Header Ads

LightBlog

TUMPONGEZE OBAMA LAKINI NI MMAREKANI


Wanaotarajia Obama kuwaokoa

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Watanzania na Waafrika wakae wakisubiri Barack Obama, rais wa 44 wa Marekani awaletee unafuu wa maisha au asababishe mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mataifa yao.

Kila mmoja, popote alipo, hana budi kueleza hisia zake kuhusiana na ushindi wa Obama lakini baada ya hapo arejee kwenye nafasi yake ya awali na kupambana na changamoto za maisha katika nchi na bara lake.

Kwa mantiki hii kusiwepo wa kusema kwamba kupanda kwa Obama kwenye kiti cha urais kutaiokoa Tanzania au Afrika.

Obama ana nchi yake. Ni Marekani. Obama ana wananchi wake. Ni Wamarekani. Obama ana majukumu yake mazito ambayo ameahidi kuyakabili. Ni majukumu ya Marekani na Wamarekani.

Majukumu ya Obama na wananchi wake ndiyo Na. 1 kwa rais wa 44 wa taifa kubwa kiuchumi na kijeshi na ambalo kwa takribani miaka 60 sasa limeitwa taifa la kibeberu duniani.

Kama ubeberu wa Marekani ungalipo leo – na hatuhitaji wa kutushawishi kuwa umeisha – basi ni Obama atakayeusimamia. Chembechembe za Uafrika ndani ya Obama haziondoi ubabe wala ubeberu wa Marekani.

Kuna mafunzo hapa. Barack Hussein Obama, mwenye damu mchanganyiko, ni raia wa Marekani. Ni uzao wa wananchi wa Marekani wenye historia ndefu ya kupigania haki na usawa wa watu wote ndani ya nchi yao.

Kuingia kwake madarakani kunampa fursa ya kujenga hoja zaidi na sahihi kwamba Waafrika-Wamarekani, kama walivyo raia wengine nchini humo, “wanaweza” na wataweza.

Ushindi wa Obama ni mwendelezo tu wa harakati za kijamii nchini Marekani za kuthibitisha kuwa weupe au weusi – jambo ambalo limekuwa msingi wa ubaguzi wa rangi nchini humo – ni mbinu chafu, ya kale, ya kishenzi, isiyo na maana tena na isiyokubalika.

Lakini siyo kwamba jambo hilo lilikuwa halijaeleweka hadi Novemba 4, bali ukurutu katika vichwa vya baadhi ya wabaguzi, ambao hutumia rangi kunyonya jasho na damu ya jamii na kunyima haki za msingi na fursa mbalimbali, huwa hauishi mara moja.

Kwamba Obama mwenye mzazi wa Kenya na mzazi wa Marekani amepanda hadi ofisi kuu ya utawala nchini humo, unaweza kuwa ushahidi mwingine kuwa Wamarekani wanaendelea kukata minyororo iliyowafunga akili kwa tarkriban karne tano; na wanachopaswa kujali sasa ni “tunda” la nchi yao na si rangi ya mwili.

Bali jambo moja ni wazi kabisa. Obama amedhihirisha kujitambua – yeye ni nani katika jamii yake – na anaweza kufanya nini kwa jamii hiyo. Alichoomba ndicho amepata.
Pamoja na urais, aliomba kuvunja zaidi nguvu za fikra dhalili zinazojali rangi kuliko utu. Ameongoza Marekani kushinda.

Obama asingechaguliwa kuwa rais wa Marekani kama siyo Mmarekani. Hivyo, jukumu lake ni kutumikia Wamarekani, kusimamia na kuendeleza mipango ya Wamarekani, kulinda taifa na Katiba ya nchi yake na kwa ujumla, kushirikiana na mataifa mengine kukabiliana na changamoto za dunia.

Tunaloweza kujifunza kutoka kwa Obama ni jinsi alivyokua, kujilea, kuingia katika jamii yake na kukubalika; kuingia katika moja ya vyama vikubwa nchini, kukubali kulelewa na kujiimarisha hadi kuwa mahiri katika siasa za chama chake; kupata uongozi kama seneta na sasa kuchaguliwa kuwa rais.

Obama ni rais kama rais mwingine wa Marekani. Chembechembe za weusi hazimfanyi awe na huruma kwa Afrika. Atakwenda kwa kufuata misingi na sera za nchi yake. Hatua yoyote ya kutaka upendeleo kwa Afrika au hata Kenya, ambayo haimo katika sera zao za mambo ya nje, yaweza hata kuhatarisha upangaji wake ikulu.

Lakini hata akitaka kuwa laini kwa Afrika, bara hili, Tanzania ikiwemo, halina sababu ya kutarajia au kusubiri fadhila za mkuu wa nchi wa Marekani.

Hakuna sababu ya kutarajia huruma na misaada kutoka Marekani wakati watawala wa nchi zetu wamejenga au wanalinda mifumo inayofuja kodi za wananchi, misaada na hata mikopo kutoka nje.

Hakuna sababu ya kutarajia Obama awe karimu wakati watawala wetu wanauza nyasi, miti, misitu, wanyama na madini kwa bei ya kutupa. Ni matumizi ya raslimali hizi ambayo yangefanya mkuu wa nchi Tanzania awe na jeuri sawa na rais wa nchi kubwa, kwani nchi yake itakuwa inajitegemea na kutembea kifua mbele.

Acha vijana wajifunze na kuiga uwezo wa Obama wa kujieleza na kujenga hoja kwa uthabiti. Acha wajifunze ujasiri wake wa kutosubiri kupewa bali wa kujitafutia. Acha wajifunze umuhimu wa elimu kama silaha muhimu maishani.

Tuwaache wakubwa na wadogo wajifunze kutokata tamaa na badala yake kuwa king’ang’anizi katika kupigania haki na fursa sawa za kijamii na kisiasa.

Baada ya hapo tumwache Obama atumikie taifa lake kama marais wengine wa Marekeni. Kama ni suala la maendeleo na mabadiliko katika maisha ya wananchi katika Afrika, tuwakabe wanaotutoza kodi, kupokea misaada na mikopo halafu wakatembeza bakuli la ombaomba.

Tanzania na Afrika, ina unyonge na umasikini wa kuletewa na watawala – ama kwa kutojali, kushiriki kuibia nchi, kuendeleza mifumo mibovu inayoendelea kufunga nchi hii kwenye bomba kuu la unyonyaji wa kimataifa au kwa ujinga.

Afrika haipaswi kutarajia Obama aingie jikoni na vyumbani mwetu kumaliza matatizo yetu. Tumpe hongera; kaandika historia. Basi! Kinachohitajika ni kuandaa mbinu za mabadiliko. Na uwezekano wa mafanikio katika kuleta mabadiliko ni mkubwa.


(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 9 Novemba 2008 chini ya safu ya SITAKI)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
Powered by Blogger.