Header Ads

LightBlog

KILIO CHA WANANCHI, WAANDISHI KUTESWA, KUUAWA


Usalama wa Mwandishi wa Habari Tanzania
Na Ndimara Tegambwage*

Mada iliyowasilishwa kwenye Mkutano Mahususi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jumanne, 14 Mei 2013 jijini Dar es Salaam. Mkutano ulileta pamoja waandishi wa habari, wanachama wa asasi mbalimbali, vyama vya siasa na watendaji serikalini. Huu ni mkutano wa kwanza nchini kujadili “Ongezeko la Ukatili wa Vyombo vya Dola na Wahusika Kutowajibishwa.”
Utangulizi
INGAWA kila mtu ana haki ya kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake,[1] kwa njia ya kutamka au hata kuandika; hapa tunajadili mtu mwenye ujuzi (na uzoefu) katika kazi ya kutafuta, kupokea, kuandaa na kusambaza taarifa na habari. Tunajadili mtu huru, mkweli, anayekuwa mahali husika, kuona, kusikia, kunusa, kuhoji, kuandika kwa usahihi na kwa kuzingatia misingi ya taaluma yake; na kusambaza taarifa au habari alizokusanya kupitia chombo chake au kile kilichomwajiri – Mwandishi wa Habari
Huyu ni mtafutaji, mwaminifu kwake na anaowaandikia, asiyehongeka, papo kwa papo au kwa ahadi; anayeandika habari za matukio zenye kina au zile za kuchunguza, kufukua na kuanika; mchambuzi mwenye kuweka bayana – kwa shabaha ya kufikirisha – hali na matukio katika muktadha wa mazingira yaliyopo, huku akisadiki kwamba shabaha yake ni kuleta au kuongeza ufahamu mpana na maarifa kwa mtu mmoja na mmoja jamii. Ni huyu ambaye huipa jamii kile kilichofichwa au kilichofichika; kuitafunia kilicho kigumu; kuichambulia chenye utata; na kutokana na maoni na matakwa ya anaowaandikia, hupata uwezo na uhalali wa kushiriki kujenga ajenda mwafaka kwa mabadiliko ya jamii yake. Ni huyuhuyu ambaye huitwa mwandishi wa umma ingawa, na hata kama yumo katika ajira binafsi au ya umma. 

Lakini katika miaka ya karibuni, kumekuwa na mwelekeo wa kuwinda mwandishi hata yule ambaye hajafikia viwango vilivyotajwa hapo juu. Pale ambapo pamekuwa pagumu kwa wawindaji kuhonga, kutishia na kulemaza, basi wameua. Hali hii imefinyaza uwanja, uwezo na kupokonya uhuru wa mwandishi katika utendaji wake wa kazi. Ni katika mazingira haya, Leonid Zagalsky[2] aliandika, “…iwapo hakuna wa kulinda waandishi wa habari, nani atalinda demokrasia?” 

Ushahidi hai mkononi
Picha ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, akisulubiwa kwa kipigo na hatimaye kulipuliwa kwa bomu na kubaki minofu mitupu akiwa mikononi mwa polisi wenye silaha, katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, haitatoka haraka vichwani mwa waandishi: Mauaji ya mtu ambaye hakuwa hata na wembe mfukoni, isipokuwa kidaka picha na sauti! Alikuwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten. Aliuawa tarehe 2 Septemba 2012. Mpigapicha Joseph Camilius Senga wa TanzaniaDaima, ambaye alinasa picha za mateso ya Mwangosi hadi kuuawa, anasimulia kuwa polisi walikuwa wakikusanya vipande vya mwili wa Mwangosi kwa kutumia ngao walizobeba.[3] Mwangosi na wenzake walikuwa wakifuatilia ufunguzi wa ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo; chama kikuu cha upinzani nchini.

Maiti ya mwandishi na mchapishaji wa gazeti la Kasi Mpya, Richard Massatu iliokotwa eneo la Igoma, jijini Mwanza (2011). Macho yalikuwa yametobolewa na mguu wa kushoto na mbavu vikiwa vimevunjika. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama wa taifa katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.

Baada ya kutoonekana nyumbani kwa siku tatu, maiti ya mwandishi Issa Ngumba wa Redio Kwizela iliokotwa tarehe 3 Januari mwaka huu (2013) katika pori la kilima Kajuruheta, sehemu ya kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.

Mbali na mauaji, kumekuwa na mashambulizi kwa waandishi mmoja mmoja. Kubenea na mshauri wa habari Ndimara Tegambwage, walivamiwa ndani ya chumba cha habari cha MwanaHALISI tarehe 5 Januari 2008. Kubenea alipigwa na kumwagiwa tindikali machoni na mwenzake alikatwa kwa panga kisogoni alikoshonwa nyuzi 15. Kubenea alilazwa Muhimbili ambako Rais Jakaya Kikwete alikwenda “kumjuliahali” kabla ya kupelekwa India kwa uchunguzi zaidi na matibabu.

Uchunguzi umeonyesha kuwa walioshambulia Kubenea na Tegambwage waliongozwa na Ferdinand Mwenda (au Ferdinand Msepa au Fredy) aliyetajwa kuwa “ofisa wa kada ya kati” wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) mwenye umri upatao miaka 30 (wakati huo) ingawa wakati wa kesi, polisi waliendelea kumwita “mfanyabiashara wa Ilala” jijini Dar es Salaam. Tangu alipokamatwa hajawahi kurudi na kuishi katika banda lake la vyumba vitatu lililoko Mtaa wa Bethlehem, Tegeta Machakani, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Waulize waandishi wa habari Mussa Juma (Mwananchi), Ramadhan Mvungi (Star TV), Jason Patinkin, anayeandikia Shirika la Habari la Ujerumani na gazeti la The Guardian la Uingereza; Elia Mbonea  (Mtanzania), Khalfan Liundi (ITV) na Aristide Dotto wa Channel TEN, juu ya kilichowakumba mapema Aprili 2013. Jason alikamatwa na polisi na kuhojiwa kwa saa sita kabla ya kuachiwa. Waandishi wengine walitimuliwa na polisi wakati wakitafuta maoni ya wakazi wa Loliondo juu ya hatua ya serikali kupokonya sehemu ya wanachoita “ardhi yetu ya miaka yote” na kuiweka chini ya mwekezwaji, Ortelo Development Compay (OBC) ya Nchi za Falme za Kiarabu (Hapa tunatumia neno “mwekezwaji” kwa makusudi. Amewekezwa kwenye mbuga na wanyamapori waliolindwa na Wamasai kwa miaka yote. Hana anachoongeza kwenye mbuga wala wanyamapori! Anavitumia kufanya biashara).

Wasikilize akina Mpoki Bukuku, mpigapicha wa Mwananchi, Christopher Kidanka, Heri Makame na wengine, ambao walipigwa na askari wa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam. Waandishi walikuwa Ukonga kushuhudia, kwa niaba ya umma, jinsi askari walivyovamia nyumba za wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), kutoa mali zao nje na kuingia kwa nguvu kwa madai kuwa askari hawakuwa na nyumba za kutosha. Kamera ya Bukuku iliharibiwa.

George Marato (ITV), Athuman Hamis, Hamad Tambo na Said Msonda (NIPASHE), Florian Kaijage (wakati huo Channel TEN) na wengine, walikamatwa na polisi (mwanzoni mwa 2005) katika kijiji cha Korotambe, kata ya Mwema, wilaya ya Tarime katika mkoa wa Mara na kushikiliwa kwa zaidi ya saa 15 wakihojiwa “kwanini mnavunja amri ya mkuu wa wilaya, Paschal Mabiti ya kutokwenda katika eneo hili.” Waandishi walikuwa wakienda kuchunguza na kuandika kiini cha mapigano kati ya koo za Wanchari na Waryanchoka.

Muulize Erick Nampesya (sasa BBC) na waandishi wengine watatu wa hapa nchini waliokamatwa na polisi katika vijiji jirani ya mgodi wa dhahabu wa North Mara. Walikwenda kutafuta ukweli juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kutolipwa fidia kwa ardhi na mali iliyokuwemo ambavyo vilichukuliwa wakati wa upanuzi wa eneo la mgodi. Ilikuwa miaka minne iliyopita.

Beldina Nyakeke (The Citizen), Mabere Makubi (Channel TEN – sasa ITV), Anna Mrosso (NIPASHE), na Anthony Mayunga (Mwananchi) walikamatwa na polisi mapema mwaka jana, katika kijiji cha Nyakunguru karibu na mgodi wa North Mara. Waliwekwa rumande kituo cha Nyamwanga, Tarime, kuhojiwa na kuachiwa baada ya saa saba. Waandishi walikuwa wakifuatilia taarifa za polisi kuua wananchi karibu na mgodi na kutupa maiti zao barabarani huku wakidai wamezipeleka kwa jamaa zao kwa mazishi. Waliachiwa kwa dhamana lakini tangu hapo hawajaitwa tena Nyamwanga.

Absalom Kibanda, mhariri mkuu mtendaji wa New Habari Media Group – kampuni inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, The African na Dimba ambaye pia ni mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, alivamiwa na kundi la watu, tarehe 5 Machi mwaka huu. Akapigwa. Akachokonolewa jicho. Akachomolewa kucha. Akakatwa kidole. Akang’olewa meno. Akatupwa nje ya lango la nyumba yake, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kwa madai mbalimbali, Richard Mgamba (sasa mhariri The Guardian on Sunday) alitishiwa kuuawa, akapingwa kwa maandamano mjini Mwanza (2006) na kuitwa “Mkenya” aliyestahili kufukuzwa nchini. Mwandishi wa kujitegemea Erick Kabendera anatishiwa kufukuzwa nchini baada ya wazazi wake walioko Bukoba kuhojiwa mara kwa mara na watu wanaojiita “wanausalama” kwa madai kuwa siyo raia. Charles Misango (TanzaniaDaima) ameripoti nyumba yake jijini Dar es Salaam kuzengewa na watu asiowajua hadi usiku wa manane au alfajiri. Kuna wakati analazimika kulala kwa ndugu zake au hotelini. Mhariri Mtendaji wa TanzaniaDaima, Ansbert Ngurumo amezuliwa kifo kupitia mitandao ya kijamii. Jenerali Ulimwengu, Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema Company Limited  (wachapishaji wa Raia Mwema) na mwendeshaji wa kipindi maarufu cha televisheni, “Jenerali On Monday” (Channel TEN), aliwahi kutishiwa kufukuzwa nchini, wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa kwa tuhuma za kutokuwa raia.

Ushahidi ni mwingi. Tunahitaji kuwa na kitabu kinachotokana na uchunguzi wa kina, ambacho kitaorodhesha waandishi wa habari, yaliyowapata, lini, wapi na katika mazingira yapi, ili kutambua kazi zao za hadhi ya kipekee na kuonyesha wanaoingia katika uandishi sasa kuwa hii si “kahawa au chai,” bali utumishi wa umma unaohitaji stadi, mbinu, kujituma, uaminifu na ujasiri.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua hapa kwamba baadhi ya matukio katika mshololo huu, kwa taarifa zilizopo, yanafanana kwa mbinu zilizotumika. Tukio la MwanaHALISI linafanana na yale ya Absalom Kibanda na Richard Massatu. Matukio haya matatu yanafanana pia na lile la utekaji na utesaji wa Dk. Steven Ulimboka.[4]

Je, watawala wanayaona haya?
Ni muhimu kujua iwapo watawala wanayaona haya. Kama wanayaona wamechukua hatua gani? Hebu tujaribu kutafakari kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya tarehe 7 Januari 2008. Alikuwa hospitali ya taifa ya rufaa, Muhimbili jijini Dar es Salaam alikoenda “kumjulia hali” Saed Kubenea, mwandishi na mchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI[5] aliyevamiwa ndani ya chumba cha habari, kupigwa na kumwagiwa tindikali machoni. Akiwa ubavuni mwa kitanda cha mwandishi, Kikwete alinukuliwa akisema, pamoja na mengine, “…waandishi waendelee kutimiza wajibu wao kwa kuchukua tahadhari ya kutosha.”[6] Kesho yake, kipindi cha waigizaji kwenye televisheni kiliigiza “waandishi” wakiwa wamevaa helmeti – kofia kama za wapanda pikipiki.[7] Mchora katuni katika gazeti moja alionyesha waandishi wakiwa wameingiza vichwa kwenye madebe. Tahadhari!

Kauli ya rais yaweza kuwa ushauri au maelekezo ya kuchukua tahadhari za kila aina. Kwa mfano, kukaa na silaha kibindoni, kuwa na walinzi, kuepuka kuandika habari zinazoweza kukera marafiki zake, wabadhilifu, wanaovunja misingi ya utawala bora, wakwapuzi, wezi, mafisadi na wahujumu uchumi wanaoweza kutaka kulipiza kisasi. Kauli yaweza pia kuwa na maana kwamba “ukiona mezea,” bila kuandika; au yaweza kuwa inaelekeza kuweka chini zana za kazi ya uandishi au kuacha uandishi wa aina fulani, na kujisalimisha kwa wale wanaoudhika kutokana na kile unachoandika.

Je, ushauri huu waweza kuwa ni kukiri pia kwamba wanaozuia waandishi wa habari kufanya kazi zao, wanaovamia vyumba vya habari na kuwadhuru na wanaowaua,  wanamzidi nguvu rais na serikali yake; na hivyo amebaki kulialia na kuwageukia waandishi kwa kauli ya “…kuwa makini na kuchukua tahadhari zaidi?” Hakika msimamo huu wa rais – kwa kujua au kutojua, kwa makusudi au kwa utuki tu – ni wa kukana waandishi na kuwaongezea   nguvu wanaowatesa na hata kuwaua.

Mazingira ambamo usalama unapotelea
Matendo mengi yaliyolenga kuwanyamazisha waandishi, kuwajengea woga na hata kuwaua, yamekuja katika kipindi cha matukio makubwa nchini, kwa mfano, kashfa za ukwapuaji mabilioni ya shilingi kutoka BoT kwa kutumia kampuni feki hata halali;[8] kupotea kwa Gavana Daudi Balali – aliyepaswa kuwa mtuhumiwa Na. 1 wa wizi katika BoT – ambaye inadaiwa alikufa na kuzikwa Marekani kama “mjusi wa dawa” – bila hata picha (wakati waliokwenda “msibani” Dar es Salaam walikuwa na kadi za mwaliko); kupatikana na kujadiliwa kwa taarifa za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kuthibitisha wizi wa moja kwa moja wa mabilioni ya shillingi serikalini; serikali kushindwa kutumia mabilioni ya shilingi kutoka nchi wahisani na hivyo kusababisha miradi kukwama;[9] kuongezeka kwa viroja vya mishahara hewa ya wafanyakazi serikalini, kashfa ya ununuzi wa rada ambamo viongozi na watendaji serikalini wametajwa kupewa mlungula ili Tanzania iuziwe chombo hicho kwa bei karibu maradufu; kashfa ya mkataba wa Richmond iliyomg’oa Edward Lowassa kutoka nafasi ya waziri mkuu; kutotolea maelezo madai makubwa ya wizi na ukiukaji maadili ya uongozi, kwa mfano, kunyamazia waliotajwa kushiriki kashfa ya rada, kuficha fedha katika mabenki ya nchi za nje; serikali kukataa kutoa hadharani majina ya wezi lunkunku waliokwapua mabilioni ya shilingi BoT na baadaye kukaa na serikali kukubaliana kurejesha sehemu ya kiasi walichoiba.

Katika kipindi hiki wakulima wameendelea kukopwa mazao – kahawa, korosho, pamba kwa miezi mingi kabla ya kupata malipo; wafugaji wameendelea kufukuzwa kila walipoenda wakiambiwa “rudi kwenu” ambako serikali, ama imeuza, kumilikisha watu wengine au kuwapa wawekezwaji; kumekuwa na ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya wananchi, kati ya wananchi na wawekezwaji na kati ya wananchi na serikali; kushuka au kumomonyoka kwa imani ya wananchi kwa polisi (kwahiyo kwa serikali) kulikodhihirishwa na wananchi kupiga na kupigana na polisi huko Biharamulo na Masasi; kuibuka kwa makundi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM); kujitokeza kwa nguvu kwa vyama vya siasa – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) ambavyo vimetikisa mizizi ya chama kilichopanga ikulu; wabunge kuzuiwa kujadili mambo makubwa ya kitaifa,[10] wizi wa mitihani, ushirikina[11] kuingia ikulu, uchochezi wa udini kuwekewa mbolea na ikulu,[12] matumizi ya Jeshi la Wananchi (JW) kwa shughuli za polisi mitaani na kuongezeka kwa idadi ya vijana wasio na elimu, wasio na kazi na wasio na matumaini ya maisha bora katika nchi wanayoita yao.

Ukizingatia yote haya, waweza kufikia hitimisho kwamba utawala umetota na uhalali wake unamomonyoka kwa kasi. Waweza pia kuwa na maoni kwamba, ama kutokana na viongozi kuwa na maslahi katika uhalifu, kushiriki uhalifu; au kwa baadhi yao kuwa sehemu ya tasnia ya uhalifu, basi wamefungwa mikono, miguu na akili. Hawawezi kutenda. Haya ndiyo mazingira ya kichaka ambamo kila mtuhumiwa au kila mwizi anaunda mbinu za kutofahamika au kutofahamika zaidi; au za “kulipiza kisasi” kwa aliyeanika uhalifu wake. Kwa upande wa waliomo serikalini, yote haya yanafanywa bila woga wa kuchukuliwa hatua kwa kuwa serikali imejikinga nyuma ya sheria ambazo tayari ziliishatamkwa kuwa hazifai; na ama zifutwe au zifanyiwe marekebisho makubwa.[13] Hazijafanyiwa lolote.

Nani adui wa mwandishi

Katika mazingira ya ukimya na uchovu wa utawala, ambamo rais anakiri kuemewa na kushindwa kulinda waandishi isipokuwa kuwaambia “…kuchukua tahadhari;” na kwa kuwa rais anaogopa kiti chake na kusema hadharani kuwa ameombewa itikafu ili afe; na kwa kuwa  serikali hadi sasa imehifadhi sheria nyingi za kukandamiza mfumo wa kukusanya, kupokea na kusambaza habari; na kwa kuwa serikali inatumia uongo[14] na mabavu kunyamazisha waandishi na hivyo kupokonya haki ya wananchi ya kupata taarifa na habari; na kwa kuwa serikali inaendelea kunyima haki ya kuwasiliana kwa kuchelewesha na hata kusitisha usajili wa magazeti bila kutoa sababu za maana;[15] na kwa kuwa serikali inanyamazia wale wanaoingilia kazi ya waandishi; kwahiyo basi, serikali ichukuliwe kuwa adui Na. 1 wa waandishi makini. Tutajiuliza zaidi iwapo, katika mazingira haya, adui wa mwandishi siyo adui wa umma!

Wanasiasa wanaonyukana ndani ya chama chao, wakisutana kwa kipindi kirefu na kuitana kila jina chafu katika mbio za kutafuta urais au “utukufu” mwingine kisiasa, nao ni adui wa mwandishi anayeanika udhaifu wa utawala ndani ya serikali na vyama. Ni hawa wanaoweza kuomba na kupata ushauri wa waliosomea kuua, ili kuajiri vikundi vya mauaji vya kuangamiza waandishi ndani ya vyumba vya habari na makazini kwao; na hata wananchi ambao hawakubaliani na mwenendo wa wa vyama vyao au serikali.

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya, wezi, wakwapuaji na mafisadi, katika mazingira ya kutota kwa utawala, wanaweza kujichukulia madaraka – wakakemea serikali, waziwazi au kimyakimya, huku wakijua viongozi watafyata; na wakati huohuo kuzuia taarifa zao kuchapishwa au kutangazwa, kwa kuhonga waandishi, na hasa wahariri; au kuamua kuondoa roho ya mwandishi mmoja mmoja ili kutengeneza blanketi la woga kwa wote.

Mwandishi adui wa Mwandishi
Ni muhimu kutaja hapa mtu anayeitwa mwandishi wa habari asiye mwaminifu kwa taaluma yake; aliyezoea au kuzoezwa kuitwa, kutumwa, kulipwa ujira mbali na apatacho kwa tajiri wake, ili kuchokonoa wenzake au wengine na kwa maslahi ya aliyemtuma. Huyu ni kauleni ambaye amechukua sura na tabia ya ombaomba. Amegeuza wakuu wa wilaya, mikoa, polisi, usalama wa taifa, mawaziri, wahalifu na watuhumiwa kuwa ATM – anachomeka ombi; anachomoa fedha au fadhila. Anahatarisha, siyo maisha yake peke yake, bali hata yale ya familia yake, wenzake na familia zao.[16] Huyu ndiye anaelekeza maadui kule ambako waandishi wenzake wanaishi, wanakutana, wanakunywa; na nani wanampenda. Hivyo, wale ambao amekuwa “akichomoa,” kwa kuwa nao ni mafisadi, wakitaka kumwondoa ili kufuta ushahidi aliochuma wakiwa katika vikao vya siri, watanyemelea hata marafiki wake, kuwajeruhi au hata kuwaua. Uchunguzi bado unaendelea kuhusu kifo cha mwandishi John Lubungo wa ITV kinachohusishwa na madai ya mahusiano yake ya “kibiashara” na wenzake.[17] Huko ndiko tunaita kupigana vita visivyo vyako. Kupigana vita usivyojua. Au, ndiko kuwa mhanga wa utawala uliotota.

Nimeongoza waandishi wa habari mara mbili kwenda maeneo ambako kuna wafugaji – Kilosa na Loliondo. Huko Kilosa (Mei 2009) tulikuta wizi wa aina yake. Viongozi wa kata wakishirikiana na wale wa wilaya, wanatoza wafugaji Sh. 500 hadi 2,000 kwa ng’ombe mmoja kwa madai ya kumkuta “katika eneo lisilohusika kwa ufugaji.” Wanakusanya mamilioni ya shilingi. Wengine wanabana wafugaji kwamba lazima wauze mifugo yao huku tayari malori ya wanunuzi waliopanganao yakirindima. Kila ng’ombe anauzwa kwa Sh. 50,000 hadi 80,000. Wanachuma kifisadi kwenye mgongo wa wafugaji.

Waandishi waliandika uporaji huu; kutokuwepo mipango ya kutenga au kugawa ardhi kwa wakulima na wafugaji na mengine mengi. Waligundua mkurugenzi wa halmashauri alikuwa anamiliki eka 10,000 katika eneo ambako wanadai hakuna ardhi ya kutosha. Walimwabia. Aling’aka. Waliandika. Lakini baada ya wiki tatu, wakapelekwa waandishi wengine kuandika kinyume cha yaliyoripotiwa; waking’ang’ania kuwa ardhi ni ndogo, mifugo mingi na wafugaji ni “wakorofi.”

Tulikwenda Loliondo (Novemba 2009). Kule Wamasai wameishi na wanyamapori kwa miaka nendarudi. Ukitaka, waweza kusema ndio walinzi wa wanyamapori. Hawali nyamapori isipokuwa mifugo yao. Tukakuta polisi wamechoma maboma yao (nyumba, maghala ya vyakula, mabanda ya mifugo na maeneo ya matambiko). Mwekezwaji hataki kuona Mmasai akikatisha. Anatumia polisi – “walinzi wa raia na mali zao(?),” kuchoma nyumba za raia na mali zao.

Wiki moja baada ya waandishi kuripoti kile walichoona ambacho hasa ni kashfa kwa watawala na nchi, kampuni ya mwekezwaji ikaita waandishi kwa posho nono. Wakaandika kinyume cha yale yaliyoripotiwa awali. Ndivyo ilivyokuwa. Kuna waandishi walioteguka na wanaoweza kununuliwa kwa bei wanayotaja wenyewe. Hili bado ni tatizo kubwa. Linaondoa usalama wa mwandishi. Linawapa matumaini watu wachafu kwamba wanaweza “kusafishwa” kwa kalamu ya anayeitwa mwandishi.

Wapo wanaoandika kijuujuu tu; bila kina, bila vyanzo makini, bila maelezo kamili, bila kutoa mwanga. Wanaandika vitu ambavyo havifikirishi. Ni muziki kwa waliogharamia; kama anayelipa mpiga zomari. Pengine mwizi ameitwa “mjasiriamali aliyefanikiwa;” fisadi ameitwa “mwenzetu;” aliyejiuzulu ameitwa “aliyestaafu,” na rojorojo nyingi za aina hiyo alimradi wamelipwa fedha au fadhila. Hawa nao wamemomonyoa usalama wa mwandishi kwa kuwa wamesaliti ukweli uliopaswa kuwa ngao yao. Huwezi kuwategemea.

Ujinga na usalama wa mwandishi
Usalama wa mwandishi unapotea na kupotelea pia katika ujinga. Wengi hawasomi. Hawaongezi maarifa. Niliowahi kuwa nao darasani watakumbuka nikiwaambia kuwa “…mwandishi wa habari ni kuku wa kienyeji” – anajitafutia; na siyo broila anayepelekewa kila kitu na hata kuwashiwa taa ndipo ale na kunywa. Ukosefu wa moyo na juhudi ya kutafuta maarifa unasukuma waandishi wengi katika “ubroila.” Wanasubiri kupewa. Wasipopewa wataomba. Wakiomba na kupewa wanatumika kama vitimbakwira. Wataangamiza usalama wetu sote – kwani wanaowapa sumu – iwe ya kuwaua au kuwaacha zezeta – wanakuwa wamejiridhisha kuwa hakuna waandishi tena.

Usalama wetu unapotea pia pale baadhi ya waandishi wanapojiingiza katika kudai kuwa “Mhimili wa Nne wa Dola.” Huku ni kuacha jukumu kuu la kuandika habari, kuweka wazi kila kinachotendeka na kwa maslahi ya umma, kupaza sauti za wananchi juu ya matakwa yao na wanachotarajia. Ni kuacha kusimama na umma, kuchunga na kuhakiki serikali/utawala na mihimili mingine ili utendaji wake ufanane na utambuzi na matarajio ya jamii. Watawala wakiona ubwege huu, wanafurahi; wanatupa vyeo vya utawala ili tutumike kuziba hata mianya michache iliyokuwepo ya mwandishi makini kupata habari na kufanya uchambuzi mwanana. Kinachofuata ni kwamba, uandishi hauwi mhimili wa nne au hata kivuli chake; na wala kilichopo hakikidhi matakwa ya nadharia tu ya kuwa mhimili wa nne.

Hitimisho: Ulinzi wa tuendako
Waandishi, mmoja mmoja hawawezi kujilinda. Wanahitaji nguvu na sauti ya pamoja. Siyo sauti ya pamoja ya waandishi peke yao; bali pamoja na sauti ya jamii inayoelekezwa kwa watawala ikisema, “sasa inatosha.” Sauti ya pamoja inayoiambia serikali kwamba, kushindwa kulinda waandishi ni kushindwa kulinda raia wote; kwahiyo kama imeshindwa wajibu huo, basi haistahili kuwepo. Na ili jamii ifikie hatua hiyo, sharti iwe imetambua umuhimu wa mwandishi kupitia kile anchoandika.

Je, kinachoandikwa kinaipa jamii ukweli na kuiongezea maarifa? Kinaiondolea ukungu wa jana na kuweka ubayana wa leo? Kinaiondolea woga na kuipa ujasiri wa kuhoji watawala wao? Je, kinaiunganisha na sisi na katika mwelekeo mmoja? Kinaweza kuipa matumaini kwamba waandishi ni wa kutegemea katika safari ya kuleta mabadiliko inayotaka? Kama jibu ni ndiyo, tukikamatwa watapaza sauti. Vyombo vyetu vya habari vikifungiwa watataka vifunguliwe. Tukiuawa watafukuza kazi viongozi wa serikali; kwani sisi ni watumishi wao. Inawezekana.

Mwisho

*Ndimara Tegambwage ni mwandishi wa habari kwa miaka 40+ sasa. Ni mwandishi wa zaidi ya vitabu 20 vikiwemo Duka la Kaya, Who Tells The Truth In Tanzania, Uhuru wa Habari Kitanzini, Uhuru Gerezani (Siku 90 za kufungiwa MwanaHALISI), Ndiuliza na Siyo Mwisho wa Maisha. Hivi sasa ni mshauri wa kujitegemea wa mambo ya habari na mawasiliano; mwezeshaji katika asasi mbalimbali zenye uhusiano na vyombo vya habari; mwezeshaji katika uandishi wa habari za uchunguzi; menta (mwelekezaji) wa waandishi katika vyombo vya habari na mmoja wa waelekezaji katika Jukwaa la Waandishi wa Habari za Uchunguzi Afrika (FAIR) yenye makao makuu Johannesburg, Afrika Kusini.




[1] Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na Ibara ya 19 ya Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu.
[2] Bulletin of the Atomic Scientists (Julai 28, 2005): Makala “Censorship by Death: Murders of Russian investigative journalists  (Udhibiti kwa njia ya kifo: Mauaji ya waandishi wa habari za uchunguzi nchini Russia).”

[3] You-Tube - http://www.youtube.com/watch?v=TKBU7hZ1WJI – Mahojiano ya Senga na waandishi wa habari wa TanzaniaDaima, 12 Aprili 2013 wakati wa mafunzo ya ndani juu ya “Jinsi ya kufanya mahojiano.”
[4] Dk. Ulimboka alitekwa 26 Juni 2012; akapigwa, akang’olewa meno na kucha na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande yapata kilometa 45 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam. Alikuwa kiongozi wa madaktari waliogoma ili “…kushinikiza kuwekwa mazingira bora ya kazi katika hospitali za serikali.”
[5] Gazeti la kila wiki ambalo serikali ilifungia kwa muda usiojulikana tangu 30 Juni 2012.
[6] TanzaniaDaima, 8 Januari 2008 (msisitzo wa mwandishi).
[7] Kikundi cha Ze Komedi katika ITV.
[8] Kampuni za Meremeta, Deep Green, Kagoda, Mwananchi Gold Ltd. Kagoda ilichota zaidi ya shilingi bilioni 40 zinazodaiwa kutumika katika uchaguzi uliomwingiza ikulu Rais Kikwete.
[9] Mwananchi, 15 Aprili 2013: Hizi ni fedha kutoka Japan, Ireland, Muungano wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Maendeleo na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
[10] Kwa mfano tu: Mgogoro wa madaktari na serikali wakidai mazingira bora ya kazi; Utekaji Dk. Steven Ulimboka; Sakata la kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
[11] Sheikh Yahya Hussein (2010) alionya wanaotaka urais kupitia CCM kuwa watakufa na kwamba “…ikulu inalindwa  kwa majeshi yasiyoonekana (majini).”
[12] Ikulu, Dar es Salaam, katika hotuba ya mwezi kwa taifa, 1 Aprili 2013, Rais Kikwete alisema misikiti mitatu imemwombea “itikafu” (dua mbaya) ili afe kwa madai kuwa anapendelea wakristo.
[13] Sheria zilizotajwa na  Tume ya Rais ya 1992 iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ni pamoja na Sheria ya Magazeti (1976) na Sheria ya Usalama wa Taifa (1970) ambazo serikali inaegemea katika kukandamiza haki ya uhuru wa maoni na kujieleza.
[14] The Zimbabwean, Ijumaa 29 Machi 2013: Rais Kikwete aapa kutofungulia MwanaHALISI “…kwa kuwa limechochea jeshi kuasi.” Habari hii iliandikwa pia na HabariLeo, Tanzania. Gazeti linalokabiliwa na kesi ya “uchochezi” ni TanzaniaDaima na siyo MwanaHALISI.
[15] Barua ya Idara ya MAELEZO ya 28 Machi 2013 kwa baadhi ya wamiliki wa magazeti, inasema serikali imesitisha usajili wa magazeti hadi Julai mwaka huu.
[16]ndimara.blogspot.com – shairi kwa Itika, mke wake Daudi Mwangosi. Mauaji yalimgusa, siyo yeye peke yake, watoto wake, ndugu na marafiki na raia wema.
[17] Lubungo aliuawa 12 Februari 2008 katika eneo la Mahenje wilayani Mbozi, yapata kilometa 75 kutoka Mbeya mjini. Inadaiwa aliambiwa kuna “habari motomoto” mpakani Tunduma; lakini alipofika Mahenje, gari lake liligongwa, akatolewa nje ya gari na kukatwakatwa mapanga. Taarifa zinasema hata abiria wake (mwanamke) aliuawa palepale. 

https://www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.