanataka mabadiliko; na mabadiliko ni kuwa na mbunge nje ya chama kilichoko ikulu.

Sasa bundi wa Mbeya Vijijini watamkenulia nani: CCM au CUF au wananchi wa vyama vyote ambao wanataka mabadiliko? Je, wakikenulia wananchi watakaa kwenye miti ya nani baada ya uchaguzi?

Kuenguliwa kwa Chadema kumefurahisha CCM kwa kiwango kikubwa na kufanya baadhi ya viongozi na wanachama kupata mdondoko. Kulikuwa na sherehe kubwa.

Ushirika wa CCM na CUF kwa upande mwingine, kujaribu kuziba Chadema umeotesha uhusiano usio wa kawaida. Hapa napo CUF walishindwa mbinu. Pingamizi moja lilitosha kufanya ukweli ubainike.

Ushirika wa CUF na CCM katika hili umeotesha nundu katika upinzani. Kwa maana nyingine, CCM wanachekelea kwamba tayari “wamevuruga wapinzani.”

Bali kwa upande mwingine, CCM wanasema waliyemwengua katika uchaguzi mkuu ndiye mgombea wa CUF na wanamfahamu. Hili lina sura mbili na manufaa tofauti kwa vyama viwili vilivyobakia.

Mgombea wa CUF aweza kudai kuwajua vizuri wana-CCM na chama chao na uongozi wa chama hicho nchini kwa ujumla. Nao CCM waweza kujitapa kuwa watamvua nguo mgombea huyo na kueleza kwa nini walimwacha mwaka 2005.

Kwa upande mwingine, kuna uwezekano wa bundi kukoleza zogo; kwamba kwa vile CUF walikuwa upande wa CCM katika kuweka pingamizi, basi Chadema hawatakuwa na utashi wa kushirikiana nao kuleta ushindi kwa upinzani.

Hilo likitokea, hata ile kazi kubwa iliyofanya CCM wapeleke “mchawi wa magoroi” – John Malecela kwenye uwanja wa mapamnano, itakuwa imepungua uzito. Lakini kwa vyovyote vile, hizi siyo hoja za kampeni. Ni vikolezo tu.

Hoja za uchaguzi Mbeya Vijijini ni kukosekana kwa mbolea au kupatikana kwa mbolea kwa kile wanachoita “vocha” lakini kwa bei ya juu ambayo wakulima hawawezi kumudu.

Hoja ni vile vinavyoitwa “shule za kata,” zilizoanzishwa kwa pupa kana kwamba kuna mashindano ya kuwa na “matundu” na siyo madarasa.

Michango kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi imefanya baadhi ya vijana wasio na kazi wala mapato ya maana vijijini kukimbia makazi yao; kwani wanawindwa kama swala na viongozi wa serikali za mitaa wanaotoka CCM.

Hoja ni makao makuu ya wilaya. Wakazi wa Mbeya Vijijini wanasema wanasumbuka kufunga safari ndefu kwenda makao makuu yao yaliyoko mjini Mbeya badala ya kuwa na makao makuu Mbalizi.

Wakazi wengi wa Mbeya Vijijini ambao ni Wasafa na Wamalila, wanadai barabara za kudumu, soko kwa mazao yao madogo ya mpunga, mahindi, ngano na ndizi; vilevile wanataka sauti katika uendeshaji wa shughuli zao tofauti na ilivyokuwa sasa kwa muda mrefu.

Ni wenyeji hao pamoja na wakazi wengine kutoka wilaya nyingine nchini ambao wanaishi Mbeya Vijijini walioahidiwa umeme na serikali kama njia ya “kumuenzi mbunge Richard Nyaulawa. Wanataka kuuona.

Hoja hizi pamoja na nyingine na vikolezo vya awali, ndivyo vinatarajiwa kwenye uwanja wa kampeni, lakini kwa kiwango kikubwa kutoka upande wa upinzani. Kama kawaida CCM itaendeleza kauli zake, “Ndiye baba, ndiye mama.”

Ukweli utabaki palepale; kwamba wananchi wanajua baba zao na mama zao; tena fika na wakati wote; siyo wakati wa uchaguzi.

Bali wakati CUF inajiandaa kukwaruzana na CCM, sharti Chadema watafute kilichowakwamisha – kupitiwa, jeuri, kutojua, kupotoshwa au kujua zaidi na waache kufanya majaribio ya kutengeneza oksijeni wakati yaliisha zamani na mabingwa kutuzwa.

Katikati ya yote hayo, Chadema sharti wafikirie jinsi ya kusimama na CUF kuleta ushindi kwa upinzani; au hata kupunguza kiwango cha ushindi na majigambo ya chama kikongwe.

Bado lolote laweza kutokea. Hakuna mshindi wa moja kwa moja hata kama bundi wataendelea kukenua. Au wananchi wapige “kura za maruhani” za Chadema? Hapana. Siyo wakati muwafaka.

(Makala hii itachapishwa katika Tanzania Daima Jumapili, 4 Januari 2009 katika safu ya SITAKI)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.