Header Ads

LightBlog

MAISHA YA WATOTO YANAPOHARIBIWA ASUBUHI

Serikali inayochekea wabakaji Liwale

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali ishindwe kuelewa umuhimu wa haraka wa kupambana na unyama unaofanywa na wabakaji katika wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.

Taarifa za wiki hii kutoka wilayani Liwale zinasema “Watoto 255 wajifungua Liwale.” Lugha laini kama vile inatoka kwa mama mzazi anayesema mwanae aliyeolewa sasa amejifungua.

Sivyo ilivyo. Tufuatane na taarifa: “Idadi hiyo ni ya watoto kuanzia miaka 12, 13, 14 na wachache wa umri wa miaka 15…Hao ni wale wanaokuja hospitali. Wengine wakiishapima na kuona wana ujauzito hawaji tena…”

Maelezo hayo yanafafanua kuwa “watoto” hawa hawajaolewa. Kwanza hawajafikia umri wa kufanya maamuzi juu ya kuwa na familia. Hawajapewa ushauri na wazazi au walinzi wao. Ni watoto waliokumbwa na jinai.

Hao ni watoto waliobakwa na wanaume wa rika mbalimbali na kuwasababishia ujauzito. Ni watoto wa umri wa kwenda shule ambao wamenyimwa na, au wamekoseshwa haki ya kupata elimu. Wametupwa mitaani.

Hao ni watoto ambao utamu wa utoto wao umekatishwa. Ambao ung’avu wa ujana wao umeingizwa doa hata kabla hawajaweza kujua jinsi ya kujihudumia. Ambao ukubwa wao huko waendako umepata kilema. Ambao maisha yao yamewekwa njiapanda.

Kitendo cha watoto wa umri mdogo tena wajawazito wapatao 255 kuhudumiwa katika hospitali moja, kina kishindo kisicho cha kawaida katika jamii husika.

Kishindo kinatokana na ukweli kwamba kwa kipindi hicho cha 2007 – 2008, idadi ya watoto waliopata ujauzito wilayani Liwale inaweza kuwa hata zaidi ya mara nne au tano ya idadi iliyopatikana.

Kwa nini? Kwa sababu takwimu zilizopo ni kutoka hospitali moja. Kuna hospitali nyingine, vituo vya afya na zahanati wilayani. Kuna wakunga wa asili vijijini au familia ambamo “watoto” wamejifungua salama na bila msaada wa kitaalam. Idai yaweza kuwa kubwa zaidi.

Tufuatane na taarifa ya mwandishi kutoka Liwale ambaye ananukuu muuguzi mkuu: “…Wanaenda kutoa mimba kienyeji …kwa kujichokonoa na vijiti. (Wazazi) wanawaleta hospitali wakiwa wanavuja damu nyingi lakini tunajitahidi kuokoa maisha yao.”

“Wanaookolewa” ni wale waliofika hospitalini. Ni wangapi walijichokonoa kwa vijiti, wakavuja sana, wakapoteza damu nyingi na kufia kwa waganga vijijini?

Ni wangapi wamefia nyumbani kwa wazazi wao wakiwa wanajifungua kutokana na wazazi, ama kuwa mbali na hospitali, au kutoamini hospitali, au kufikiria kuwa watatozwa fedha wakati wao hawana chochote?

Wangapi wamekufa wakiwa wanatoa mimba au kutokana na matatizo mbalimbali ya ujauzito lakini hawajaripotiwa kufa? Wangapi wametelekezwa na wazazi wao kwa madai ya “kuwaaibisha” na sasa hawajulikani iwapo wako hai au wamekufa?

Wangapi wamepata matatizo ya ukosefu wa chakula (achana na chakula bora), mahali pa kuishi na kukosekana utulivu wa moyo hadi ujauzito kuharibika na hivyo afya zao kutetereka na wengine kupoteza maisha?

Watoto hawa wa umri mdogo hawajaolewa. Wamevamiwa na kubakwa na wanaume nyumbani kwao, njiani, vichakani, shuleni, kwenye nyumba za kulala wageni na kokote walikopelekwa kwa tendo la ngono.

Ni huzuni iliyoje kusikia kuwa kati ya watoto wajawazito 130 waliopelekwa hospitalini Liwale mwaka jana, ni 13 tu ambao walijifungua kwa njia ya kawaida.

Wengine, kutokana na viungo vyao kuwa vichanga na hivyo kushindwa kuhimili kazi kubwa ya kujifungua, ilibidi wapewe msaada wa nyongeza ikiwa ni pamoja na upasuaji mdogo.

Hilo ni janga la Liwale. Lakini ni janga la taifa zima. Halihitaji kufumbiwa macho. Linaambatana na janga jingine la ubakaji. Wabakaji wamevuka mipaka. Wanabaka watoto na kuwaingiza katika hali ya familia wakiwa bado hawajajitambua.

Ukiangalia umri uliotajwa wa kati ya miaka 12 na 15, utakuta ni umri wa kwenda shule. Hapa, ama kuna ukatili mkubwa wa kuwabaka watoto kwa nguvu au hakuna mazingira muwafaka – shuleni na nyumbani – kiasi kwamba ubakaji unafanywa kwa njia ya vishawishi.

Mathalani, shule zisizo na walimu au zenye walimu wachache; zisizo na madawati, vitabu na vifaa mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia; zisizo na mafunzo ya nyongeza kwa yale ya darasani; zinaweza kuwa mahabusi ambamo watoto wengi watapenda kuasi au kushawishiwa kuasi.

Shuleni ambako hakuna shughuli za kuimba, midahalo, kucheza michezo mbalimbali kama mpira, kikapu, tenesi, kukimbia, kuruka, kuvuta kamba na michezo mingine ya riadha, ni mahali pa kuchosha pasipokuza akili na pasipo vishawishi vya kusoma.

Mahali ambako ufundishaji ni ule wa kukaririsha na siyo kufikirisha kwa njia ya kushirikisha wanafunzi kutafuta majibu na ufumbuzi, panaweza pia kuzaa tabia ya kukata tamaa na kuogopa kwenda shule; hivyo kunufaisha wabakaji.

Aidha, umasikini uliokithiri katika kaya, ambako wazazi wanamwambia mtoto wa kike asiwaulize kitoweo “kwa kuwa amekua,” unaweza kuchochea mazingira ya kubakwa wakiwa na umri mdogo.

Lakini ubakaji pia unaweza kushamiri kutokana na ujinga wa wazazi na wanafuzi. Ni kwa kiwango gani elimu ya uzazi imetolewa kwa wazazi na watoto tangu wakiwa na umri mdogo?

Kinachotendeka Liwale kipo kila wilaya nchini. Watoto wa kike wanaingizwa katika maisha ya familia kabla ya muda wao – “mtoto amezaa mtoto.” Katika hali hii, maisha ya kichanga na “mtoto-mama” yanabaki mashakani.

Serikali ina jukumu la kuwahakikishia watoto wa kike ulinzi wa haki zao zote za msingi kuanzia uhai na elimu.

Serikali haina budi kutafuta kiini cha tatizo hili – mazingira ya kiuchumi na kijamii ambamo ukatili huu unafanyika – na kutafuta ufumbuzi wa kudumu Liwale na nchini nzima. Kusubiri ni kuongeza tatizo na hata vifo.

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya Tanzania Daima Jumapili, 16 Novemba 2008)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
Powered by Blogger.