Header Ads

LightBlog

WAZIRI ANAPOKUWA MHANGA WA SHERIA CHAFU

Waziri Khatib ‘anavyotishiwa nyau’

Na ndimara Tegambwage

SITAKI mtu yeyote amzomee rafiki yangu Mohammed Seif Khatib, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia masuala ya Muungano na aliyewahi kuwa waziri wa habari, utamaduni na michezo.

Khatib ana kampuni. Inachapisha gazeti. Linaitwa Taifa Huru. Amelichapisha. Anataka kugawa nakala 2,000 za gazeti lake kwa viongozi na wananchi kwenye sherehe za miaka 45 ya Mapinduzi zilizofanyika Gombani, Chakechake, Pemba, 12 Januari 2009, lakini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inamzuia.

Mhariri wa gazeti Daud Ismail Juma anasema alipigiwa simu na “viongozi” wa serikali kwamba asithubutu kusambaza gazeti hilo Gombani. Anamtaja Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Said Shaaban.

Hapa kuna kitu. Kitu hicho hakiwezi kuelezwa vizuri na viongozi wa SMZ wala Khatib. Sharti tuanze sasa kuchokonoa kwa njia ya kutunga ushahidi hatua kwa hatua.

Uchapishaji gazeti ni biashara na huduma. Kuna kununua na kuuza lakini kuna kukidhi haki na matakwa ya jamii ya kusambaziwa habari na maoni yao.

Je, katika hili kulikuwa na haja ya kuomba kibali cha kusambaza nakala 2,000 au hata 5,000 kwenye mkutano wa hadhara hata kama zilikuwa zinatolewa bure?

Woga wa Khatib na mhariri wake unatoka wapi hadi wakajipalia mkaa kwa kuomba vibali visivyohusika? Khatib anasema waliandika barua kuomba kusambaza gazeti lao siku ya mapinduzi.

Gazeti linaweza kusambazwa siku yoyote – mchana au usiku – na mahali popote. Kulikuwa na nini katika gazeti mpaka wamiliki wakashindwa kujiamini na kuomba ruhusa ya kulisambaza? Walikuwa wanatafuta kinga gani na ya nini?

Rafiki yangu ananambia kuwa hatua ya kuomba kusambaza gazeti mkutanoni inaendana na methali isemayo, “Nyani alipomaliza miti aliingia porini,” na huko yalimkuta. Hapa yamemkuta Khatibu na Taifa Huru waliotaka kuonyesha kile ambacho wafuatiliaji Zanzibar wameita, “Nia njema kwa SMZ.”

Sasa gazeti limezuiwa kuuzwa Visiwani. Nakala chache zimepatikana Dar es Salaam. Yawezekana amri imetokana na dosari za hapa na pale katika mawasiliano au hata katika usajili; lakini hayo ni mambo ya kuelekeza, kutatua na kuendelea na kazi. Kusimamisha usambazaji gazeti ni kuingilia uhuru wa habari na maoni.

SMZ ina gazeti liitwalo “Zanzibar Leo.” Hili ni mahususi kwa habari za serikali. Hii ndiyo maana wasomaji na hata wasiolisoma wamelipa jina la “Albamu ya Karume.” Ni jina la utani lakini lililosheheni maana nzito.

Gazeti hili litaandika, kuandika na kuandika juu ya rais wa Zanzibar; litaandika juu ya viongozi wake na hatimaye litaandika taarifa chache juu ya wananchi. Taarifa zote zitakuwa za mnyooko; na kama kwamba kuna sheria maalum, halitaandika lolote jema juu ya upinzani – vyama vya upinzani au viongozi wake.

Kwa upande mwingine, kampuni ya Zanzibar Media Corporation ya Waziri Khatib ambayo inachapisha Taifa Huru inatiliwa mashaka na baadhi ya viongozi wa SMZ. Gazeti la Asumini ambalo limerithiwa na Taifa Huru lilikuwa na chembechembe za kukosoa utawala na wakati mwingine kuandika kiduchu juu ya upinzani.

Hata hivyo, Yusuf Bakari, mchuuzi wa soko kuu Unguja (markiti) anasema, “Kuandika juu ya upinzani ilikuwa njia ya kutafuta uhalali wa wasomaji walio wengi na siyo kwa nia njema.” Hata hivyo, liliandika.

Lakini toleo la kwanza la Taifa Huru, halikuwa na jambo kubwa la kutikisa serikali. Kwa ujumla, maudhui yaliegemea upande wa serikali. Kwa hiyo kuzuiwa kwa gazeti hakuwezi kuwa kumetokana na taarifa mbaya dhidi ya serikali.

Labda sasa tuangalie siasa za Zanzibar. Amri ya kuzuia gazeti imetoka ofisi ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. Waziri wake ni Ali Juma Shamhuna ambaye pia ni Naibu Waziri Kiongozi anayetajwa kuwa na nia ya kugombea urais Zanzibar mwaka 2010.

Waziri Mohammed Seif Khatib naye anatajwa kuwa “anataka,” acha ije 2010. Madai ni kwamba Khatib atatumia gazeti lake kama ngalawa ya kuelea kisiasa na kwa masafa marefu na mapana; kujitangaza na kuzamisha wengine pale wakati ukiwadia.

Bali Shamhuna na Khatib siyo pekee wanaotaka urais Zanzibar. Hamid Mahmmoud anatajwa kuwa kipenzi cha kiongozi mkuu wa sasa wa SMZ. Hamid ni Jaji Mkuu Zanzibar.

Mwingine anayetajwa ni Mohammed Aboud, Naibu Waziri Afrika Mashariki. Tena huyu anadaiwa kuwa ndiye anaweza kuwa chaguo la Rais Jakaya Kikwete. Nani ajuaye?

Hata hivyo, tayari kuna madai ambayo hayajathibitishwa kwamba Khatib yuko karibu sana na Rais Jakaya Kikwete na kwamba alishiriki “njama” zilizomkosesha Shamhuna ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mahusiano yote ya kisiasa yakiishatajwa na kupimwa, tunarejea kwenye hoja kuu kwamba kufungia chombo cha habari ni kupora uhuru wa habari; na hilo halikubaliki kwa kisingizio chochote kile hata cha kutafuta ufalme wa kisiasa.

Waziri Khatib amewahi kuwa waziri wa habari katika serikali ya muungano. Mpaka leo ni mserikali. Anajua kilio cha wananchi na wadau wote wa habari cha kutaka kuondolewa kwa sheria, taratibu, kanuni na hata visingizio pale panapohusu uhuru wa kuwasiliana.

Kwamba Zanzibar bado mtu anaweza kupiga simu na kuzuia gazeti kusambazwa, hakika ni msiba mkubwa. Na Khatib ameanza kuonja machungu akingali serikalini na akiwa waziri.

Je, atakaporudi mitaani, hali itakuwaje? Bila shaka itakuwa mbaya zaidi. Atajuta kwa nini hakujiunga na wananchi na wadau wa uhuru wa habari kupigania kuondolewa kwa sheria, kanuni, taratibu na visingizio vinavyosababisha kuporwa kwa uhuru.

Atajuta, na ameanza kujuta, kwa nini hajaweza kutumia nafasi yake kushawishi na kuleta mabadiliko katika eneo hili la uhuru wa habari katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini bado anayo nafasi.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 18 Januari 2009) katika safu ya SITAKI.

No comments

Powered by Blogger.