Header Ads

LightBlog
MTWARA: Changanoto ikiwa koroma hugeuka tatizo

Kilichopo Mtwara, siyo maasi. Wananchi na wakazi wa Mtwara wanaasi nini na nani? Kilichopo Mtwata ni vuguvugu la wananchi kuwaambia watawala kuwa kinachofanyika sicho. Tena wanafanya hivyo kwa kuwakilisha wananchi wengine pote nchini ambako mazingira kama yanayoonekana Mtwara yameleta dhiki kuu kwa wengi na hata vifo.

Kumwaga askari polisi mjini Mtwara na mkoa mzima; kuwaongezea askari wa Jeshi la Wananchi (JW); kufunika wananchi kwa mabomu ya machozi, kufyatua risasi za moto, kuua mama mjamzito kwa risasi moto; kujeruhi, kukamata wananchi kutoka majumbani mwao na kuwalundika mahabusi - yote haya hayawezi kuwa suluhisho. Wala siyo majibu kwa vuguvugu. Hapana!

Imefikia wakati vuguvugu linaanza kuleta fafanuzi kali na kakamavu. Kwenye mitandao mkononi, na hapa naripoti, kuna kirefu cha Mtwara kama kinavyosambazwa:
M - Maarifa
T - Tunayo
W - Wazawa
A - Amkeni
R - Rais
A - Ametusahau

Nani ameandika au nani amewaandikia? Ubunifu huu hauwezi kupuuzwa au kudharauliwa. Hauwezi pia kuzimwa kwa mabomu ya machozi, kamatakamata na hata mauaji ya raia. Yuko wapi mtu wa nje (ya nchi) anayechochea wananchi kuandika haya?

Kilichoko Mtwara ni vuguvugu la kutoa tahadhari kwa watawala, kwamba yaliyotokea kwingine nchini yasitokee Mtwara. Ni hivi: Kila palipopatikana madini nchini, watu walihamishwa; mali zao zilichukuliwa au kuharibiwa; wengine wanatajwa kufukiwa wakiwa hai ndani ya "migodi" - mashimo waliyochimba kwa mikono. Ni vilio vya miaka mingi. Jinsi machozi yanavyoendelea kuwatiririka; ndivyo dhahabu, almasi, tanzanite na madini mengine yanavyozidi kutiririkia mikononi mwa wanaoitwa wawekezaji. Hakika hawa ni wawekezwaji.

Itashangaza kila mmoja mwenye akili timamu iwapo serikali itashindwa, itakataa, itadharau kukaa chini na wananchi na kuwaambia; na hata kuwaeleza kwa maandishi - kwamba kuna mikataba hii hapa - iwe wazi na kuonyeshwa kwa wawakilishi wao bungeni; kuna mafao haya - na wao wajue watanufaikaje; kuna sera au tupe maoni ya sera ya uchimbaji gesi - ndipo iendelee kutekeleza miradi yake.

Kwani miardi hii ni ya nani na kwa faida ya nani? Kama ni kwa faida ya wananchi na wananchi wanataka kujua mafao yake kwao, kwanini wasiambiwe na hata kushirikishwa kikamilifu katika kuweka vipaumbele vitakavyotumia mafao hayo?

Katika baadhi ya nchi, serikali zimejipangia, kwa mfano: Mapato yote kutokana na dhahabbu yatakwenda kwenye hudumia ya wajawazito na watoto. Mapato yote kutoka almasi, yatakwenda kwenye elimu ya msingi (darasa la kwanza hadi 14). Mapato yote kutoka tanzanite yatakwenda kuhudumia elimu ya juu. Mapato yote kutoka gesi asilia yatakwenda (eneo jingine kwa manufaa ya umma kwa ujumla).

Utawala nchini hauna mipango ya aina hii. Mtasomewa tarakimu walizotaka kusoma na hutajua kipi kimetumika wapi na kiasi gani. Na kama kuna usiri tangu mwanzo, bila kujua mikataba inasemaje na mavuno yatakuwaje; basi kila mmoja anaona "sasa tumeliwa." Dhabu iliyoibwa na kampuni ya Meremeta kwa ushirikiano na wanasiasa, haitafahamika; bei waliyouzia haitatajwa. Walionufaika hao ndio kitendawili. Ni vitu jumlajumla tu. Kiza.

Kitu kimoja hakiwatembelei watawala akilini. Ni kwamba miongoni mwa askari wanaokwenda kukamata, kupiga, kulipua mabomu na wakati mwingine kuua; kuna watoto, ndugu na jamaa wa wazazi, ndugu na marafiki wa wanaodai kupewa maelezo juu ya gesi na vipi watafaidika nayo. Matokeo yake ni nini huko tuendako?

Lakini ni kweli serikali inahitaji msaada wa mawazo kuhusu hili? Kama inauhitaji, kwanini haiutafuti? Ni huu hapa: Wape wananchi taarifa wanazotaka. Washirikishe katika maamuzi. Washirikishe katika kujenga miradi. Washirikishe katika kulinda miradi hiyo. Tatizo liko wapi?



Serikali isikubali kufanya changamoto kuwa tatizo; linaweza kuishinda kulimaliza.

mwisho

No comments

Powered by Blogger.