Header Ads

LightBlog

SERIKALI YAAFIKI KAZI YA FOUNDATION

Kigeugeu cha serikali kuhusu AZAKi

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ibadili msimamo wake wa kutambua na kuthamini asasi za kiraia nchini (AZAKi) uliosisitizwa na mawaziri wawili wiki hii.

Katika Tamasha la Sita na Maonyesho ya Asasi za Kiraia yaliyomalizika Ijumaa, serikali imetamka kuwa inatambua na kuthamini kazi za AZAKi na kwamba iko tayari kushirikiana nazo.

Wa kwanza kutoa kauli hiyo alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Margaret Sitta pale alipofungua maonyesho kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mwingine alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Batilda Buriani aliyefungua jukwaa la kila mwaka la asasi hizo katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Kwa miaka mingi sasa baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakielekeza shutuma na kejeli kwa AZAKi. Wamedai kuwa asasi hizi “ni za mfukoni” wakiwa na maana kuwa ni za wababaishaji; wamedai ni za mtu mmojammoja; zinafuja fedha tu; hazina manufaa kwa jamii na kwamba zinatumiwa na wafadhili.

Katika msafara wa mamba na kenge wamo. Lakini siyo msafara wa kenge na siyo siku zote. Ndio maana methali zinabadilika: Samaki mmoja akioza katika furushi, usitupe wote; bwaga furushi chini na changua ambao hawajaoza. Siyo wote waliooza.

Hili linathibitishwa na asasi mwavuli ya Foundation for Civil Society. Kwa miaka mitano sasa Foundation imesimamia asasi hizi kwa maana ya kuzipa uwezo. Imetafiti kuwepo kwake, mahali zilipo, kazi zake, mafanikio na changamoto zake.

Wakati kazi hiyo inaendelea, Foundation imejikita katika jukumu la kuzipa uwezo; ili ziweze kujipa sura, taswira na mwelekeo unaoendelea. Ni uwezo huo ambao unazipa AZAKi heshima na thamani mbele ya jamii. Aliyeona kazi za asasi Mnazi Mmoja au kuhudhuria jukwaa, hawezi tena kubeza.

AZAKi huanzishwa na wananchi katika maeneo yao. Ni matunda ya akili zao. Ni matokeo ya mahusiano na mfumo wa maisha na mazingira pale wanapoishi. Nyingine zaweza kuanzishwa kwa ushauri na ushawishi mwanana uliolenga kuinua hadhi ya wahusika.

Asasi hizi zinatokana na utashi binafsi wa wanaoziunda. Malengo yake yameelekezwa katika kukabiliana na changamoto za mahali walipo na ushirikiano miongoni mwa asasi mbalimbali (mitandao) zenye malengo yaleyale au yanayoshabihiana katika Kata, wilaya, mkoa na taifa.

Kwa hiyo, hata ziwe asasi zenye kazi moja au zinazohusika na shughuli nyingi, shabaha imekuwa moja: Kubadili mazingira wanapoishi ili yawe bora zaidi kwao na jamii. Hapo ndipo kuna umuhimu wa AZAKi.

Raia wanapounda chombo chao kwa madhumuni ya kukabiliana na changamoto katika mazingira yao, wanakuwa wametambua jukumu lao katika maendeleo yao wenyewe. Wanakuwa waelewa kuwa hawawezi kusubiri serikali ya mtaa au kuu kuwafanyia kila kitu.

Lakini muhimu zaidi, wanakuwa wametambua umuhimu wa kujiunga pamoja, kufikiri pamoja na kutenda pamoja. Wanakuwa wamejifunza kujitegemea kwa njia ya vitendo.

Kwenye moyo huo, ukiongeza uwezeshaji kwa njia ya raslimali watu, uelewa katika kupanga na kutekeleza, ufundi katika asasi zinazohusiana na uzalishaji na kiwango fulani cha fedha, raia watafanya shughuli zao bila kusubiri kuhubiriwa na wanasiasa au warasimu kutoka serikalini.

Kwa hiyo AZAKi ni hatua muhimu katika kujitegemea. Kwanza, kujitegemea kifikra na kuweza kufanya maamuzi sahihi miongoni mwa wanachama wa asasi na jamii kwa ujumla.

Pili, kujitegemea kwa uzalishaji wa mawazo na mazao ambavyo vinanufaisha jamii ya karibu na mbali kama ilivyodhihirika jijini Dar es Salaam wiki hii.

AZAKi zilizokutana Dar es Salaam katika tamasha la sita ni chemchemi ya mwamko wa jamii nzima. Wakati waliokuwa hawajaunda asasi watakuwa wamechocheka kuanzisha haraka; wale waliomo wamepata fursa ya kupeana uzoefu na fikra mpya.

Kupanuka kwa shughuli za AZAKi na kuongezeka kwa asasi nyingine, kuna maana ya kupatikana kwa fursa zaidi za wananchi kuwa pamoja, kufikiri pamoja na kutenda pamoja.

Hii ndiyo nguvu ya jamii ya kiraia. Ndiyo chimbuko la heshima na thamani ya asasi. Jamii iliyoungana kwa njia ya AZAKi ina nguvu ya kufikiri, kutambua mazingira na matakwa yake, uelewa na uwezo wa kusema “ndiyo” au “hapana.”

Hata katika nchi zilizoendelea, AZAKi zina nafasi kubwa katika kuamua mwelekeo wa nchi, kwa kuwa zinachangia fikra na ni kiwakilishi cha matakwa ya jamii pana. Hujafaulu kisiasa au kiuchumi kwa kuacha AZAKi nje ya duara la fikra na utendaji.

Na hapa wengi tunafikiria asasi zilizojiunga na Foundation. Lakini kuna nyingine nyingi ambazo hazijasajiliwa kisheria. Zina nguvu kuu katika maamuzi pale zilipo na zinapata ushawishi kutoka kwa zile ambazo zimepiga hatua katika kuzalisha mawazo na mazao.

Kwa hiyo kazi hii ya kukuza uwezo wa AZAKi, ambayo inafanywa na Foundation for Civil Society, hainabudi kuendelezwa, kukuzwa na kutetewa kwa viwango vyote. Hainabudi kupanuliwa kufikia wengine ambao wana hamu ya kuwa asasi inayotambulika kimuundo.

Ni kwa msingi huo sitaki kuona au kusikia serikali inarudi nyuma na kuanza kubeza AZAKi, hata kama itatokea mara moja au mara kadhaa serikali kutofautiana kimawazo na moja au baadhi ya asasi katika utekelezaji wake.

Jamii ambamo AZAKi zimeenea kuna uhuru mpana wa kufikiri na kutoa maoni; jamii nzima inaongea bila woga wala aibu na inatenda kwa uhakika. Foundation itakuwa imefanikiwa iwapo itafikisha Tanzania katika kiwango hicho. Na ifike huko!

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Toleo la kesho 30 Novemba 2008)

No comments

Powered by Blogger.