Header Ads

LightBlog

SERIKALI INALEA MIGOGORO VYUO VIKUU

Unyapara unavyoua vyuo vikuu


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ifukuze wanafunzi wa vyuo vikuu kwa visingizio vya kushindwa kujaza fomu au kwa sababu yoyote ile.

Sababu pekee ya wanafunzi kugoma ilikuwa kutosikilizwa na utawala vyuoni; kutosikilizwa na Bodi ya Mikopo na kutosikilizwa na serikali kwa ujumla.

Hoja kuu ya wanafunzi wengi ni kwamba wazazi wao hawana uwezo wa kulipa kiasi cha fedha kinachohitajika, hata kama ni kuchangia karo. Hicho ndicho kiini cha mgogoro.

Hatua ya kugoma inakuja ili kuongeza sauti kwa madai yao ya kutaka Bodi ya Mikopo Vyuo Vikuu iwalipie karo kwa asilimia 100 kutokana na wazazi kutokuwa na uwezo.

Kwamba kuna baadhi ya wazazi wa wanafunzi hawana uwezo wa kulipa hata Sh. 100,000 kwa mwaka ni jambo ambalo haliwezi kukanwa. Ni wengi sana. Mapato yao – ya familia nyingi – hayafikii kiasi hicho kwa mwaka.

Hata kwa takwimu za waziri wa fedha kwamba kila Mtanzania sasa ana pato la Sh. 1,500 kutwa, bado hakuna mwananchi anayepata kiasi hicho (au Sh. 43,580 kwa mwezi) anaweza kugharimia elimu chuo kikuu. Hizi ni “takwimu za faraja.”

Ili kupata takwimu hizo, unachukua anayepata mabilioni ya shilingi kila mwezi; unaweka anayepata mamilioni, unaweka anayepata malaki na anayepata maelfu; unaunganisha asiye na chochote.

Jumla ya fedha unazopata unagawia kiumbe mtu anayepumua (hata wasio na kitu na vichanga ambavyo havijazalisha) ndipo unapata Sh. 1,500 kwa siku. Ukweli unabaki palepale, kwamba wengi hawana hata Sh. 200 na miongoni mwao ni wazazi wa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu.

Takwimu za serikali ni kwa ajili ya kupima kukua na siyo maendeleo ya uchumi. Maendeleo huonekana kwa watu na kukua huonekana kwenye tarakimu, tarakimu, tarakimu! Mawili yasipooana kinabaki kicheko cha nyani.

Na hivyo ndivyo ilivyo. Wanafunzi katika vyuo vikuu ama walilie serikali ili isikie kilio chao na kufanya mabadiliko au wazazi wao wauze kila walichonacho ili watoto wapate elimu ya juu.

Uwezekano mkubwa ni kwamba wasio na cha kuuza watakuwa wengi. Wenye vya kuuza havitatosheleza hata malipo ya nusu mwaka. Wenye vizito kidogo huenda wakapata asilimia inayohitajika lakini kwa mwaka mmoja na nusu au miwili. Basi!

Hapa, ama wazazi na wanafunzi watafute mikopo ya kuwanyonga kutoka kwa yeyote mwenye fedha na kuweka roho zao rehani; au wauze moyo, utumbo, vipande vya mwili au mwili mzima ili wapate karo.

Kinachoonekana haraka kuwa kinaweza kufanyika ni kuacha masomo. Lakini utaacha masomo ili ufanye nini wakati shabaha yako – tangu shule za awali – ni kupata maarifa na kuyatumia kwa manufaa yako na jamii nzima?

Wanafunzi vyuo vikuu hawataki kusalimu amri kwa umasikini wa wazazi wao na familia zao. Wanaomba serikali iwawezeshe kusoma kwa kuwagharimia na wao warejeshe malipo baada ya kumalisha masomo.

Katika mazingira magumu ya aina hii, mgomo ni kitu ambacho hakiepukiki; hasa mgomo unapokuwa njia ya kukumbushia, kusisitizia na hata kushinikizia hoja.

Kwa hiyo, hatua yoyote inayochukuliwa na watawala vyuoni sharti ipimwe na ukweli wa maisha ya wazazi wa wanafunzi. Hivyo kuwafukuza wanafunzi ni kuwaadhibu kwa kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia karo.

Kinachoongeza machungu ni masharti ya watawala vyuo vikuu ambayo yanaundwa nje kabisa ya uelewa wa mazingira yanayowakabili wazazi na watoto wao.

Hoja kuu ni kwamba wanafunzi hawana fedha za kulipa. Kuweka masharti ya kurejea chuoni wakiwa na fedha, ama ni kuwakejeli au kuwaambia wafanye tuliyojadili hapo juu ikiwa ni pamoja na kujinadi wenyewe.

Mwanafunzi ambaye tayari ni bidhaa atarejea vipi chuoni? Bidhaa inakaaje darasani na kusikiliza mhadhiri akitema moto? Yule ambaye anajua muhula ujao hatarejea chuoni ana amani gani moyoni?

Hapa ndipo kila mwenye nia njema kwa elimu ya juu nchini anapaswa kuitaka serikali, kuacha kuona wingi wa wanafunzi vyuo vikuu kama kitu cha kujivunia wakati haiwezi kuwahudumia.

Sharti kuwepo mpango maalum wa kuhakikisha waliochaguliwa kwenda vyuo vikuu wanawezeshwa kukaa huko na kusoma katika mazingira yasiyotibua akili kwa amri za kulipa wasichokuwa nacho.

Hapa patahitajika kujua nani wamechaguliwa; wana uwezo gani kifedha na wasio na uwezo wanapata vipi elimu ya juu. Hii ndiyo kazi ya utawala vyuoni, ukiwakilisha serikali.

Kuwa wakali kama manyigu na kukariri kauli kwamba kila mmoja ana uwezo wa kulipa Sh. 400,000 au 600,000, ni kushindwa kazi ndogo ya kuchambua uwezo wa wahusika na hata kupendekeza kwa serikali hatua muwafaka za kuchukuliwa.

Sasa tutegemee vyuo vikuu kuwa sehemu ya minyukano kati ya watawala wa vyuo na wanafunzi. Asiye na fedha asisome; aliyenazo apete hata kama hakufaulu!

Ikifikia hatua hiyo ndipo serikali itajua kwamba, ujenzi na upanuzi wa vyuo vikuu vyake ni kwa kutafuta sifa tu za takwimu za “wasomi” na siyo ubora wa maarifa kwa maendeleo.

Serikali haina budi kuamua. Kulipa karo. Wanafunzi wasome; tena katika mazingira bora na vifaa vinavyostahili na iweke utaratibu wa kurejesha fedha hizo pindi wanafunzi wanapohitimu.

Kwa watawala vyuoni kukatalia wanafunzi zaidi ya 2,000 kurudi masomoni, kama ilivyoelezwa juzi, kwa visingizio visivyo na mashiko, ni kukana ukweli unaotafutwa na elimu na kushindwa kutumia madaraka waliyokabidhiwa.

Unyapara ukiisha, maarifa na hekima vitatawala. Tatizo la wanafunzi kushindwa kulipa karo linaweza kugeuka na kuwa changamoto; kwani litakubaliwa na kutatuliwa. Sitaki liendelee.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika Tanzania Daima Jumapili toleo la 11 Januari 2009)

No comments

Powered by Blogger.