Kilichoko
mahakamani
kinazungumzika,
kinaandikika
Ndugu zangu,
Nimekuwa nikieleza na hata kuelekeza, tofauti
na baadhi ya wenzangu katika uandishi, kwamba jambo lililoko mahakamani
linaweza kuandikwa. Kwa nini?
1.
Kwamba jambo liko mahakamani, hakuzuii mambo mengine kutendeka juu ya
hilohilo na nje ya mahakama. Dunia haisimami kwa kuwa jambo liko
mahakamani. Mwenendo wa kilichosababisha kuwa mahakamani hausiti au
kufutika eti kwa kuwa tayari kuna shauri mahakamani. Hamu na haki ya
kujua haviondoki eti kwa kuwa jambo liko mahakamani. Hapana!
2. Sheria
haikuzuii na hasa haipaswi kukuzuia kuandika mlolongo wa matukio nje ya
mahakama
unaohusu watu wenye shauri lililoko mahakamani. Matukio nje ya mahakama
yaweza kutoa nuru zaidi juu ya wahusika katika shauri na hata juu ya
shauri lenyewe. Taarifa juu ya matukio haya zaweza kuwa za msaada kwa wakili
wa utetezi na wakili wa upande wa mashitaka. Wakati zinaweza kumpa
mmoja nuru zaidi juu ya kilichotendeka, zaweza pia kumpa mwingine nuru
juu ya kujenga ngome.
3.
Hakimu au Jaji anahitaji hoja mshibano na ushahidi mwanana. Uamuzi wake
haupaswi kuongozwa au kutawaliwa au kufungwa na taarifa za magazeti,
redio, televisheni au chombo chochote kile cha kutoa taarifa au habari.
Umadhubuti wa hakimu au jaji; hekima, uaminifu wake kwake binafsi na kwa
kazi yake juu ya kesi iliyoko mbele yake, havipaswi kupanguliwa na
taarifa za nje ya hoja zilizoko mahakamani kwa madai kuwa "zimeathiri
maamuzi."
4.
Tuna ushahidi ambako baadhi ya mahakimu na majaji madhubuti wamepuuza
na kutupilia mbali madai ya kuathiriwa na vyombo vya habari wakiuliza,
"Una uhakika na unaamini kuwa mimi siwezi kufanya kazi hii; siwezi kuwa
na maoni na siwezi kuona haki mpaka niambiwe na vyombo vya habari?"
5.
Hili lina maana kwamba kupogoka; kuangalia sheria kwa makengengeza na
hata kutoa upendeleo wa waziwazi na uliofichika, ni shabaha, tena ya
makusudi, ya hakimu au jaji na siyo kuathiriwa na taarifa za chombo cha
habari.
6.
Twende kwa serikali. Taarifa ya serikali ambayo iliahidiwa; kama
ingekuwepo, isingeingilia shauri lililoko mahakamani. Haikuwepo au kuna
kilichoingia
katikati na kusababisha wasiitoe, ambacho ni wao pekee wanaokijua.
Kwamba serikali haitatoa taarifa kwa kuwa imegundua shauri lake na
madaktari liko mahakamani, ni sababu ya kizembe mno kutolewa na mamlaka.
Na kama serikali inaweza kusahau ilichofanya juzi tu, basi hii ni barua
kwa umma ya kuomba kuaga ikulu.
7.
Sheria haizuii wala kufunga, kwa mfano serikali, kutoka na taarifa
inayosema: "Tumepata fedha za kutosha. Sasa madaktari watalipwa nusu ya wanachodai. Hapa tutapata pa kupumulia na kuendelea na majadiliano." Sheria ipi itazuia hili. Sheria yaweza kununa iwapo serikali itatoka na kusema, "Mtakoma. Msimamo wetu ni uleule, liwalo na aliwe!"
8.
Hili halikubaliki mbele ya hekima, achilia mbali mahakama. Huwezi
kwenda mahakamani kuomba nafuu; ukarudi kesho yake kukaza nguvu ya amri
ya kukupa nafuu; na kesho yake ukatoka kifua mbele, kwa kutumia nafuu
ileile, kuwakomalia wale uliozuia, na isivyo haki,
lakini ilivyo halali kisheria. Utakuwa umetumia nguvu ya mahakama
kujinufaisha binafsi na utakuwa unajigamba kana kwamba umeweka "mahakama
mfukoni."
(Andishi hili lilitawanywa kwa wana-mabadiliko katika google proup, Alhamisi 28 Juni 2012. Ni sehemu ya mjadala uliohusu kushindwa kwa serikali kutoa taarifa iliyoahidi kutoa bungeni juu ya mgomo wa madaktari. Spika wa bunge Anne Makinda alisema serikali haitatoa tamko kwa kuwa kuna shauri mahakamani).
No comments
Post a Comment