Header Ads

LightBlog

IGP HAWEZI KUCHUNGUZA SERIKALI

Migomo inasababishwa na serikali,
Polisi watachunguzaje mwajiri wao?


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema apoteze muda kuchunguza kiini cha migomo vyuoni au popote pale nchini. Kwani kiini kinajulikana.

Tuanzie kwenye kitongoji. Wenyeviti wa vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba wamegoma kuanzia Novemba 10 mwaka huu. Wanadai malimbikizo ya posho zao za miaka miwili. Wanadai haki yao.

Wanafunzi wa shule za msingi za serikali – Tabata na Mbagala jijini Dar es Salaam na baadhi ya shule mikoani – wameandamana kudai haki yao ya kufundishwa. Hii ni baada ya mgomo baridi na mgomo wa wazi wa walimu. Wanadai haki yao.

Walimu wameandamana na kugoma kufundisha. Wanadai malimbikizo ya mishahara yao, posho za kujikimu pale walipopewa uhamisho, malipo ya likizo, nyongeza za mishahara ambazo zimekwama kwa kipindi kirefu na marupurupu yao mengine. Wanadai haki yao.

Wanafunzi katika vyuo vikuu vya serikali wameandamana vyuoni kwao na kugoma kuingia madarasani wakitaka serikali iondoe utaratibu wa uchangiaji karo wanaosema unaumiza wanafunzi ambao wazazi wao ni masikini.

Zimwi la uchangiaji linatishia vyuo kubaki vya wenye fedha ambao siyo lazima wawe na uwezo. Pindi waliochaguliwa kuingia vyuoni kwa utaratibu wa alama maalum za kinachoitwa “kushinda” watakapoondolewa, vyuo vitafurika wenye fedha hata kama ni kugeuza makazi hayo kuwa mapango ya wavuta bangi.

Wanafunzi wanapinga ubaguzi katika mfumo mzima wa uchangiaji, lakini pia wanadai haki ya kunufaika na raslimali za nchi hii – nyasi, miti, misitu, mito, maziwa, bahari, madini, ardhi na nyingine – ambazo zimeneemesha watu wa nje kuliko wazawa wa Mama Tanzania.

Kusoma ni haki yao. Kusomeshwa na raslimali za nchi yao ni haki yao pia. Kugoma na kuandamana kusisitiza haki, maoni na msimamao wao ni haki yao katika kukumbusha viongozi wanaokaa kimya wakijifariji, “acha waseme watachoka!”

Vyama vya wafanyakazi vinaandaa migomo. Vinataka kima cha chini cha mshahara kipandishwe. Vinasema mishahara ya sasa halingani na hali halisi ya maisha nchini. Vinadai haki ya kuishi ya wanachama wake.

Wafanyakazi wa benki (National Microfinance Bank) ya Dar es Salaam wanagoma. Wanataka mkataba wao na mwajiri utiwe saini na wao wapate hisa zao katika benki. Wanadai haki yao.

Wastaafu hawana wa kugomea. Wanaandamana. Wanaziba barabara. Wanapanga kuweka kambi ikulu ingawa wanatishwa. Mama ntilie waliokuwa wakiwapa chakula, pale karibu na kituo cha garimoshi jijini Dar es Salaam, wameacha kutoa mkopo wa chakula.

Wastaafu wanapinga kufa. Wanadai kulipwa. Wakataa kauli za baadhi ya viongozi kuwa waliishalipwa zamani. Wanataka kusikilizwa.

Hakuna haja ya kuendelea kuorodhesha wanaogoma na wanaoandamana katika Tanzania leo. Hakuna haja ya kurodhesha sababu zinazofanya wagome na kuandamana. Ziko wazi.

Ni bahati mbaya kwamba Saidi Mwema hawezi kuchunguza wale wanaochelewesha na wanaonyima haki wenyeviti wa vitongoji Tandahimba, wanafunzi shule za msingi, walimu nchi nzima, wanafunzi vyuoni na wafanyakazi mahali pao pa kazi. Hawezi.

Mwema hawezi kwa kuwa waliomwajiri ndio chanzo cha malalamiko, migomo na maandamano. Labda ataelewa hili vizuri pale polisi wakigoma au wakiandamana.

Mwema hawezi na wala hana haja ya kufanya uchunguzi. Wanaoleta na wanaochochea migomo wanafahamika. Ni wale waliokabidhiwa madaraka katika maeneo mbalimbali ya utawala na hawafanyi kazi yao.

Ni wale wanaoona watendaji hawatendi lakini wanawaacha kwenye madaraka hadi malalamiko, migomo na maandamano. Ni serikali ambayo inakaa kimya huku wananchi wakilia na kusaga meno; lakini pia wakiigeukia na kuilaani vikali. Mwema hawezi kuchunguza serikali.

Pamoja na kwamba kugoma ni haki ya mtu kusisitiza madai yake, leo hii ondoa malalamiko ya wanaogoma kwa kuwapa haki zao; nani atasikia sauti zao, migomo wala maandamano? Mwema hahitaji kuchunguza.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 23 Oktoba 2008 chini ya safu ya SITAKI).

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

3 comments

freddy macha said...

Ndimara, hii makala yako kuhusu migomo imenikumbusha makala zako za miaka ya Sabini wakati ukifafanua mambo katika gazeti la Uhuru. Unakumbuka? Unagusa ini na mafigo kabisa. Na ukichunguza kila kitu ni kama wakati ule wa 1970-78; hali ngumu ya uchumi, migomo,heka heka, reggae, wanasafu (leo ongeza wanablogu) mikakati na harakati. Na wewe umo ndani huchoki, nakuona. Je, kitabu chako cha Kaya bado kinapatikana? Waeleze wasomaji waliozaliwa karibuni wakisome. Andika pia vingine.Fikra zako na mtindo wako wa kuandika unahitajika ...

ndimara tegambwage said...

Nakujibu Macha, Salama hukooo?Bado naandika. Nina zaidi ya vitabu 20 sasa. Nusu ni vya watoto lakini vyote vya harakati. Duka la Kaya kipo; juzijuzi niliambiwa kinatumika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Mwanza - fasihi katika ualimu. Siku moja mwaka jana, nilialikwa kuongea na jumuia ya vyuo vikuu Morogoro. Niliposimama na kutambulishwa kuwa ndiye mwandishi wa Duka la Kaya, karibu zaidi ya nusu ya hadhira walisimama na kushangilia. Waliishakisoma. Nadhani kiliwakuna sana...vingine pia vina moto uleule. Asante kwa kunikumbusha kazi ile iliyoandikwa katika kipindi kigumu...

freddy macha said...

Kuna kijana mmoja mhadhiri anakutafuta umtumie vitabu vya Duka la Kaya akuuzie hapa Majuu.
Naomba tuwasiliane tafadhali.
Simu yangu bado unayo? Nitumie basi SmS.

Powered by Blogger.