Header Ads

LightBlog

Shairi: LINI TUTASEMA SASA BASI?


 MCT YAJADILI 
UKATILI TANZANIA

Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jumanne, 14 Mei 2013, lilifanya Mkutano Mahususi ukishirikisha Jopo la Magwiji la asasi hiyo, jijini Dar es Salaam. Mkutano ulileta pamoja waandishi wa habari, wanachama wa asasi mbalimbali, vyama vya siasa na watendaji serikalini.

Huu ni mkutano wa kwanza nchini kujadili “Ongezeko la Ukatili wa Vyombo vya Dola na Wahusika Kutowajibishwa.”

Kwenye mkutano huo, mwanahabari na mwenyekiti wa Bodi ya gazeti la RAIA MWEMA, Jenerali Ulimwengu aliwasilisha Mada Kuu juu ya ukatili wa vyombo vya dola huku watendaji wakiondoka bila kuchukuliwa hatua.

Prof. Bonaventura Rutinwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwasilisha mada juu ya “Maana na Matumizi ya Sheria ya Kutoripoti Mashauri yaliyo Mahakamani” na Ndimara Tegambwage aliwasilisha juu ya “Usalama wa Waandishi wa Habati Nchini.”

Prof. wa sheria, Issa Shivji alisambaza kwa wote waliohudhuria, “kielekezi” kilichofanyiwa uchunguzi juu ya ukatili uliokithiri nchini na kuonyesha kuwa walioutenda hawakuchukuliwa hatua.

Hapa chini ni shairi lililotungwa na Ndimara Tegambwage ambalo lilisomwa na Prof. Penina Mlama, likiwa sehemu ya ufunguzi wa Mkutano Mahususi.



LINI TUTASEMA SASA BASI!

Siiiiiiiiiiiiiii!`
Wasikie wakisema
Na hata kujinoma
Bila aibu!
Bila woga wa kukamatwa
Bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa
Bila woga wa kusutwa!

Ati nini? Eeh?
Wapi? Lini?
Amekufa? Ameuawa?
Oooh!

Si yule bwana mdogo;
Yule pale barazani
Anauza karanga na bisi?
Risasi imemtua mgongoni
Lakini ni bahati mbaya!
Ati ililenga waandamanaji
Lakini yenyewe ikachagua yeye?
Oooh!

Na mmoja ni mmoja
Ni uhai mwanana
Na wengi ni mmojammoja,
Mmoja hapa, mmoja pale
Ni mmojammoja wengi:
Makumi, mamia, maelfu, mamilioni
Nchi yawa uwanja wa maangamizi!

Yametokea Arusha
Wakasema bahati mbaya
Yakajirudia Morogoro
Vifo ni bahati mbaya
Yalitokea Unguja na Pemba
Sasa yashamiri mijini na vijijini:
Sikiliza: twaambiwa bahati mbaya.

Siiiiiiiiiiiiiii!
Ni bahati mbaya kuua juzi  
Ni bahati mbaya kuua jana
Ni bahati mbaya kuua leo
Itakuwa bahati mbaya kuua kesho!
Basi na ije sheria
“Bahati mbaya!” kuhalalisha.

Ni bahati mbaya kuua mmoja
Ni bahati mbaya kuua watano
Ni bahati mbaya kuua watano mara tano;
Bali watasema, bila aibu
Bila woga wa kukamatwa
Bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa
Bila woga wa kusutwa!

Penye upenyo wataimba
Ilikuwa bahati mbaya
Penye utata na malengo
Watadai “majambazi”
Wasonaswa na mitego-gumba;
Na intelijensia watachomoza
Kwa uchunguzi usoisha.

Siiiiiiiiiiiiiiii!

Siyo mtu tu afaye
Kuna mali na fedha
Na hata mtima wa umma.

Sikilizeni uporaji
Kihenge kikuu cha umma
Wao waita taasisi;
Ni kuchovya na kuchomoa,
Ni kuchovya na kuchomoa
Wanakula hadi ukoko –
Halafu nini?
Mkuu anapotea
Mkuu anaugua
Mkuu anakufa
Na kufukiwa kama mende –
Hakuna mwakilishi.

Siiiiiiiiiiiiii!
Walokwapua naye wa hai
Wendelea kutumbua.
Waloidhinisha wizi wangalipo
Kuziba mifereji ya taarifa
Na bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa

Ya mikataba ni mfano
Hata uwani kusainia
Manono wampa wakuja
Wenyewe wapewa makombo
Jeuri yajaza kifua
Madudu kufunika
Hapa chini “funika”
Hapa kati “funika”
Hapa kati kabisa “funika”
Bungeni, wizarani na ikulu –
Bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa

Mazingaombwe tumeona
Funga kazi ya wizi
Kwa watunza mali ya umma.
Wamekana, wametuna
Wamefura kwa hasira:
Hapana! Si kweli! Waongo nyie!
Mchuzi ulipokolea mbiombio Ulaya
Ati “chenji” kuchukua
Bila aibu, bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa

Wanaona wanohini
Wanatulia tuli,
Mithili ya maji mtungini.
Wanyama waibwa hai
Nao wang’ata ulimi;
Ardhi ya wenyeji yaporwa  
Kwa mwekezwaji kukabidhiwa.
Haki, uhuru vyaporwa
Mbele ya macho yao:
Bila woga wa kukamatwa
Bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa

Siiiiiiiiiiiiiiii!
Useme lipi uache lipi?

Wizi uliokithiri vitengoni
Kwenye miji na vitengo vya majiji
Wenyewe waita mchwa; eti hakuna dawa
Wizi vitengo vya umma
Wenyewe wajitutumua kufidia.
Wanetu wala “unga,” wawa mateja
Wenyewe wajidai kuwa na yao orodha;
Wanasema wawapa muda kujisahihisha.
Hapa tulipo twazama.
Asiyeiba ni mpumbavu
Jizi ni mfano wa mafanikio.

Hakuna kilicho gizani
Ni kweupe pepepe!
Washika usukani wanaona na
Wenzao kushiriki
Ukimya umetanda
Utamaduni wa kutotenda:
Bila woga wa kushitakiwa
Bila woga wa kuadhibiwa

Siiiiiiiiiiiiii!
Lini tuseme sasa basi?

Mwisho
 https://www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.