Header Ads

LightBlog

MUGABE ANATAKA KUFIA IKULU

SITAKI

Mugabe anavyoisha kama sabuni

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Afrika iendelee kukumbatia Robert Mugabe, rais wa sasa wa Zimbabwe ambaye hakika amechoka, amechakaa na hana jipya la kufaa nchi yake na bara hili.

Katika Zimbabwe hivi sasa, aliyebakia mtu wa karibu sana na Mugabe na mshauri pekee mwandani ni mke wake. Ukiona askari wa jeshi la ulinzi wanaanza kushiriki maandamano, ujue jamii imepokea mlio wa bundi. Ishara mbaya kwa Mugabe.

Ukiona askari polisi wameanza kushiriki uporaji katika maduka ya biashara jijini Harare badala ya kulinda amani; na wengine wakigoma kuwapiga wananchi wasiokuwa na hatia, ujue harufu ya bundi imepita. Ishara mbaya kwa Mugabe.

Angalia walimu – nguzo kuu katika Afrika ya wanasiasa na serikali wakati wa mapambano na shida kuu. Ona walivyoanza kuikaba koo serikali wakidai kulipwa mishahara katika fedha za kigeni, kwani thamani ya dola ya nchi imeporomoka kupindukia. Jua basi, huu ni mbomoko.

Ukiona wanasiasa wenza wa Mugabe wanaanza kumkatalia, kumkana, kumpinga; na wengine kwa woga wakiamua kuacha kazi za kisiasa ili isionekane wanapinga “komredi,” ujue Mugabe kabakiwa na mvumo wa sauti na si mantiki ya kauli. Mlio wa bundi.

Mgabe alichuja. Wananchi wakasema sasa basi. Akakataa. Ili abaki madarakani akaanzisha uvamizi wa mashamba ya wazungu ili kupata sifa za wakati huo. Yakavamiwa. Yakachukuliwa na mawaziri wake, maofisa wake, marafiki zake na vijana wa mijini waliojiita “wapigania uhuru” lakini ambao walikuwa hawajazaliwa wakati wa vita vya ukombozi.

Mugabe aliona anakwenda na mkondo wa maji. Ni pale wanajeshi walipotaka kustaafu akiwa hana hata senti ya kuwalipa. Mungu bariki, vikaingia vita Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Akaahirisha malipo ya wastaafu; akapeleka majeshi vitani na kuahirisha kasheshe. Bundi huyo.

Kilimo kikadorora. Chakula kikapungua na hatimaye kukosekana. Mugabe hakuona tatizo. Aliona kuwa ni wafanyabiashara waliokuwa wakificha vyakula. Akavamia wachuuzi wa Harare. Akawapiga. Akawapora. Njaa haikuisha. Ndio hasa imeota ndevu. Sauti ya bundi.

Hakuna atakayesahau operesheni ya kuwaswaga wakazi wa Harare nje ya jiji hilo ili wakakae shamba na wasiwe vichaka vya “wapinzani” mjini. Nyumba na vibanda walimoishi vilivunjwa. Walikosa makazi. Walikosa chakula. Walipoteza mali zao – ndogo, chache au nyingi – kila mmoja na kiwango chake.

Busara zikavuma dunia nzima. Mugabe umechoka. Akajibu: Hapana. Kilimo kikafifia. Uchumi ukadorora zaidi. Amani ikapungua na kubakia kwenye makazi ya walioko kwenye utawala. Hasira na chuki vikatawala. Sauti ya bundi.

Naye Mugabe hakukaa kimya. Kila tatizo akalihusisha na wakoloni wa zamani wa Uingereza. Akavurumisha maneno makali kwa Uingerza na Marekani. Akasema matatizo yanaletwa na ubeberu. Akataka wananchi waelewe hivyo. Wananchi wakaelewa tofauti na alivyotaka. Sauti ya bundi.

Bado anataka kutawala. Nyenzo yake pekee ya kisiasa ikiwa bado ileile; kwamba Waingereza hawakutoa fedha za kufidia wazungu walioshika mashamba makubwa aliyoamua kuwanyang’anya.

Suala la umilikishaji ardhi lilihitaji kushughulikiwa miaka kumi baada ya uhuru; kwa mujibu wa Katiba ya uhuru iliyoandikiwa Uingereza. Baada ya miaka hiyo Mugabe alikuwa “bize” na uhondo wa ikulu. Ujenzi wa kasri. Ulimbikizaji ainaaina na majigambo ya kupambana na ubeberu.

Mugabe alisahau kuwa aliingia mjini akiwa na wapiganaji; ambao hawakuwa na jembe, panga, koleo, nyumba wala shamba; bali bunduki. Badala ya kutumia miaka kumi ya kwanza ya uhuru kujenga misingi ya kuwapa makazi, anawaambia washindane na wengine katika kuvamia mashamba ya wazungu.

Kutwaa mashamba ya wazungu na wengine wenye ardhi kubwa katikati ya wananchiwasiokuwa na ardhi, ni suala linalokubalika lakini lililohitaji mipango na utaratibu katika kugawana raslimali za taifa. Mugabe alijisahau. Hadi bundi alipolia na yeye kuamuru, “Kamata!”

Chunga haya: Uhaba wa chakula na njaa. Kukosekana kwa fedha za ndani zitokanazo na kodi na kutokuwepo fedha za kigeni kutokana na kutokuwa na bidhaa za kutosha zilizouzwa nje. Ukame. Mafuriko. Mipango mibovu isiyokidhi matakwa ya nchi. Kupungua kwa misaada kutoka nje kulikotokana na wafadhili kutilia mashaka utawala wa Mugabe.

Ongeza haya: Kujitokeza kwa chama cha upinzani chenye nguvu. Migomo ya vyama vya wafanyakazi. Mwamko wa wananchi kuhusu haki zao. Tishio la jeshi kuasi, isipokuwa askari wachache walio karibu na rais. Kauli za viongozi wa mataifa mbalimbali juu ya mwenendo wa uchumi na utawala nchini Zimbabwe.

Yote haya na mengine, yalifanya Mugabe akose pumzi. Kukosekana kwa pumzi kunatokana na kukosekana kwa majibu kwa maswali mengi aliyoulizwa na wananchi, walimu, vyama vya wafanyakazi, askari na wanasiasa wenzake.

Matokeo ya kukosea majibu, ni kutumia mkono wa chuma. Mugabe akawa mbogo; dikiteta. Akamwaga chumvi kwenye kidonda. Akavunja haki za msingi za binadamu kwa kuziba mifereji ya mawasiliano – kupokonya uhuru wa maoni – na kujenga woga katika jamii kwa shabaha ya kuinyamazisha. Bundi hilooo!

Ni uchaguzi mkuu wa mwisho nchini humo uliompa Mugabe hali halisi ya utashi wa wananchi. Akabwagwa katika kinyang’anyiro cha ubunge na urais. Hakupata kura za kutosha kutamkwa kuwa rais moja kwa moja.

Marudio ya uchaguzi wa rais ndiyo yalionyesha sura yake kamili. Akatishia kuita jeshi lake kuchukua nchi. Akatangaza, kupitia askari wake watiifu sana au waoga, kwamba yuko tayari kuanzisha upya vita vya kukomboa nchi kwa njia ya silaha. Akatoa macho. Akafoka dunia nzima ikasikia.

Katika hali isiyo ya kawaida, Mugabe akarudia kutamka kuwa chama cha upinzani kinatumiwa na wazungu na mabeberu na kwamba hawezi kutawaliwa na wakoloni. Kauli za kijasiri katika mazingira magumu na tata.

Polisi wa Mugabe wakawaandama wapinzani. Wakawakamata. Wakawapiga. Wakawafunga. Wakawazuia kufanya mikutano. Mugabe na ZANU-PF wakawa pekee walioingia kwenye raudi ya pili ya uchaguzi wa rais. Sasa nchi haitawaliki na yeye, pamoja na kujiita rais, ameshindwa kuunda serikali.

Nani, miongoni mwa viongozi wa Afrika ambaye hajui yote haya? Mugabe anaendelea kubebembelezwa kwa lipi; hadi lini na kwa faida ipi na ya nani?

Mugabe ametoka kuwa mpigania uhuru shupavu wa Zimbabwe huru, kuwa rais na sasa dondandugu la Afrika lisilotamanika nchini mwake na bara zima. Ameonyesha kutoshaurika. Acha Mugabe aende na maji.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 7 Desemba 2008) Mwandishi anapatikana kwa:
Simu:0713 614872
imeili: ndimara@yahoo.com

2 comments

Fita Lutonja said...

Makala nzuri nimefurahi sana ila natamani kuwaokoa watanzania wenzangu wanaisha maisha magumu kama wako jehanamu

Fita Lutonja said...

Nitembele katika blogu www.fitalutonja.blogspot.com

Powered by Blogger.