Header Ads

LightBlog

MTIHANI MWINGINE KWA CHAMA CHA MAPINDUZI

Uchaguzi na bundi wa Mbeya Vijijini

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI mashujaa wa Tarime washindwe kudhihirisha ushujaa huo katika jimbo la uchaguzi la Mbeya Vijijini. Kwani mazingira yanaonyesha wana kila sababu ya kufanya vizuri.

Lakini mara hii, uwanja una milima mikubwa na mabonde ya kina kirefu, huku bundi wakiwa wamelaliana matawini mwa miti ya mirefu ya kisiasa.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinampeleka rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kufungua kampeni zake. Kwa mujibu wa habari za ndani ya CCM, kiongozi wa kampeni ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Mtaalam wa kampeni na ambaye hana rekodi ya kupoteza jimbo katika chaguzi ndogo ni John Samwel Malecela, makamu mwenyekiti mstaafu na mmoja wa washindani 11 ndani ya CCM waliowania tiketi ya kugombea urais mwaka 2005.

Kiongozi mwingine muhimu kwa upande wa CCM ni kijana Nape Nnauye ambaye tayari ameonya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kutishia “kumlipulia” kashfa Ali Hassan Mwinyi.

Kinachofurahisha katika kampeni za kupata mbunge atakayerithi ofisi ya Richard Nyaulawa, mbunge aliyefariki mwezi mmoja uliopita, ni kwamba viongozi wakuu wanne wa kampeni ya CCM wana mgogoro, ama ndani au nje ya chama chao.

Hao ni Malecela, Nape, Waziri wa Habari ambaye jina lake liko kifungoni na William Ngeleja, waziri wa nishati na madini. Tutaangalia kwa ufupi tu jinsi watakavyojilazimisha kufanya kampeni ya kupata mbunge na kurejeshea CCM kiti cha Mbeya Vijijini.

Tuanze na aliyetajwa mwisho, William Ngeleja. Ikitokea akakanyaga uwanjani Mbeya, atakuwa na kazi ngumu ya kueleza kile alichonukuliwa akisema.

Mara baada ya kifo cha Nyaulawa, Ngeleja alidakwa na vyombo vya habari akisema kwamba serikali itapeleka umeme katika jimbo la Mbeya Vijijini ikiwa njia bora ya “kumuenzi” mbunge aliyefariki.

Wapiga kura watataka kujua kwa nini serikali ilisubiri kifo cha mbunge wao ndipo itangaze kuwa itawapelekea umeme wakazi wa jimbo hilo. Hata hivyo watataka kujua iwapo hiyo ni ahadi ya kweli au kauli za kukidhi haja iliyopo.

Bila shaka Ngeleja atajiuma midomo. Atadai waandishi wa habari walimnukuu vibaya au kwamba aliishasahihisha usemi wake. Vyovote itakavyokuwa, kuna mgogoro kati ya chama kinachoongoza serikali na wakazi wa Mbeya Vijijini juu ya suala hilo na mengine mengi.

Kuna mzee “Tingatinga.” Huyu ni John Malecela. Asiwepo wa kudai kuwa mzee huyu hasahau au huweka kinyongo; au kwamba amesahau na amesamehe. Huyu ni mhanga wa siasa za “shingo-kwa-shingo” kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005.

Ni Malecela huyuhuyu aliyesema wakati wa kugombea nafasi ya mgombea urais ndani ya CCM kwamba amekuwa “tingatinga” linalotengeneza barabara lakini likishamaliza kazi, basi haliruhusiwi huitumia.

Alikuwa anajenga hoja ya kulea na kuimarisha chama chake; kupigania na kuleta ushindi katika chaguzi za marudio na kutafuta muwafaka penye mifarakano. Lakini lilipokuja suala la kugombea urais, yakaja madai kuwa “huyo ni mzee.”

Katika kuleta ushindi kwa chama wakati wa chaguzi, Malecela alikuwa kijana; tena mbichi kabisa. Katika kutafuta urais, akaonekana mzee asiyeweza. Alisononeka. Alibubujikwa machozi ya ndani kwa ndani. Hatimaye akasema amesamehe. Leo anakwenda Mbeya Vijijini kutafuta mbunge.

Hakuna ushahidi kwamba Malecela aliwahi kugombana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba; lakini kuna tetesi kwamba asingependa kufanya naye kazi huko Mbeya.

Taarifa zilizopo ni kwamba kutoiva huko ndiko kumefanya vikao vya CCM kumteua Malecela kwenda Mbeya na pia kutompa jukumu kubwa Makamba katika kampeni hata kama atakwenda uwanjani.

Kiongozi mwingine anayekwenda Mbeya ni Nape Nnauye. Huyu anafahamika kwa kauli kali ndani ya chama. Ni majuzi tu viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM walipendekeza avuliwe uanachama kutokana na kushambulia baadhi yao kwa kushiriki ufisadi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, ni Nape aliyenukuliwa hivi karibuni akisema katibu mkuu wa chama chake, Yusufu Makamba “anakumbatia mafisadi” ndani ya chama.

Inaambukiza hamu kutaka kuona Nape amekaa jukwaa moja na Makamba wakitafuta mbunge wa Mbeya Vijijini. Ni shauku ya wapiga kura kujua iwapo wanaotetea mafisadi hakika wanastahili kushinda katika uwanja huu.

Jukwaa lilelile la CCM lina waziri wa habari, utamaduni na michezo ambaye vyombo huru vya habari vilifungia jina lake kuandikwa kutokana na hatua yake kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa siku 90.

Jina lake na kazi zake vitaandikwa katika magazeti ya CCM, serikali na baadhi ya magazeti ya wamiliki binafsi walio maswahiba wa CCM.

Kifungo cha waziri kinafahamika nchi nzima. Ilikuwa baada ya kufungia gazeti, wahariri wa vyombo huru vya habari – katika jukwaa lao – waliamua kumwadhibu waziri kwa kususia kuandika habari zake na inapotokea zikaandikwa, basi jina lake lisiandikwe.

Waziri aliye “kifungoni,” na wakati huohuo ndiye naibu katibu mkuu wa CCM, anapoteza uzito na hadhi mbele ya wananchi. Hatua tu ya kulipua taarifa kuhusu alivyoua chombo cha habari cha wananchi, inatosha kumwambukiza kizunguzungu na kuleta kizaazaa mikutanoni na hata kusababisha kukosekana kwa kura.

Mbeya Vijijini ni mtihani mgumu kwa CCM hata bila kutaja ahadi lukuki ambazo viongozi wametoa lakini hawajatekeleza na uwezekano wa kufanya hivyo ni finyu.

Hata hivyo, Mbeya ni milima na mabonde yenye rutuba kisiasa. Kila mwenye ufundi wa kutumia milima na mabonde hayo aweza kuvuna. Lakini bundi walioko mitini wakikwekweza vicheko, waweza kuelekeza kilio nyumbani mwa yeyote.

Kilio kitakuwa kwa nani? Mashujaa wa Tarime? Chama kikongwe? Vyama vingine? Tusubiri msimu mpya wa siasa za njiapanda.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28 Desemba 2008)

No comments

Powered by Blogger.