Header Ads

LightBlog

UDINI, UDINI TANZANIA




Serikali inapoeneza udini 'kwa wimbo'

KUNA mazingaombwe mapya. Yote kutoka serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni haya: Serikali inataka Wakristo na Waislamu kukaa meza moja na kutafuta “suluhu.”

Serikali haisemi ni suluhu ipi. Inabwaga jumlajumla tu kwamba kuwepo na “mapatano.” Mapatano yapi? Yalikuwepo? Tangu lini? Yametoweka? Tangu lini? Yalikuwa yameletwa na Wakristo au Waislamu? Nani ameondoa mapatano au mwafaka?

Hii basi ni mara nyingine serikali inashindwa kazi yake; inapuuzia kazi yake; inakwepa kazi yake; inazembea kazi yake; badala yake “inatafuta mchawi” au mahali pa kuegesha lawama.

Serikali ilipoua wananchi katika maandamano huko Zanzibar (2001), iliharakisha kutangazia dunia kuwa ni “kutokana na mgogoro” kati ya CCM na Chama cha wananchi – CUF.

Wakati huo CUF haikuwa serikalini. Ilikuwa asasi ya kijamii kama nyingine. Vilevile, CCM ilikuwa asasi ya kijamii ingawa ndiyo inaunda serikali. Ili kupunguza makali ya “serikali kuua,” watawala wakajenga hoja ya kwamba migogoro na vifo ni kutokana na vyama viwili vya siasa.

Hapa ndipo serikali ilitaka mjadala kati ya CCM na CUF badala ya serikali iliyoua kukubali kosa, kuomba radhi na kufanya mabadiliko ya kuleta amani – kwa njia ya kuwaacha wananchi wakajieleza kwa kuandamana na kupinga wasichokitaka na kueleza wanachokitaka.

Niliwahi kuona mambo kama haya wakati wa uenyekiti wa Augustine Mrema katika chama cha NCCR-Mageuzi. Wakati huo CCM ilijinyakulia fursa ya kutangaza kile ambacho Mrema alitaka; shabaha ikiwa kubomoa chama kipya.

Siku zote Mrema alipiga kelele kuwa Katibu Mkuu Mabere Marando alikuwa anaharibu chama, anajali wasomi peke yao, anataka kumpindua (wakati ni Marando aliyemwachia uenyekiti), anakula fedha za chama; anafanya ushushushu (wakati Mrema naye alipitia mafunzo ya chekechea ya ushushushu).

CCM walipoona Mrema amewapa kianzio wakamuunga mkono; wakatembeza kampeni kubwa kuwa NCCR-Mageuzi kulikuwa na mgogoro kati ya Mwenyekiti Mrema na Katibu Mkuu Marando. Hilooo! Likavuma.

CCM na Mrema walijua walichokuwa wakifanya: Kuondoa fikra za wananchi kwenye kitu halisi kilichokuwa ndani ya NCCR-Mageuzi na kufanya “tatizo kuwa ugomvi kati ya Mrema na Marando.”

Ni wakati huo niliandika kitabu, “Hatma ya Mageuzi Tanzania,” nikieleza kwamba tulikuwa na mwenyekiti mwenye ugonjwa wa “kisukari cha siasa” kilichopenda kuimbwa, kusifiwa, kuabudiwa na hatimaye ni Mrema aliyesema kuwa yeye ni mtawala wa chama na kwamba akisema geuka ugeuke, akisema inama uiname.

Niliandika kuwa sisi wengine tuliamua kutoinama. Tukasema ataondoka kwa vyovyote vile. Aliondoka. Hapana. Aliondoshwa. Kitabu kingine kinakuja juu ya Historia ya Mageuzi na kitamweka pazuri katika mwelekeo wa kumpinga kwelikweli – kupinga udikiteta; na sisi kupigania haki na uhuru ndani ya chama cha siasa.

Hiyo ni mara nyingine ambapo watawala walipata mwanya wa kupakazia; kuunga mkono ushetani wa mtu mmoja; kusakizia wasiohusika na kubomoa misingi ya umoja na haki katika asasi changa.

Leo serikali inataka Wakristo na Waislamu wakutane “ili kumaliza mgogoro kati yao.” Mgogoro upi ambao serikali inaufahamu na iko wapi historia yake?

Hapa kuna serikali. Angalau iliundwa na kutangazwa, hata kama haionekani kufanya kama wananchi wengi walivyotarajia.

Ni serikali inayopaswa kusimamia usajili wa madhehebu mbalimbali nchini. Ni serikali inayojua vema sheria za usajili na uendeshaji madhehebu. Serikali haipaswi kujua maungamo, sala wala swala katika makanisa au misikiti; lakini inajua jinsi asasi hizo zinavyopaswa kujiendesha ili kukidhi kile zilichookusudia.

Mara zote serikali hujigamba kuwa ni “mkono mrefu.” Nadhani ni sikio refu pia na jicho refu. Sharti ione anayekwenda kinyume au aliyelalamikiwa kwenda kinyume. Hii yetu bilashaka ina sikio fupi, jicho fupi na mkono mfupi au uliokatwa.

Katika hili la Wakristo na Waislamu serikali inaonyesha inashindwa kazi yake; inapuuzia kazi yake; inakwepa kazi yake; inazembea kazi yake; badala yake “inatafuta mchawi” au mahali pa kuegesha lawama.

Sasa serikali inataka Waislamu na Wakristo wakutane kujadililiana na kutafuta ufumbuzi wa “mgogoro” wao. Mgogoro upi? Serikali ina wataalam katika nyanja mbalimbali. Je, imewatumia na kuona waumini hawa wana mgogoro gani?

Inachofanya serikali ni kuongelea “mgogoro” kila uchao. Tukio la kuchoma makanisa linaitwa “mgogoro kati ya Wakristo na Waislamu.” Madai ya kukojolea msahafu yanaitwa mgogoro kati ya Wakristo na Waislamu.

Mihadhara ya kutukana madhehebu mengine; jambo ambalo linaweza kuitwa uchokozi au makusudi maalum ya kuinua, kuibua na kusambaza chuki; badala ya kuonekana kinyume cha sheria, inaitwa migogoro kati ya Waislamu na Wakristo.

Majibizano juu ya nani achinje ng’ombe au mbuzi au kuku (na siyo nguruwe), nayo yanaitwa mgogoro. Leo rafiki yangu anayefanya biashara ya kupiga muziki kwenye sherehe na yeye ni Mwislamu, ananiambia kuwa sherehe nyingi ni za Wakristo lakini sasa hawamwaliki tena. Atakufa njaa.

Hii haiwezi kuwa migogoro kati ya Waislamu na Wakristo. Hapa kuna ukosefu wa utawala. Wanaopaswa kusimamia sheria, taratibu na kanuni ama wana maslahi katika vineno na ugomvi mdogo utakaozaa ugomvi mkubwa na hata vita na maafa; au ni wapumbavu tu wanaochezea “shilingi chooni.”

Hapa amekosekana mtumishi wa umma – serikali – anayejali maisha ya mmoja na wengi pia. Amekosekana mwenye upeo wa masafa kugundua kuwa kile ambacho serikali inaita migogoro ya waumini, ni migogoro kati ya serikali yenyewe na wale inaopaswa kutumikia – umma.

Matumizi ya kauli za kutaka waumini wa madhehebu fulani ndio wapigie kura mgombea fulani kama ilivyoonekana (CCM) katika uchaguzi mkuu 2010 na uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka juzi, hayaonyeshi ujinga wala upumbavu wa wanaotumia dini, bali yanathibitisha kutokuwepo utawala.

“Acha nifanye hili. Hakuna wa kunigusa.” Na kweli wanafanya. Na kweli hawaguswi. Na hali inaendelea kuwa ileile. Serikali inalialia: Wakristo, Waislamu malizeni migogoro yenu. Serikali yenyewe haimo! Migogoro ipi? Na kadri serikali inavyotaja migogoro inakuwa hakika inapandikiza migogoro.

Hivi inaachia hali hii ili iweje? Ili watawala waweje? Ili huko tuendako kuweje? Na wao watakuwa wapi?

Mwisho


No comments

Powered by Blogger.